RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

UNAMTUMIKIAJE MUNGU KWA VIUNGO ALIVYOKUPA?



Musa akamwambia Bwana Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako; maana mimi si mwepesi wa kusema, na ulimi wangu ni mzito. Bwana akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, Bwana?#Kutoka 4:10-11

Waweza kuona kama ni jambo la kawaida kwa sababu Mungu amekujalia viungo vyote katika mwili wako. Lakini huwa nikipita mitaani na kuona walemavu huwa ninajitafakari mara mbili mbili. Kanisani kwetu tuna walemavu wawili ambao kila jumapili huwa sio rahisi kuwakosa ibadani. Na ikitokea kazi yoyote ya kanisa pasipo kujali ugumu wake watu hawa huwa hawakosi. Wakati ambao unaweza kuwakosa watu waliojaliwa viungo vyote vya mwili hawa ndugu wawili huwa hawakosi. Nikiwaona huwa natiwa moyo na kusema nitatumia kwa nguvu zangu zote maishani mwangu pasipo kujali maisha gani ninaishi kumtumikia Mungu aliye hai. Ikiwa mlemavu aweza kutumika kwa nguvu hivi je mimi niliyejaliwa kuwa na viungo vyote nina sababu gani ya kukwepa kumtumikia Mungu. Ole wangu mwanadamu mimi nisipomtumikia Mungu!

Wapendwa wangu sijui kama wewe huwa unalitafakari hili. Mungu anatufunulia kupitia mtumishi wake Musa kwamba kuwa Bubu, Albino, Kilema, Kipofu ni Mungu ndiye aliyeruhusu kuwa hivyo. Ndugu yangu wewe ambaye umejaliwa viungo vyote unajitoaje kwa kutumia viungo vyako kumtumikia Mungu?

Kwa mfano, Namna gani unajitoa kuwaonyesha upendo wa Kristo walemavu mbali mbali. Au ndo ukikutana na mlemavu unatafuta shilingi 100 au 200 ndo unampa? Upendo wako kwake thamani yake ni shilingi 100? Au serious mwana wa Mungu? Kweli toka ndani ya moyo wako thamani ya upendo wako kwa mlemavu ni shilingi 100? Huwezi ukajitoa mara moja kuchukua kilo ya sukari ukampelekea mlemavu yule jirani yako? Huwezi ukanunua kilo ya nyama ukampelekea yule mlemavu mtaani kwenu? Au huwezi kuchukua kilo ya unga ukampitishia yule mlemavu huwa unampita na gari yako pale mtaa Fulani kila siku urudipo au uendapo kazini? Au kaupendo kako kamekuwa kadogo hivyo kwao kwa kuwapa shilingi 100? Shilingi 100 anunue nini? Yesu tusaidie!
Nilifuatilia maisha ya Mwinjilisti mmoja wa Injili wa Vietnamu Nick Vujicic (aliyeko pichani). Mtumishi huyu hana mikono na Miguu yake ni mifupi ina ulemavu. Mtumishi huyu alikutana na Yesu na sasa anaihubiri Injili kwa kiwango kisicho cha kawaida. Ameweza kutengeneza makundi ya maombi na watu wamekuwa wakiifanya kazi ya Mungu pamoja naye. Nikatafakari sana sisi tuliowazima tunatumiaje viungo vyetu kuieneza Injili! Ikiwa walemavu wanaweza kumtumikia Mungu kwa jinsi walivyo, mimi na wewe tuliojaliwa viungo vyote kwanini tusitumike kwa namna iwayo yote kuieneza injili? Kwa nini?

Mungu ametujalia wanadamu vitu vingi maishani mwetu ambavyo tukivitakari tunaweza kumtumikia Mungu vizuri. Wakati nilivyomaliza chuo maana nilisomea mambo ya Information Technology nikaaanza kujitafakari namna gani naweza kumtumikia Mungu kupitia maarifa haya aliyonipa kuyasomea. Moja ya vitu ambavyo vilinipa deni ni namna ambavyo watu tulikuwa tukiutumia muda wetu kwenye mitandao ya kijamii. Nikajikuta nimekuwa na deni kubwa sana kwanini mitandao ya kijamii itawaliwe na mambo mabaya mabaya tu. Kwa nini injili isitawale mitandaoni? Kwanini nisitumie Injili kuwafikishia watu habari njema za wokovu wa Bwana wangu Yesu Kristo. Kwanini nisitumie Internet kuomba pamoja na mtu yeyote duniani? Nikaanza kujenga hamu ya kumtumikia Mungu kwa kuisambaza injili kwa njia ya mtandao. Jambo hili likaumbika kipekee na Mungu kwa kuwa ni mwaminifu alianza kugusa maisha ya watu. Watu wakaguswa na injili. Na kwa kuwa maombi hayana mipaka kama ambavyo Internet haina mipaka Mungu ameendelea kuponya na kuokoa watu kwa njia ya Injili hii hii ambayo tumeihubiri kwa njia ya mtandao. Unatumiaje viungo vyako kwa ajili ya kumtumikia Mungu mpendwa wangu?

Na sijui hata kama huwa unafikiria kwamba hata walemavu hao pia wanahitaji Injili. Mara ngapi unawapa Injili watu hawa? Mara ngapi umejaribu kuwafikishia habari njema za Yesu Kristo?
Mungu atusaidie sana kuyatumia maarifa haya kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Maandiko yanasema ‘ siku za mwisho maarifa yataongezeka’ #Daniel 12:4
Yatafakari hayo na Mungu akusaidie.

Mungu akubariki sana. Ukiwa una jambo lolote unataka tuombe pamoja nawe mkono wa Mungu uingilie kati katika tatizo lako basi wasiliana nasi: Whatsapp prayerline 0758 443 873, au tutumie SMS au kutupigia kupitia 0712 204 937 . Waweza pia kutuandikiainfo@nenolauzima.org
JE UNATAKA KUMWAMINI YESU?

Ikiwa unataka kumwamini Yesu awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako akupe nguvu ya ushindi muda uliokubalika ni sasa hivi. Usichelewe chukua maamuzi. Omba maombi haya kwa Imani:
‘Sema Bwana Yesu ninakuja kwako kama nilivyo. Asante kwa sababu umeniokoa pale msalabani. Ninaamini kwamba ulikufa na kufufuka. Ninaomba unisamehe dhambi zangu zote. Nioshe kwa damu yako Kristo. Niandike jina langu katika kitabu chako cha uzima. Karibu Roho Mtakatifu ndani yangu. Niongoze katika kutembea katika nguvu ya ufufuo wa Kristo nikutumikie daima. Katika jina la Yesu ninaomba. Amina’.

Ndugu ikiwa umeomba sala hii kwanza tujulishe tuendelee kukuombea ukue katika Imani na katika kumtafuta Mungu. Jifunze kuwa na Ushirika na Roho Mtakatifu kila siku. Jifunze neno lake na omba kila siku. Omba kujazwa Roho Mtakatifu kila siku. Nawe utatembea katika nguvu za Mungu. Jifunze kukutanika na wakristo wengine mahala popote katika dhehebu lililo karibu nawe wanaojifunza neno la Mungu na kuomba pamoja. Roho Mtakatifu anakupenda sana. Na Mungu akubariki sana.
Share ujumbe huu ikiwa umependezwa nao ili na wengine wabarikiwe na pia elekeza watu waweze ku-like ukurasa wetu wa facebook www.facebook.com/UshuhudawaInjilitujifunze pamoja nao neno la Mungu.

Comments