RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NABII YASPI BENDERA AFUNGUKA KWA KUONGELEA UCHAGUZI WA URAIS 2015

Stori: Chande Abdallah na Deogratius Mongela

NABII wa Kanisa la The Revelation lililopo Buza- Kipera jijini Dar, Yaspi Bendera ameibuka na kusema joto la uchaguzi mkuu ujao (2015) ni balaa kubwa kufuatia maono aliyopewa wakati akishiriki ibada katika nyakati mbalimbali kanisani kwake, Risasi Jumatano linakupa mkanda kamili.

Nabii wa Kanisa la The Revelation lililopo Buza Kipera jijini Dar, Yaspi Bendera.


Akizungumza wakati wa ibada kanisani hapo Jumapili iliyopita na baadaye na waandishi wetu, Nabii Yaspi alisema kuna mgongano mkubwa miongoni mwa watu wanaotajwa kugombea urais ili kumrithi Rais Jakaya Kikwete ‘JK’ ambaye alimwelezea kama kiongozi anayemuona kiroho mara kwa mara.


Mhe. Edward Lowasa.


“Nimemuona Rais Kikwete katika maono yangu kama mtu aliye kwenye vita kubwa ya kiroho, nikaandaa maombi hapa kanisani na tukamuombea kwa muda wa nusu saa, tunamshukuru Mungu hali yake inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa upasuaji wa tezi dume nchini Marekani.

“Lakini bado namuona akiwa na maumivu kuanzia sehemu za kiuno, uti wa mgongo hadi shingoni kwake. Hivi sasa ninapomuombea atasikia moto unawaka kupitia kwenye sehemu hizo na kuwa mzima kabisa.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.


“Tunamuombea baraka na uzima rais ili aweze kukabidhi madaraka vizuri kwa rais ajae,” alisema nabii huyo na kuongeza:

“Tulilazimika kumuombea rais ili asipatwe na madhara kwani kama asingefanyiwa upasuaji uliofana, huenda tungempoteza, hivyo wagombea urais kila mtu angefanya analotaka na kusababisha nchi kuwa na vurugu kubwa kuanzia sasa hadi mwakani.”

Waandishi wetu waliokuwa eneo la tukio walimshuhudia Nabii Yaspi akiwa ameshika picha ya rais na waumini wake wakizama katika maombi kwa ajili ya Rais Kikwete na walipomaliza kuomba, nabii huyo alisema tatizo lake limemalizika.

WAGOMBEA WENGINE
Kana kwamba hiyo haitoshi, Nabii Yaspi alisema anawaona kwenye maono yake baadhi ya wenye nia ya kugombea urais mwakani wanapita kwa waganga wa kienyeji ‘mlingotini’ kwa ajili ya ‘kupulizia’ lakini akasema hawatafanikiwa kwa kuwa yeye alishamwomba Mungu rais ajaye atoke kwake.


Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.


NJE YA KANISA
Nje ya kanisa, nabii huyo alizungumza na Risasi Mchanganyiko ambapo lilimuuliza kuhusu anavyoona mwelekeo wa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwakani.

Risasi Mchanganyiko: Vipi kuhusu ule utafiti wa ile Taasisi ya Twaweza ambao umewagawa wananchi?

Nabii: “Utafiti umefanywa vizuri na nadhani kila kitu kipo kama kilivyoainishwa, lakini kama walivyosema wenyewe kwenye ripoti yao, upepo unaweza kubadilika wakati wowote maana miujiza ya Mungu huja bila kutarajiwa.”


Wazari wa mambo ya nje Benard Membe.


Risasi Mchanganyiko: “Nani atashinda urais mwakani?”

Nabii: “Hivi unauliza swali kama hilo kweli wakati huu? Ripoti iliyotolewa imemaliza kila kitu na majibu yako wazi kabisa, labda huyo aliyetajwa aamue kupita njia zisizomfurahisha Mungu ili kuupata huo urais.”

TUJIKUMBUSHE

Utafiti uliotolewa na Taasisi ya Twaweza hivi karibuni ulisema kuwa endapo uchaguzi mkuu wa Tanzania ungefanyika hivi sasa, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa angeibuka mshindi, akifuatiwa kwa karibu na waziri mkuu wa sasa, Mizengo Pinda, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbroad Slaa akiibuka katika nafasi ya tatu.

Hata hivyo, wengine wanaotajwa kuwania urais mwakani ni January Makamba ambaye ni Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Mbembe, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, William Ngeleja na Emanuel Nchimbi.

Comments