RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MWALIMU JOHN MTANGOO: KWA NINI WANAKWAYA WENGI NI MASKINI?


KWA NINI WANAKWAYA WENGI NI MASKINI?
Kwa kiwango cha kidunia kuwa maskini ni kuishi kwa kutegemea kipato cha chini ya dola moja kwa siku. Japokuwa haya ni maisha ya watanzania walio wengi, ili kuongeza mvuto kwa vikundi vya uimbaji ilipaswa kuwa tofauti.

1. Imeonekana ama kufikirika kwamba kwaya ni kwa watu wasio na kazi ama wasio busy. Watu wengi walioanza kuimba kwaya Mungu akionesha dalili za kuwabariki wanaacha kuimba. Ni kawaida kwaya kuchagua mfadhili ambaye alikuwa ni muimbaji wao zamani. HIVI HUONI KWAMBA UKIFANIKIWA NDANI YA KWAYA UKAENDELEA KUIMBA UTAWAAMBUKIZA WENGINE NJIA ULIZOPITIA WEWE KUFANIKIWA?

2. Waimbaji wengi wanapoteza muda kwa kitu wasichokipenda hivyo kujifungia milango ya mafanikio. MUNGU ANASEMA MTU AKINIPENDA ATAZISHIKA AMRI ZANGU. Kama huishi katika utii wa Mungu utategemea nini? MAANDIKO YANASEMA MTU AKINITUMIKIA BABA YANGU ATAMUHESHIMU. Unataka heshima gani ukiwa mlevi, mzinzi, muongo, mchonganishi, mfitini n.k Milango ya kiuchumi lazima itajifunga tu! Kumbuka heshima ya Mungu kwako ina furaha na amani. Kama humpendi Mungu usipoteze muda wako kuja kuimba.

3. HUDUMA NI VITA!
Unadhani kuimba ni kujifurahisha tu? Kuimba ni kutangaza sifa za ukuu wa Mungu. Unadhani kuzimu inashangilia? Amin Amin nakuambia kujiingiza kwa kundi la kumsifu Mungu ni kutangaza vita na Ibilisi na jeshi lake. Sasa wewe silaha za Mungu huna, unaingiaje kwenye vita usiyoijua? 

4. WAIMBAJI WABINAFSI
kwanini nafasi nyingi za kazi haziletwi kwenye kwaya? Utaambiwa hawakidhi vigezo. Swali ni wenye vigezo wanapatikana wapi? Jibu ni wamejiendeleza kielimu. Sasa kama tunachangishana kununua vyombo, harusi na ubarikio kwa nini tusichangishane kusoma? 

Elimu inafungua maono. Waimbaji wengi wanaishia kuwa na maisha duni kwa sababu WATU WANGU WANAANGAMIZWA KWA KUKOSA MAARIFA. Wewe muimbaji ambaye Mungu amekufungulia milango usione raha kuwa mwenyewe, usione raha kutetemekewa mwenyewe kwa kuwa ndiye unatoa mchango mkubwa kwa kundi bali ibua mawazo na maono makuu yatakayo ibua uchumi wa muimbaji mwenzio. Wafadhili na walezi wekeni nguvu kwenye kuimarisha uchumi wa waimbaji kielimu na kibiashara. Msipende kuwapa kwaya samaki wafundisheni namna ya kuvua.
Mungu akubariki na kukufungulia baraka za kiuchumi unapomtumikia kwa njia ya uimbaji kwa uaminifu.


Mwalimu na mtayarishaji wa muziki wa injili Tanzania
John Mtangoo 2016


Comments