RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

ELIZABETH NGAIZA: HISTORIA YA PASAKA

Elizabeth Ngaiza mwimbaji wa nyimbo za Injili ambaye anatamba na albamu yake ya SEMA NAO BWANA ambayo inaweza kukutoa mahali fulani kiimani na kwenda hatua nyingi ya kimafanikio kama utachukua ujumbe aliouimba na kuufanyia kazi. Mwimbaji ambaye anasambaza kazi zake mwenye katika gari yake, amesema unaweza kumpata kwa kupiga simu +255 714 294 0716. Leo anataka kutujuza juu ya Historia ya Pasaka.

Elizabeth Ngaiza

Katika Biblia, Pasaka ilianza kwa mara ya kwanza katika kitabu cha Kutoka 12, tafadhali tenga muda ukisome kitabu hiki kizima. Katika Pasaka hii ya kwanza, wana wa Israel waliagizwa kupakaa damu ya kondoo kwenye vizingiti vya juu na miimo ya milango yao kabla ya Mungu kuleta pigo la kumi kwa watu wa Misri, ambalo lilikuwa ni pigo la kuwauwa wazaliwa wote wa kwanza wa Wamisri.

Mungu aliagiza WaIsrael wapakae damu hiyo kwenye milango yao ili Malaika atakapokuwa anapita kuwaua wamisri, asiwaue na WaIsraeli pia. Na Malaika alipokuwa akipita, aliwaua wazaliwa wa kwanza wa Wamisri, na aliacha kudhuru kila nyumba ya WaIsraeli, mradi tuu iwe imepakwa damu ya kondoo mlangoni.

Elizabeth Ngaiza

DAMU ILIKUWA YA LAZIMA
Katika Kutoka 12:23, inasema “BWANA apitapo katika nchi yote kuwapiga Wamisri, ataiona damu kwenye vizingiti na kwenye miimo ya milango naye atapita juu, wala hatamruhusu mwangamizi kuingia katika nyumba zetu na kuwapiga ninyi“. Jambo lililotakiwa hapa ili na Waisraeli wasipigwe, na wao kuweka damu kwenye milango yao. Bwana alichokuwa anaangalia si kuona kama nyumba fulani ni ya Muisrael au la, Yeye alikuwa anaangalia kama kuna damu mlangoni au la. Hii ina maana kuwa kama Mwisrael yeyote asingepakaa damu ya kondoo huyo katika mlango wake, angeangamia pamoja na Wamisri. Umeona msisitizo wa damu katika Pasaka hii ya kwanza? Na siku hiyo ndiyo siku ambayo wazaliwa wa kwanza wa Wamisri walikufa, na Waisraeli wote wakatoka utumwani Misri na kuanza safari ya kuelekea katika nchi ya Kaanani waliyoandaliwa na Bwana.

Na baada ya hayo, Mungu aliwaagiza WaIsrael kuiadhimisha siku hii daima na hata akasema “Watoto wenu watakapowauliza, ‘Sikukuu hii ina maana gani kwenu?’,Basi waambieni, ‘Hii ni dhabihu ya Pasaka kwa BWANA, ambaye alipita juu ya nyumba zetu alipowapiga Wamisri“(Kutoka 12:26-27). Kwa hiyo kuadhimisha Pasaka ni agizo la Mungu. Na pia Mungu akaendelea kusema “Kwa sababu BWANA aliutenga usiku ule ili kuwatoa Waisraeli katika nchi ya Misri katika usiku huu Waisrael wote wanapaswa kuadhimisha kwa kukesha ili kumheshimu BWANA katika vizazi vijavyo.” (Kutoka 12:42).

Hivyo ndivyo namna Pasaka ilivyoanza kwa agizo la Mungu mwenyewe, na ukisoma katika Kutoka 12, ndivyo ilivyoendelea kuadhimishwa mara nyingi katika kipindi cha Agano la Kale. Kuna wakati wana wa Israel walikaa muda mrefu sana bila kuadhimisha Pasaka, lakini kila mara alipoinuka mtu aliyeisoma sheria ya Mungu, walitubu na kuendelea tena kuadhimisha siku hii ya Pasaka.

Kwa siku ya leo nimeona nikukumbushe namna Pasaka ilivyoanza ili usiwe unaadhimisha Pasaka kwa namna ya mwili tu, bali uadhimishe Pasaka kuanzia moyoni. Na ikitokea umeulizwa na mtu asiyeamini au asiyefahamu, basi uwe tayari kumweleza kwa upole kuhusu Pasaka. Nitakuletea sehemu ya pili ya somo hili ili kujifunza zaidi pia.

Comments