RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SERIKALI IMETANGAZA KUANZA KUTUMIKA RASMI KWA ALAMA HIZI ZA AFRIKA MASHARIKI

May 19 2016 Serikali imetangaza rasmi alama za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitakazotumika kwenye Ofisi za Serikali na katika shughuli zote rasmi za kiserikali.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mindi Kasiga amezitaja alama hizo kuwa ni bendera ya Taifa, bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wimbo wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na wimbo wa Taifa.

Kasiga amesema kuanzia sasa bendera ya Jumuiya hiyo itapepea sambamba na Bendera ya Taifa kwenye Ofisi zote za Serikali huku wimbo wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki ukiimbwa sambamba na wimbo wa Taifa katika shughuli rasmi za serikali kuanzia ngazi za Halmashauri hadi Taifa, ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo kifungu cha 7(a).

“Mkataba huu unasisitiza jumuiya hii kuwa jumuiya ya watu, hivyo watanzania watahusishwa katika hatua zote za mtangamano huo, pamoja na kushirikishwa kikamilifu katika hatua mbalimbali za jumuiya ili kujua madhumuni ya kunufaika na fursa mbalimbali zitakazaopatikana ndani ya Jumuiya hiyo”,

Aidha, Kasiga ameongeza kuwa matumizi ya alama hizi ni njia mojawapop ya kujenga uzalendo na kumfanya Mwananchi ajisikie kuwa sehemu ya ushirikiano huu.

Vilevile, taasisi binafsi zinaweza kutumia alama hizi, huku shule na vyuo vikisisitizwa kutumia alama hzi kama sehemu ya kuelimisha na kuhamasisha vijana kuhusu Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaratibu upatikanaji wa sampuli ya alama hizo kwa gharama za taasisi, wizara au Ofisi husika.