RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SOMO LA UKRISTO LAKACHWA CHUO KIKUU CHA OXFORD


Taswira ya juu majengo ya Chuo Kikuu cha Oxford

Wanachuo wa mwaka wa pili na tatu katika Chuo Kikuu cha Oxford kilichopo Uingereza wanalazimika kuchagua masomo mengine tofauti na somo la Ukristo, kutokana na kubadilika kwa mfumo wa masomo.

Katika kile kinachoelezwa kama mabadiliko ya mfumo huo, wanachuo watalazimika kuchagua aidha kati ya kusoma somo la Ubudha, ama Mtazamo wa Wanawake na Kanisa, huku wale wa mwaka wa kwanza pekee wakitakiwa kusoma kuhusiana na Ukristo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa bodi ya Kitivo cha Thiolojia Profesa Johannes Zachhuber ambaye amenukuliwa na Christian Today, ameeleza kuwa chanzo cha kubadilika kwa mfumo wa masomo hayo ni kutokana na namna dini inavyochukuliwa na kuendeshwa nchini Uingereza.

Aidha baadhi ya watu wametoa maoni yao; wengine wakieleza kufurahia jambo hilo kutokana na maana hasa ya neno thiolojia, ambayo humaanisha masomo ya Mungu/miungu, na kwamba kunyambua maeneo mengine tofauti na Ukristo pekee itafaa; Napo wengine wakitiririsha vifungu vya Biblia kutoka Kitabu cha 2 Timotheo 4:1-4 yenye kuzungumzia zama ambazo watu watakataa ukweli na kutaka kusikia hadithi za uongo.


Kufahamu kwa undani zaidi, GK imemtafuta Mwalimu wa Neno la Mungu, Mchungaji Benjamin Israel wa Jijini Arusha, ambaye anaeleza kwamba kujifunza dini nyingine tofauti na ukristo halisi kuna faida na hasara zake. Kwani mtu anaweza kujifunza akatekwa, ama ukasaidika kujua jinsi maandiko yanavyotimia kwa nyakati za leo.

"Kwenye vyuo vya Biblia kuwepo masomo ya dini mbalimbali ni sahihi. Kwani tunaamini wale wote waliokwenda vyuo hivyo wamekomaa kiroho na wanao Uwezo wa kula vyakula vigumu na si maziwa." Anaeleza Mchungaji Benjamin na kuongezaw kwamba alipofika mwaka wa pili chuo cha Biblia alikutana na somo linaitwa "World Religions".

"Tulijifunza habari ya dini nyingi sana ikiwemo, Budhism (Ubudha), Hinduism (Uhindu), Islamic (Uislamu) n.k. ambapo niligundua kuna dini zaidi ya mia tatu, zote zikiwa na lengo la kumtafuta Mungu lakini kila mmoja na mtazamo wake, njia yake na Imani yake. Hii inawasaidia watumishi wahubirio injili kujua namna ya kuhubiri pindi atakapokutana na mtu wa dini Fulani, japo wachache huvutiwa na baadhi ya dini na kujikuta kuukana ukristo." Anamaliza kueleza Mchungaji Benjamin.

Comments