RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

ROSE MUHANDO MATUKIO YAKO YANAFUNDISHA NINI?

Muimbaji wa Injili asiyechuja Bongo, Rose Muhando.

KWAKO
Muimbaji Injili usiyechuja Bongo, Rose Muhando. Hongera kwa kumtumikia Mungu kwa muda mrefu, hakika kila mmoja anakutambua kwa uwezo wako mkubwa wa kuimba.

Nimekukumbuka leo kwa barua maana nimeshindwa kuvumilia mambo yanayoripotiwa kuhusu wewe. Tena bora ungekuwa raia wa kawaida kama nilivyo mimi, wewe ni maarufu, sijui kama unalitambua hilo.
Madhumuni ya barua hii ni kutaka kukukumbusha juu ya wajibu wako kama kioo cha jamii. Kupitia nyimbo zako, watu wengi wamepata kubarikiwa na kumrudia Mungu, sasa iweje uwe unawabadilisha watu wakati wewe mwenyewe hubadiliki?

Wimbo wa wewe kuchukua fedha na kutotokea kwenye huduma tumeuchoka! Hebu tubadilishie kidogo aina ya maisha yako. Unachukuaje fedha ya mtu kama huna uhakika wa kutokea kwenye hafla iliyokusudiwa?

Huoni kama unajiharibia heshima yako. Juzikati hapa tumesikia umeingia mitini katika uzinduzi wa albamu ya mwimbaji mwenzio, John Lissu uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, mara sijui umeko peshwa milioni moja hujazilipa, una mpango gani?

Kwa uzoefu wangu wa kwenye habari, imefika wakati hata nikiambiwa ishu yoyote ya wewe kuingia mitini na fedha, siku hizi wala sishtuki maana nimeshaanza kukuzoea.Nachelea kusema wanakuonea maana hata kama wewe ni mti mwema kiasi gani, haiwezekani kila siku uwe unapigwa mawe.

Kwa nini wasisemwe na wengine? Kuna kitu cha kujifunza na kukifanyia kazi haraka sana pindi utakapoisoma hii barua.Ni aibu kwa mwimbaji wa Injili mwenye taito kubwa kama yako kuwa na majanga kila kukicha. Utawafanya hata viongozi wa dini na jamii mbalimbali waogope hata kukualika katika matamasha au ibada zao wakihofia kupigwa changa la macho.

Nimeanza kufuatilia nyimbo zako siku nyingi, naamini kabisa kuna kitu spesho Mungu amekiweka katika ubongo wako kama njia mojawapo ya kuwakomboa watu mbalimbali wanaopatwa na majaribu mbalimbali katika maisha ya kila siku.

Nitumie fursa hii kukuomba sana, mama ubadili mwenendo wako na watu waweze kukuamini kama ilivyokuwa zamani enzi zile ambazo ndiyo ulikuwa unaanza kuwika kwenye muziki wa Injili. Yawezekana vitu vingine vinavyotajwa juu yako huwa vinazushwa lakini najua lisemwalo lipo, kuna madai mengi ya matukio ya hovyo dhidi yako ambayo hata nikiyataja hapa ni aibu kubwa.

Cha msingi nikuombe ubadilike, jisahihishe katika maeneo yote mabaya ambayo yanakushushia heshima yako uliyoijenga kwa muda mrefu.

Ni matumaini yangu utakuwa umenielewa.

Wasalaam,
Erick Evarist.

Comments