RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SOMO: MAJESHI YA WAFU - ASKOFU GWAJIMA

Askofu Mkuu Dr. Josephat Gwajima wa GCTC

Luka 16:19 “Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula siku zote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.”

Kifo maana yake ni utengano kati ya mwii na Roho vinatengana. Kuna aina tatu za kifo:- aina ya kwanza ni kutengana roho na mwili, aina ya pili ni kule kutokumwamini Yesu Kristo na kumpokea kwenye maisha kama Bwana na mwokozi wa maisha yako (Efeso 2:1, 6). na aina ya tatu ya kifo ni kule kutupwa jehanamu ya moto.

Mtu anapokuwa amekufa hapa duniani huwa anachukuliwa na malaika na kupelekwa paradiso au kuzimu, tofauti inakuwa kama amempokea Bwana Yesu kwenye maisha yake na kuishi maisha matakatifu anachukuliwa na malaika watakatifu na kwenda mbinguni lakini kama amekufa dhambini bila kumpokea Bwana Yesu mtu huyo anachukuliwa na malaika walioasi (mashetani) na kupelekwa kifungoni Kuzimu. Kuzimu ni sehemu ya kifungo ambayo roho za watu ambao hawajamtii Mungu zinakaa huko. Kuzimu ipo hapahapa duniani katika nchi ndipo kuzimu ilipo.

Ufunuo 12: 7 “Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule Joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.”

Ufunuo 9: 1 “Malaika wa tano akapiga baragumu, nikaona nyota iliyotoka mbinguni, imeanguka juu ya nchi; naye akapewa ufunguo wa shimo la kuzimu. 11 Na juu yao wanaye mfalme, naye ni malaika wa kuzimu, jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kiyunani analo jina lake Apolioni.”

Kuzimu kuna mfalme wake ambaye ni malaika wa kuzimu aitwaye apolioni. Wale malaika walioasi mbinguni wote walitupwa kuzimu na mfalme wake ibilisi. Kuzimu ilitengenezwa kama kifungo(jela) na shetani ni mkuu wa jela hiyo ambaye hawaachi wafungwa wake waende zao.

Yuda 1:6 “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.”

Kuzimu watu huingia kupitia baharini, kwenye mashimo, maporini, maofisini, na nyumba za watu maeneo yote haya watu hupitia kuelekea kuzimu lilipo shimo kuu la ibilisi.

Tofauti kati ya kuzimu na Jehanamu.

2Petro 2: 4 “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu”

Kuzimu ni makao makuu ya serikali ya giza, ni makao makuu ya malaika walioasi, mashetani, ni sehemu ambayo wanakwenda watu wasiomwamini Bwana Yesu watendao dhambi. Pia kuna mashimo madogomadogo ya kuzimu yapo kila mahali hapa duniani, kwenye madaraja makubwa, baharini, maofisini, kwenye mapori, na sehemu nyingine. Kuzimu ni hapahapa duniani, ni gereza la kifungo. Kuzimu inaweza kuitwa moyo wa nchi, ina tumbo, mdomo, mikono. (Kuzimu hii ipo kwenye ulimwengu wa rohoni hapahapa duniani)

Kuzimu ni sehemu ambayo wale waliokufa katika dhambi wanapokwenda huko wanapoteza utashi wao (uhuru wao) sababu wapo kifungoni wanafanya mapenzi ya mkuu wa kuzimu ambaye ni shetani.

Zaburi 55:15 “Mauti na iwapate kwa ghafula, Na washuke kuzimu wangali hai, Maana uovu u makaoni mwao na katikati yao.”

Kundi la pili la watu wanaokwenda kuzimu ni wale wanaochukuliwa wakiwa hai au kwa lugha nyingine wanaitwa misukule ambao roho zao zinachukuliwa na kwenda kutumikishwa kufanya kazi mbalimbali sambamba na vipawa walivyopewa na Mungu. Na kundi la tatu ni wale watu wanaoenda kuzimu kwa maamuzi yao wenyewe kutafuta vitu mbalimbali kama mafanikio, fedha au umaarufu duniani. Watu hawa ni wasanii wa mziki wa kidunia, wanasiasa na hata baadhi ya wahubiri huenda huko kuzimu ili waweze kupewa uwezo wa kutambulika na dunia yote.

Zaburi 9:17 ”Wadhalimu watarejea kuzimu, Naam, mataifa yote wanaomsahau Mungu.”

kuzimu ndio chanzo cha hekima ya duniani ambapo watu wanaotaka umaarufu au utajiri hapa duniani wanashuka kuelekea huko ili wafanikiwe na kueleweka hapa duniani.

Mathayo 25:30 “Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.”

Mathayo 10:28 “Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.”

Luka 3:17 “ambaye pepeo lake li mkononi mwake, naye atausafisha sana uwanda wake, na kuikusanya ngano ghalani mwake, bali makapi atayateketeza kwa moto usiozimika.”

Ufunuo 20:13 “Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”

Kuzimu inaona kila kitu kinachoendelea duniani, tawala zote za duniani zinaongozwa kutokea kuzimu, Serikali zote za duniani na watu maarufu wote wa kimziki na kisiasa wanaongozwa kutokea pale na kama mtu anataka kupanda na kuvuma hapa duniani lazima aende kuzimu. Ndiomaana Hekima ya mbinguni ikitaka kushika falme na kuenea Duniani inapata upinzani mkubwa sababu ni Falme mbili zinakuwa zikipigana katika nchi moja lakini saa imefika kwa Falme zote za Duniani kugeuka na kuwa Falme za Mwanakondoo Yesu Kristo kabla hajarudi kuja kulichukua kanisa.

Maana ya majeshi ya wafu.

Kuzimu nguvu yake ni mashetani, shetani anatumia mashetani kuwateka wanadamu, Mungu hajawahi kumlaani Binadamu bali aliilaani ardhi. Mungu hapendi kumtesa mwanadamu na hivyo anampenda kila mwanadamu. 

Shetani anafahamu kwamba Mungu anampenda mwanadamu ndiomaana anatumia roho za wanadamu kutenda mapenzi yake hapa duniani kwasababu binadamu anamjua binadamu koo hadi koo. Anajua wanadamu akiwatumia kuwashughulikia wanadamu wenzao atafanikiwa sana. Wanadamu huwezi kuwateketeza au kuwauwa kwa jina la Yesu sababu wao ni roho zinazoshubiria hukumu na kukombolewa, Ipo damu ya Yesu ambayo inatuwezesha kujitenganisha nao wanadamu wanaotumiwa na shetani kama majeshi ya wafu kuja kutushambulia na kuzishinda kazi zao zote kwa jina la Yesu.

Majeshi ya wafu ni wanadamu waliokufa kwenye dhambi na wale walioibiwa na kutekwa (kufanywa mateka). Kuzimu hutumia silaha kubwa ya majeshi ya watu waliokufa dhambini ili kufanya vita na wewe. Vita uliyo nayo ni kwasababu ya jinsi ulivyo ndani yako, ni jinsi roho yako ilivyo, wanajua nia yako, wanajua nguvu yako na unaweza kuwafanya nini kwa nguvu ulizo nazo hapa duniani.

Ukiri:-
“Kwa jina la Yesu, majeshi ya wafu yaliyopangwa kinyume na mimi naamuru kuanzia leo yakose nguvu juu yangu kwa jina la Yesu”

1Samweli 28:3 “Basi Samweli alikuwa amefariki dunia, nao Israeli wote walikuwa wamemwomboleza, na kumzika huko Rama, ndani ya mji wake mwenyewe. Tena Sauli alikuwa amewaondolea mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi. Nao Wafilisti wakakusanyika, wakaenda kufanya kambi huko Shunemu; naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote, nao wakapiga hema katika Gilboa. Basi alipowaona hao majeshi ya Wafilisti, huyo Sauli akaogopa, na moyo wake ukatetemeka sana. Lakini Sauli alipouliza kwa Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Ndipo Sauli akawaambia watumishi wake, Nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake. Watumishi wake wakamwambia, Tazama, yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Basi Sauli akajigeuza, na kuvaa mavazi mengine, kisha akaenda, yeye na watu wawili pamoja naye, wakamfikilia yule mwanamke usiku; akasema, Tafadhali unibashirie kwa utambuzi, ukanipandishie yeye nitakayemtaja kwako. Yule mwanamke akamwambia, Angalia, unajua alivyofanya Sauli, jinsi alivyowakatilia mbali hao wenye pepo wa utambuzi na wachawi katika nchi; mbona basi wanitegea tanzi uhai wangu, ili kuniua? Naye Sauli akamwapia kwa Bwana, akasema, Aishivyo Bwana, haitakupata adhabu yo yote kwa jambo hili. Ndipo yule mwanamke aliposema, Je! Ni nani nitakayekupandishia? Naye akasema, Nipandishie Samweli. Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli. Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi. Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia. Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje. Samweli akasema, Kwa nini kuniuliza mimi, akiwa Bwana amekuacha, naye amekuwa adui yako? Yeye Bwana amekutendea kama alivyosema kwa kinywa changu; Bwana amekurarulia ufalme mkononi mwako, na kumpa jirani yako, yaani, Daudi. Kwa sababu wewe hukuitii sauti ya Bwana, wala hukumtimilizia hasira yake kali juu ya Amaleki; kwa sababu hii Bwana amekutendea hili leo. Tena pamoja na wewe Bwana atawatia Israeli mikononi mwa Wafilisti; hata na kesho wewe na wanao mtakuwapo pamoja nami; tena Bwana atawatia jeshi la Israeli pia mikononi mwa Wafilisti. Mara Sauli akaanguka chini kifulifuli, akaingiwa na hofu kuu kwa sababu ya maneno hayo ya Samweli, wala hakuwa na nguvu yo yote; kwa maana hakula chakula mchana kutwa, wala usiku kucha.”

Sauli alikufa wakati ule na wanawe wote walipokwenda kwenye vita. Tumeona maneno ya mtu aliyeoka kuzimu yametimia kama alivyosema kwa mtu aliyeko duniani.

(Zamani kabla Yesu hajaja wanadamu wote ambao walikuwa wanaishi maisha matakatifu walikua wakifa wanakwenda kuzimu ambapo kulikuwa na shimo kubwa lenye moto ambalo lilikuwa linawatendanisha na watu waliokufa dhambini, Baadaye Yesu alipokuja akafa msalabani alikwenda kuwahubiria wale waliokufa wangali watakatifu na kuwaeleza yye ndiye waliyekuwa wanamsubiria na kusikia habari zake, Yesu aliwatoa kule na kuwabadilishia makao yao hivyo ikawa hadi leo watu wanaokufa wakiwa wameishi maisha matakatifu wanakwenda paradiso sio kuzimu tena)

Inawezekana unashambuliwa na mtu ambaye ni askari wa kuzimu aliye ndani ya mtu, ambaye ameamriwa na shetani aje kukushambulia, wewe unakuwa unakemea mapepo na mashetani lakini bado vita inazidi kupamba moto, kinachofanyika ni kwamba shetani anakuwa anawabana kule kuzimu kama wafungwa waje kukutesa huku duniani, wanakuwa wameshageuzwa akili zao zimeharibiwa wamekuwa kama mashetani wa kuzimu. 

Siku moja Yesu alijaribiwa na masadukayo(hawaamini kiama) ambao walimuuliza kwamba 'mwalimu akioa na kama hajazaa torati inasema mwanamke huyu aolewe na ndugu yake' yesu akasema sawa kabisa na wale masadukayo wamamwambia kua mwanamke ambaye ameolewa na mtu na ndugu zake saba na wote hawa hakuna aliyezaa naye sasa akienda mbinguni atakua mke wa nani ndipo Yesu akawaambia mbinguni tunaishi kama malaika hakuna kuoa wala kuolewa.

Vivyohivyo na wale watu waliorudishwa msukule wanasema walikuwa wanafanya kazi ya kuua watoto wachanga, kusababisha ajali, kuharibu ndoa za watu, kunyonya damu n.k… hivyo na watu walikufa kwenye dhambi huja kukufuata kwa jinsi unavyo jiungamanisha nao kwenye kuwaomba au kuwaombea, kufanya matambiko nk unakuwa unajiunganisha nao na wewe unakuwa mmoja wa wafungwa wa kuzimu unayengojea sikumoja ukaungane nao.

Ukiri:-
“Kwajina la Yesu kuanzia leo watu wote waliokufa kaatika dhambi ambao wanatumwa na shetani kuja kuniletea balaa, laana, magonjwa, mikosi, umasikini najitenga nao kwa jina la Yesu kama ni ajali baki hukohuko, kama ni magonjwa najitenga nayo, ninajitenga nayo kwa jina la Yesu. Watu wa aina yeyote walio kuzimu ambao wanatumwa na lusifa ninawakana kwa jina la Yesu, ninajitenga nao kwa jina la Yesu kristo”

Kuwashinda mapepo na majini ni kazi ndogo sana kwasababu unawashinda kwa damu ya Yesu na jina la Yesu lakini majesh ya wafu kufanya vita nao ni kazi kwasababu ukiwauwa kwa jina la Yesu hawafi kwasababu Mungu anawapenda hivyo wanasubiria kukombolewa.

Duniani kuna mashetani wengi kuliko wanadamu, wanaweza kuwatosha watu wote bilioni saba na yakabaki sababu ya watu walikufa katika dhambi wanageuzwa na kuwa mashetani na roho zao zina nguvu sana kuliko mapepo.

Sababu inayosababisha majeshi ya wafu yapate nguvu ni Ibada za wafu, kuwaombea wafu waliokufa katika dhambi ni kuiamsha ghadhabu ya Mungu. “MUNGU HAPENDI UWAOMBE WAFU WALIKUFA”

Kumb18:10 “Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.”

Ukiri
“ikiwa niliwahi kushiriki ibada ya kuwaomba wafu naifuta kwa damu ya Yesu.”

Mathayo 8:22 “Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.”

Sababu nyingine ni kuomba makaburini, pia sababu nyingine ambayo inawaimarisha wafu ni kunyoa nywele kwaajili ya mtu aliyekufa akiwa dhambini. Utaratibu huu ulianzia kwenye Biblia hutakiwi kunyoa ina maanisha unaponyoa nywele zako na wewe utamfuata kule aendako.

Sababu nyingine ni maneno ya mwisho kabla hajafariki. Sababu nyingine ni zile salamu zinazounganisha watu waliokufa (kule kusalimiana kwa kutaja jina la Babu wa ukoo.

Inawezekana shida uliyonayo imeletwa na yule mtu aliyekufa katika dhambi ambao wanaona ni halali wewe kutokuzaa, kutokufaniniwa, kutokufanikiwa unatakiwa useme mwenyewe unahama kwa jina la Yesu na kuingia katika ukoo wa Ibrahimu Isaka na Yakobo ukoo wa Yesu kristo. Najitenga nao kwa jina la Yesu, najitenga na wivu wenu, najitenga na umaskini wenu, najitenga na mipango yao kwa damu ya Yesu.

Usimpeleke mtoto kwenye kuingizwa kwenye ukoo wala usihudhurie arobaini kwa sababu sisi tuliokolewa hatuna kitu kinachoitwa arobaini kwenye Ufalme wetu.

Omba maombi ya kujitenganisha na wafu waliokufa dhambini sababu wao ni silaha kubwa na pekee ya shetani kuharibu maisha yako.

Mafundisho haya yanapatikana kwenye kitabu cha Majeshi ya wafu ambapo sehemu ya pili na kuendelea yameelezewa kiundani na kila sehemu kuna mwongozo wa maombi. Unaweza kujipatia nakala yako.

SOURCE: GOSPEL KITAA

Comments