RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

VIGEZO VYA KUZINGATIA KUJIAMINI


By Geofrey Mwakatika
Ni vigumu kuelezea moja kwa moja kujiamini maana yake nini? Lakini mtazamo wa mwanadamu juu ya namna wenzake wanavyomchukulia inaweza kuwa kutafsiri ya neno kujiamini. Ikiwa utajilinganisha na wengine na hatimaye kuhisi aibu, ujue unakabiliwa na tatizo la kujiamini.
 Mwimbaji wa Gospel Tanzania, Mess Chengula-mfanyabiashara Kariakoo na mfanyabiashara wa vifaa vya pikipiki 

kuna mambo mengi yanayoweza kumfanya mtu asijiamini mbele ya wenzake, kiasi cha kujiona duni kwa hili na lile na wakati mwingine hali hiyo humfanya ashindwe kufanya hata mambo ambayo anayajua na kwamba amekuwa akiyafanya kila siku, Kisaikolojia huu ni ugonjwa ambao unaweza kuathiri uwezo wa mtu , namaanisha kwamba mtu anaweza kuwa si mlemavu wa miguu, lakini akatembea mbele za watu upande upande, anaweza kuwa na akili lakini akajikuta hawezi kuzitumia kwa sababu si mwenye kujiamini.
Kama ilivyo kwa magonjwa mengine, kuponywa kwa tiba, tatizo hili la kutokujiamini nalo linatakiwa litibiwe. Zipo njia nyingi ambazo mtu anaweza kuzitumia kujenga hali ya kujiamini, yako mambo muhimu ya msingi ambayo mtu akiyazingatia na kuyafanyia kazi anaweza kuondokana na hali ya kutokujiamini.

Kujizoeza kujiamini
Njia moja muhimu sana kisaikolojia ya kujenga hali ya kujiamini ni kupenda kusikiliza maneno ya kutia moyo na yenye ujasiri kutoka kwa watu maarufu. Kwa mfano, viongozi wenye msimamo, watetezi wa haki za binadamu, wanasiasa wanaotetea maslahi ya nchi bila hofu na kadhalika. Hotuba na maneno yao yakipata sehemu kubwa katika akili ya mtu, lazima yatajenga hali ya kujiamini kama wale anaowasikiliza.

Mwimbaji wa Gospel Christina Shusho aliyefanikiwa katika ulimwengu wa Gospel Tanzania

Kubali matokeo
Ifahamike kuwa ukiwaza kwa kina sana juu ya mahitaji yako, zao litakalofuata hapo ni akili kukuletea sababu za kushindwa kufanikisha mambo unayoyataka. Sababu hizo ukizipa nguvu sana ya kuziwaza zitakupa jibu la haiwezekani. Unapokuwa na mawazo yenye mlango huo wa kutokufanikiwa, uwezo wako wa kujiamini hushuka na kujikuta unashindwa katika mambo uyafanyayo. Katika maisha lazima mtu akawa na wakati wa kuachia mawazo yake na kukubaliana na matokeo yaliyopo hasa pale hali ya kushindwa inapokuwa kubwa.


Pata Msaada toka kwa watu wengine

jambo jingine la muhimu katika kuhitimisha uwezo wa mtu kujiamini ni kupata msaada wa mawazo kutoka wa watu wengine ambao ni makini katika maisha yao. Kama kuna jambo ambalo linakuwa gumu katika mawazo yako na limekosa ufumbuzi kiasi cha kukufanya usijiamini, washirikishe wengine wakusaidie na kukutia moyo wa kuendelea kukabiliana na hali yako ya kutojiamini.


Pendelea kukaa mbele
Katika kujenga hali ya kujiamini ni vizuri zaidi unapokuwa shule, ofisini, kwenye mikutano, semina ukawa na tabia ya kuketi nafasi za mbele. Ni ukweli kuwa, watu wengi hawapendi kukaa sehemu za mbele kwa sababu ya hofu ya kuonekana kwa urahisi na pengine kuwa wa kwanza kuulizwa au kuchangia hoja, tabia hiyo huondoa hali ya mtu kujiamini. Ili kujenga ujasiri ni vema mtu akapendelea kuketi vitu vya mbele na mara nyingi kuwa wa kwanza katika kufanya mambo.

Mwonekano sahihi
Namna mtu mwenyewe anavyouweka mwili wake linaweza kuwa ni tatizo la kumfanya ashindwe kujiamini. Kwa mfano,mtu kama si mlemavu lakini akajikuta anatembea miguu upande, mabega juu, kichwa chini au juu sana au kutembea akiwa anadundika kama mpira, ni vibaya kwa vile kitaalamu huchangia kumuondolea mtu ujasiri mbele za watu.
Ushauri wangu ni kwamba mtu anatakiwa kuupa mwili wake umuhimu na kuuweka kama alivyoumbwa, haifai kuwa mtu wa kuinama na kuficha uso, kusimama tenga pale unapoitwa au kuwa mbele za watu. Si vema pia kujipapasa mwilini au kutazama pembeni. Ni vizuri kila mtu kulinda mwonekano wake wa asili mbele za wenzake.


Kutembea haraka
Njia rahisi ambayo imethibitika kuweza kumuondolea mtu hali ya kutokujiamini ni kutembea kwa mwendo wa haraka. Haipendezi unapokuwa njiani kutembea kama mgonjwa, uliyechoka. Ukiwa hivyo ni rahisi sana kuwafanya watu wakukodolee macho ambayo yatakufanya wewe uhisi tofauti. Utembeaji wa haraka una faida nyingi, lakini kubwa kabisa ni kuwafanya watu wengine wakuone wewe ni mtu wa kazi usiyetaka kupoteza muda wako, mtu makini na mwenye mipango. Kitaalamu mwendo unaoruhusiwa ni wa asilimia 25, usizidi sana kiasi cha kuonekana kama unakimbia.

Pingana na wengine
Mtu akijiona duni mwenyewe ni rahisi kwake kudhani kuwa watu wengine ndiyo wenye mambo ya kweli na hivyo kujikuta akifuata mkumbo na kupotoshwa katika ukweli. Ili mtu aweze kuwa sahihi katika mawazo ya vile anavyoamini ni lazima awe na tabia ya kupingana na wenzake. Ni jambo baya kukubaliana na watu katika mawazo yao bila kupinga katika kile unachoamini, kufanya hivyo kunaweza kuyafanya maneno ya uongo ya wengine yakaaminika na kuuacha ukweli wa mtu asiyejiamini ukipuuzwa kwa sababu tu hakuwa na ujasiri wa kukabiliana na hoja za wenzake.

Comments