RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MKUU CHUO CHA UHASIBU ARUSHA (IAA) AFUNGWA MWAKA MMOJA KWA KUAJIRI WATUMISHI DARASA LA 7


Mkuu wa Chuo cha Uhasibu (IAA) mkoani Arusha, Profesa Johannes Monyo amehukumiwa kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja baada ya mahakama kujiridhisha kuwa mkuu huyo aliajiri watumishi wanane wenye elimu ya darasa la saba bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma.

Akitoa hukumu katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Hakimu Devotha Msofe alisema Profesa Monyo akiwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Njiro, aliwaingiza watumishi wanane kwenye ajira ya kudumu bila ya kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Mkuu Utumishi.

“Mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa ulifanya kosa hili la kuajiri wafanyakazi wanane bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma hivyo mahakama hii inakutia hatiani kwa kukupa kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja,”alisema Hakimu Msofe.

Awali, Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Adam Kilongozi alidai kuwa Juni, 2010 Profesa Monyo anatuhumiwa kuwapa ajira watumishi wanane ambao ni Pamela Maboko, Samson Mbarya, Mawazo Ndaro, Juma Nyarutu, Lilian Ngowi, Godfrey Mollel, Musa Maiki na Salim Shabani.