RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

ESCROW: KKKT WAMCHARUKA JUU YA WANAOJIHUSISHA NA UFISADI WASIWEKWE VIPORO





Kanisa la kiinjili la Kilutheri dayosisi ya kaskazini (KKKT) limeitaka serikali isiache viporo katika kuwachukulia hatua za kisheria watumishi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya ya raslimali za taifa kwa manufaa yao kwa kuwa hali hiyo inawakatisha tamaa watanzania.

Rai hiyo imetolewa na askofu mteule wa kanisa hilo Dr Fredrick Shoo baada ya kusimikwa rasmi kushika nafasi hiyo kuchukua nafasi ya askofu Dr Martin Shao aliyestaafu katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi wa serikali na vyama vya siasa akiwemo mwenyekiti mtendaji wa makampuni ya IPP Dr Reginald Mengi.

Askofu Dr Shoo amesema, inasikitisha kuona bado kuna taarifa za kuenea kwa ufisadi mkubwa miongoni mwa viongozi wa serikali na baadhi yao wakionyesha ujeuri na ukakamavu huku viporo vikiendelea kukaa muda mrefu ambavyo mwisho wake kuwa sumu ambayo madhara yake ni makubwa kwa taifa.

Wakizungumza katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na waziri mkuu mstaafu Mh Edward Lowasa na kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni Mh Freeman Mbowe maaskofu Isaack Amani wa kanisa katoliki na mkuu wa kanisa la KKKT Dr Alex Malasusa wamesisitiza umuhimu wa kudumisha amani kuelekea katika matukio makubwa mawili mwaka huu ya kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

Katika hotuba yake iliyosomwa na waziri wa nchi ya rais utawala bora Mh George Mkuchika rais Kikwete amesema, serikali itaendelea kushirikiana na madhehebu ya dini kuboresha huduma za jamii ikiwemo sekta ya elimu ambayo imeanza kuleta mafanikio hasa katika shule za sekondari za kata.

Comments