RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

JIFUNZE KUJIONA VILE MUNGU ANAKUONA

Unajionaje? Tulia kwa muda na fikiria ni nini unawaza juu yako leo. Mara nyingi huwa tunajiona thamani yetu kama watu wanavyotuona badala ya jinsi Mungu anavyotuona. Unaweza kujiona hufai sababu ya makosa uliyoyafanya zamani au kujiona kuwa huwezi kufanikisha jambo lolote kubwa n.k. Haitupasi kufikiri namna hii bali tunapaswa kufikiria Mungu anatuonaje.

Unapoishi ili kufurahisha watu wengine na kuogopa watasema nini juu yako unakuwa unawapa watu nafasi ya kupanga thamani yako. Kuna wanawake wengine wanaishi ili kuwapendeza wazazi wao hata kama kwa kufanya hivyo wanamkosea Mungu na kukosa amani katika maisha yao. Wengine thamani yao inawekwa na mume / mchumba. Anashindwa kufanya jambo analolipenda ili kuleta mafanikio katika maisha yake na hata kuacha kuufuata mpango wa Mungu sababu anaogopa kuonekana chini / hafai na mume / mchumba. Ameacha maisha yake yaongozwe na mtu na kusahau kutafuta kujua Mungu anamuonaje. Na hata inafikia mahali mtu anaishi ili kuwependeza washirika wenzie kanisani au watumishi wa Mungu ili wamuone anafaa badala ya kuufuata mpango wa Mungu. Mtu anadiriki kuacha huduma / karama Mungu aliyompa na kufanya yale anayoona yanapata kibali kwa washirika wenzie ili aweze kuonekana wathamani mbele zao.

Ukweli ni kwamba, thamani yetu ipo ndani ya Yesu Kristo. Yesu alijitoa na kufa kwa ajili yetu maana anajua kuwa tu watu wathamani sana. Kwa kifo chake tumepata msamaha, upendo na ukombozi wa kweli. hatuhitaji kuwapendeza wanadamu ili tuonekane ni wa thamani maana Yesu alishamaliza yote msalabani.


1Petro 1:3-4 Asifiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema yake kuu ametufanya tuzaliwe upya ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kutoka kwa wafu; 4na tupokee urithi usioharibika, usiooza na usiochuja, ambao umewekwa mbinguni kwa ajili yenu.

Unaweza kujiona huna thamani sababu ya yale ambayo yalitokea katika maisha yako siku za nyuma. kama jambo linalokusumbua ni dhambi ya nyuma ambayo hujaitubia basi tubu na omba rehema za Mungu kisha uendelee mbele. Kama ni hali fulani ya manyanyaso au kuonewa uliipitia usikubali ikuharibie maisha yako ya sasa, makabidhi Yesu masumbufu yako yote na kataa hali yako ya nyumba kukusababisha kujiona hufai au huna thamani.

1Petro 1:6-7 6Furahini sana katika hilo, ingawa sasa kwa kitambo kidogo ni lazima mpate majaribu ya kila aina. 7Majaribu yataifanya imani yenu, ambayo ina thamani kuliko dhahabu, iwe imepimwa na kuthibitishwa kuwa ya kweli kama vile dhahabu ambayo ingawa ni kitu kiharibikacho, hupimwa kwa moto. Ndipo mtapata sifa, utukufu na heshima siku ile Yesu Kristo atakapofunuliwa.

Neema ya Mungu ni zawadi kwa wote wamwaminio. 1Pet 1:10. Ni neema ya Mungu inayotuponya na kutupa uhuru wa kuishi maisha mapya. Ni lazima tubadilishe fikra zetu na kuikubali neema ya Mungu. Tambua jambo linalokusumbua, Tafuta / Tafakari njia sahihi ya kukabiliana na jambo hilo na mkabidhi Mungu na endelea kukiri ushindi katika Yesu. Kila mara jione vile ambavyo Mungu anakuona, yaani mwenye thamani sana mbele zake. Yeremia 1:5, Mathayo 10:28-31, 1Petro 5:7

Inuka, Timiza ndoto zako maana wewe ni wa thamani sana.

Comments