RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ABARIKI KANISA LA KIASKOFU LA ROHO MTAKATIFU JIMBO LA KONDOA MKOA WA DODOMA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilali, akiwahutubia Waumini wa Dini ya Kikristo wakati wa sherehe za Kuweka wakfu, Kanisa la Kiaskofu la Roho Mtakatifu Jimbo la Kondoa zilizofanyika jana Desemba , 2014 Wilaya ya Kondoa Mkoa wa Dodoma.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akipongeza na Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kondoa, Bernadin Mfumbusa, baada ya kuzungumza na waumini wa kanisa la kiaskofu la Roho mtakatifu jimbo la Kondoa juzi.

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akiwa katika picha ya pamoja na Maaskofu na mashekh wa Wilaya ya Kondoa mkoa wa Dodoma baada ya kuzungumza na waumini wa Dini ya kikiristo jana.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Askofu mkuu wa Kanisa Katoliki Tanzania, Kardinali Polcarp Pengo, baada ya kumalizika kwa Sherehe za Kutabaruku kuweka wakfu na kubariki kanisa la kiaskofu la Roho Mtakatifu la jimbo la Kondoa iliofanyika wilayani Kondoa mkoa wa Dodoma jana.

Na Mwandishi Maalum - Kondoa

Serikali imewataka Watanzania kuwakataa na kuwakemea kwa nguvu zote watu watakaobainika kuvuruga amani nchini.
Akizungumza katika sherehe za kuweka wakfu Kanisa la Kiaskofu la Roho Mtakatifu Jimbo la Kondoa, mkoani Dodoma zilizofanyika juzi  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal amesema hatua hiyo itasaidia katika kuiwezesha Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani chini ya misingi ya upendo, umoja na mshikamano ulioasisiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

"Katika siku za hivi karibuni, zimeanza kujitokeza dalili mbaya za baadhi ya wenzetu ndani ya jamii kuanza kuchezea amani tuliyo nayo. Tunaona vitendo vyao, hata kusikia kauli zao," alidokeza Dkt. Bilal.
Makamu wa Rais aliwahakikishia waumini hao kuwa serikali inathamini amani na itaendelea kulinda amani ya Watanzania, kwa gharama yoyote na kamwe haitaruhusu mtu au kikundi chochote kile, kwa sababu na kisingizio chochote kuchezea na kuvuruga amani ya Watanzania.

"Tutatumia nguvu zote kuhakikisha Watanzania wanaendelea kuishi kwa furaha, bila vitisho vya usalama wa maisha na mali zao. Mkono wa sheria utamwangukia kwa kishindo, yeyote atakayebainika kuchafua amani ya wananchi wetu. Tutasimamia hili kwa ujasiri na hatutalegeza kamba," alisema Makamu wa Rais.

Dkt. Bilal aliwakumbusha viongozi wa dini wa madhehebu yote nchini kuzidi kuliombea amani Taifa kwani amani ni sharti la kwanza kwa maendeleo ya binadamu na hata vitabu vitakatifu duniani vinafundisha na kusisitiza amani kwa wanadamu.

"Nchi yetu imebarikiwa kuwa na amani, utulivu, umoja na mshikamano tangu tupate uhuru", alisema Dkt. Bilal na kuongeza "baraka hizi haziwafurahishi baadhi ya wenzetu, wanakesha kutuombea mabaya ili mradi tu, waone tunafarakana. Watu wa Mungu mna wajibu wa kupiga goti kila siku kuliombea Taifa letu. Amani ikitoweka hakuna pakukimbilia".

Aidha, Aliwakumbusha waumini wa dini zote nchini kwamba, kila mtu ana wajibu wa kuheshimu dini au imani ya mtu mwingine na kusema dini yoyote ya kweli, haichochei chuki wala vurugu.
"Napenda nitoe angalizo kwamba, ni marufuku na dhambi kubwa, kwa mtu au kikundi cha watu, kukashifu imani au dini ya watu wengine," alisema Dkt. Bilal na kusisitiza kuwa "dini zote ni njia tu tunazotumia wanadamu kwa lengo la kumuabudu Mwenyezi Mungu. Hivyo tofauti zetu za kuabudu na kiimani, kamwe zisitugawe".

Ibada ya kuweka wakfu kanisa hilo iliongozwa na Mhadhama Polycap Pengo na kuhudhuriwa na Maaskofu kutoka maeneo mbali mbali nchini, waumini na viongozi wa serikali.

Comments