RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA INAKUPA FAIDA SABA TU ZA KUJISOMEA VITABA NA NAKALA MBALIMBALI KATIKA MAISHA YAKO

Kupenda kusoma ni tabia nzuri ambayo kila mtu ni muhimu awe nayo. Tunalazimika kusoma kwasababu asili ya mazingira yetu kuna mambo mengi ya kujifunza licha ya matukio mengi ya kidunia yanayotokea kila siku. Ukiachilia mabadiliko ya kijamii (namna tunavyoishi), kiteknolojia, kisiasa na ya kiuchumi yanayotokea ulimwenguni bado kuna sababu ya msingi ya mtu kupenda kujisomea hata pale anapokuwa amemaliza masomo yake shuleni (vyuoni). Inapendeza na kuleta hamasa pale mtu anaposoma mambo ya kujiendeleza yeye binafsi kwaajili ya kujijenga na kuimarisha maisha yake mbali na vile vitu anavyosoma au alivyosoma darasani kama taaluma yake ya kikazi. Ikiwa bado unakuwa mzito katika kupenda kusoma zijue faida 7 za kupenda kujisomea na hakika utajifunza kitu kuhusu kusoma.
                          
                                                                              Rulea Sanga

1. Noa maarifa (panua ufahamu na uelewa wako) kwa kusoma

Usomaji wa vitabu utakufanya ujue mambo mengi katika mazingira yako. Hebu tafakari kama leo utasoma kitu fulani cha kukusaida au kubadilisha maisha yako, bila shaka utakuwa umeingiza kitu cha ziada katika maisha yako kwa siku ya leo.

Mfano: Kwa siku ya leo umesoma namna ya kumhudumia mtu aliyepata ajali (iwe ni ajali kazini, nyumbani, barabarani n.k)kwa kumpatia huduma ya kwanza. Kwa kujifunza namna ya kutoa huduma ya kwanza kwa mtu anayehitaji msaada utakuwa umesoma kitu muhimu sana cha kuweza kukusaidia popote pale na wakati wowote ule kwakuwa utakuwa unatambua na kufahamu nini cha kufanya. Kila siku soma chochote kile cha kukuongezea maarifa ya maisha na ipo siku utatumia ujuzi ulionao kujisaidia mwenyewe au mtu mwingine kutatua matitizo.

2. Kusoma kunaongeza utashi wa kutamka maneno vizuri

Unaposoma sana ndivyo unavyoona na kujua mengi, ni vigumu kwako kushindwa kusoma kabisa au kutamka maneno vizuri ikiwa unafahamu asilimia kubwa ya maneno. Kama wewe ni msomaji mzuri wa vitabu au unaperuzi sana kwenye mtandao wa intaneti utakuwa umesoma maneno mengi sana kiasi cha kuweza kutamka vizuri maneno mengi bila shida yoyote. Huwezi kuwa unafahamu maneno yote bali utajiongezea uwezo kutambua maneno na kukisia vizuri namna yanavyosomwa na kutamkwa. Fanya hivyo na utaongeza ujuzi wako wa kuongea na kusoma maneno vizuri.

3. Kusoma kunaongeza uwezo wa kuhifadhi kumbukumbu


Ukisoma na kuvutiwa na kitu ulichosoma bila shaka utahifadhi kumbukumbu akilini au kwenye karatasi ya kile ulichosoma kwa manufaa ya baadae. Ukiwa umesoma hadithi yenye mkasa wa kuburudisha, matukio yaliyotokea mahali fulani au historia ya kitu fulani, kumbukumbu hizo za kile ulichosoma zitahusisha mambo mengine ili uweze kukumbuka kitu chenyewe. Hivi ndivyo mfumo wa kumbukumbu unavyofanya kazi.

Mfano: Ili uweze kuvuta taswira ya hadithi uliyosoma kwenye kitabu fulani ni lazima utakumbuka picha ya kitabu chenyewe ndipo ukumbuke ndani mwa kitabu hadithi yenyewe ilikuwa inahusu nini. Ubongo unafanya kazi nyingi sana katika mwili wa mwanadamu, kwa kadri unavyojaza kichwa chako na mambo mengi mazuri ndivyo unavyoufanya ubongo uboreshe kumbukumbu halisi ya kile unachotaka ukumbuke.

4. Kusoma kunaongeza uwezo wa kufikiri


Unaweza soma kitabu chenye maelezo mengi ya kimafumbo au misamiati ya kukutaka kufikri ili uweze kuelewa, wakati ukiendelea kusoma utakuwa unajiuliza maswali mengi ni yapi majibu ya hicho unachosoma. Kwa kutafakari ili ufumbue kilichoandikwa utapanua fikra zako na hivyo kuongeza uwezo wako wa kutambua, kufahamu na kuelewa mambo kwa haraka. Faida moja wapo ya kuongeza uwezo wako wa kufikiri ni kuweza kutatua matatizo unayokumbana nayo katika mazingira yako kwa usahihi na ufanisi mkubwa.

5. Kusoma kunaongeza ujuzi wa kuandika vizuri


Ukiwa unasoma kila siku kwa walau dakika chache (dakika 15-30) tu iwe ni gazeti au jarida la habari, kitabu au kurasa kadhaa za tovuti mbalimbali kwenye intaneti, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuwa umesoma na kuona mengi. Unaposoma sana ndivyo unavyoongeza ujuzi wako katika kupangilia na kuandika maneno vizuri. Makala nyingi tunazosoma kwenye magazeti na tovuti za kuaminika kwenye mtandao wa intaneti zinakuwa zimeandikwa na waandishi au watunzi mahiri katika sanaa ya uandishi. Hivyo unaposoma kazi zao unajifunza mengi kuhusu namna ya kuandika na kupanga kazi zako za kimaandishi vizuri.

6. Kusoma kunapunguza msongo wa mawazo

Inaaminika kusoma kunaweza kukuchangamsha kwa kuhamisha mawazo yako kabisa na kufuatilia kile unachosoma kwenye kitabu kwa wakati huo.

Mfano: Ukichukua jarida la vichekesho, mkasa wa maisha wenye kukupa hamasa au kitabu takatifu cha kiimani (BIBLIA au QURAN TUKUFU). Kwa kadri utakavyokuwa unasoma na kujifariji ndivyo unavyokuwa unatuliza akili na kuwa katika hali ya amani na utulivu wa nafsi. Utakavyokuwa na utulivu wa nafsi na akili ndivyo utakavyokuwa na afya njema kwa kuondokana na maradhi kama ya kuathirika kisaikolojia, shinikizo la damu (blood pressure) nakadhalika.

7. Kusoma kuna burudisha
Inafurahisha sana kumkuta mtu anasoma gazeti akicheka kwa kuwa amefurahisha na kile anachosoma. Hadithi za kwenye vitabu, mashairi na vibonzo (katuni) vya magazetini na majarida mbalimbali ni baadhi tu ya viburudisho unavyoweza kusoma na kufurahi. Ulimwengu wa vitabu una mengi ya kusoma, kujifunza na kuburudika kazi ni kwako.

Comments