RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MTOTO ALIYEBATIZWA PEKE YAKE AFANYA MAAJABU IKIWA NI PAMOJA NA KUPONA AJALI MBAYA YA MAFINGA MKOA WA IRING




Na Haruni Sanchawa
MTOTO Jacqueline Lepenza, aliyenusurika katika ajali mbaya ya basi lililogongana na lori huko Mafinga mkoani Iringa wiki mbili zilizopita, ameripotiwa kuwa na maajabu baada ya baba yake mzazi kujitokeza na kusimulia, Uwazi linakutaarifu.


Jacqueline Lepenza, akiwa na baba'ke.

Willy Lupenza, baba mzazi wa mtoto huyo mwenye umri wa miaka mitatu na nusu, alisema marehemu mke wake, Anjela Osward (35) (pichani) alikuwa amekwenda nyumbani kwao Ilembula mkoani Njombe kwa ajili ya ubatizo wa binti yao huyo.

Alisema katika hali ya kushangaza, siku ya ubatizo huo, Jacqueline alibatizwa peke yake pasipo watoto wenzake kupewa baraka hizo kwa sababu ambazo hazikueleweka.“Ndugu mwandishi, hili ni tukio ambalo sitalisahau katika maisha yangu, kwa sababu haiwezekani mtoto abatizwe peke yake halafu kwenye ajali, idadi kubwa ya watu wapoteze maisha lakini yeye anusurike.”

Alisema baada ya ajali, mtoto wake huyo alikutwa na watu waliojitokeza kuwasaidia majeruhi akiwa amelala juu ya bati la kuzuia matope kwenye tairi ya lori lililokuwa limebeba kontena huku akilia na matairi yakiendelea kuzunguka.

Alisema haelewi mtoto huyo alitokaje ndani ya basi hadi kwenye bati hilo la lori, kwani licha ya kukutwa mzima, lakini eneo hilo pia lilikuwa hatarishi kwa mwanaye ambaye alimpoteza mama yake aliyekuwa mmoja kati ya watu zaidi ya 50 waliofariki dunia.


...Akiwa na bibi yake.

Willy alisema Machi 11, mwaka huu alipata taarifa kwa njia ya simu kutoka kwa shemeji yake ambaye yuko mkoani Iringa kwa shughuli zake za kibiashara juu ya tukio hilo, baada ya yeye naye kuarifiwa na Jeshi la Polisi Iringa baada ya kuokotwa kwa simu ya mkewe.

Alisema baada ya kupigiwa na polisi waliofika katika eneo la tukio mapema, shemeji yake huyo alimpigia na kumjulisha juu ya mkewe kupata matatizo Mafinga.“Nilianza safari mara moja kuelekea huko, lakini nilipofika Morogoro nilipata taarifa za uhakika zilizoniaminisha kuwa mke wangu alikuwa amefariki dunia,” alisema.

Aliongeza kuwa aliendelea kufanya mawasiliano na ndugu kujua alipo mtoto, hadi alipoambiwa kuwa kulikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa wodini (Hospitali ya Wilaya Mafinga), hivyo akaambiwa kama anaweza kuwatumia picha yake kwa njia ya mtandao ili waweze kumfananisha.

“Niliwatumia picha kwa Mtandao wa WhatsApp, kumbe siku ya ajali mwanangu alikuwa amevaa gauni ambalo aliwahi kulivaa siku za nyuma, na ndiyo picha niliyowatumia, walimtambua kirahisi na alipofanyiwa uchunguzi wa kidaktari ikagundulika kuwa hakuwa na matatizo yoyote kiafya,” alisema baba huyo.


Mama wa Jacqueline, Anjela Osward enzi za uhai wake.

Kufuatia kufika Mafinga na kuutambua mwili wa mke wake, aliomba mwili huo kutopelekwa sehemu yoyote ili urudishwe nyumbani kwao Ilembula kwa mazishi yaliyofanyika katika Kijiji cha Mwambaga.Kuhusu hali ya mtoto kwa sasa, Willy alisema anaendelea vizuri na anamshukuru Mungu pamoja na madaktari na polisi walioshiriki katika tukio hilo ambalo mwanaye huyo alipona kimaajabu.

Ajali hiyo ilihusisha lori aina ya Scania namba T 689 APJ mali ya Cipex Company lililokuwa likiendeshwa na Maka Sebastian (26) na basi aina ya Scania namba T 438 CED mali ya Majinja lililokuwa likiendeshwa na Baraka Gabriel (38).

Comments