RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SOMO: UFALME WA MBINGUNI - DUNIANI - ASKOFU GWAJIMA




SOMO: UFALME WA MBINGUNI - DUNIANI

Biblia sio kitabu cha kidini kwasababu kinaitwa kilichobeba Agano. Agano maana yake ni (mkataba). Biblia ina Agano la Kale na Agano Jipya, kwenye vitabu vya kidini Biblia haimo miongoni mwavyo. Unapokuwa unafungua Biblia utakutana na Agano la kale na Agano la Jipya. Biblia ni kitabu cha kisheria. Ni hati ya kisheria, ni mkataba wa kisheria hivyo sio kitabu cha dini. Biblia ni sheria.

BIBLIA INAHUSU NINI?
1. Biblia inahusu Mfalme.
2. Biblia inahusu familia ya kifalme.
Ni hati ya kisheria ambayo inahusu Mfalme na familia ya kifalme.
3. Biblia inahusu Serikali ya Ufalme.
4. Biblia inahusu katiba ya Ufalme/ni katiba ya Ufalme.

“Serikali hii ya kifalme imetoa ahadi zake kwenye katiba kwa wana wa Ufalme ambao ni sisi tuliomkiri Mfalme Yesu kuwa mmiliki wetu ndani ya ufalme wa mbinguni hapa Duniani”

5. Biblia inahusu nchi inayoitwa Mbinguni.
Sisi ni koloni la nchi hiyo hapa duniani.

Baadhi ya makanisa ya kidini hutumia Biblia kudonoa mistari tofauti na kutengeneza mila yao kitu ambacho sio lengo la Ufalme wa Mbinguni kwasababu Biblia ni hati ya kisheria ambayo inahusu Mfalme na Ufalme wake.

Ukielewa maaana ya Biblia na kama mtu amekufa au ana kansa au ana UKIMWI basi hilo sio tatizo kwasababu tunayo katiba yenye Mfalme ambaye ametupa ili tuifuate. Mungu ameanzisha koloni lake hapa Duniani kueneza Ufalme wa Mbinguni. Ndio maana Yesu alikuwa akitoa mifano mingi kuifananisha na Ufalme wa Mungu. Yesu aliwafundisha wanafunzi kuomba kwamba waombe Baba Yetu uliye mbinguni(maana yake watambue Baba yao yupo mbinguni si mahali pengine), Jina lako litukuzwe Ufalme wako uje mapenzi yako yatimizwe utakalo lifanyke duniani kama mbinguni (Ufalme wa mbinguni uje duniani na lolote linalotendeka mbinguni litendeke hapa duniani).

Ndiyo maana Mungu alimfanya Adamu kuwa koloni la Mbinguni hapa duniani lakini Adamu alijitangazia uhuru na kujitoa kwenye koloni la Mbinguni hivyo Mungu akaamua aje atupe koloni lake tena kupitia kwa Bwana Yesu. Mungu alitengeneza katiba ya koloni hilo ambayo ni Biblia.

“Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;” Wakolosai 1:13-14

“Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.” Mathayo 4:17-8

“Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia. Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu.”Mathayo 10:7

“Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu),” Mathayo 24:14-15

“Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake.” Mathayo 6:33

Cha kutafuta kwanza ni Ufalme na haki yake na mengine yote yatakuja, mtazidishiwa.

Kwanini mtu unapookoka unaitwa umezaliwa mara ya pili?

Unaposema kwamba Bwana Yesu nakupokea kama Bwana na mwokozi wa ……………
Unaposema hivyo wewe unaitwa raia wa Mbinguni unayeishi duniani (mfano: Mzungu anapokuja Tanzania kutokea Uingereza anaitwa raia wa Uingereza anayeishi Tanzania) lakini wewe unakuwa raia wa Mbinguni kwa kuzaliwa mara ya pili unayeishi duniani.

“Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;” Wafilipi 3:20

URAIA WA MBINGUNI UNAPATIKANAJE?

Kuna uraia wa kununua hapa duniani lakini kuna uraia wa kuzaliwa mara ya pili(rohoni) umekuwa raia wa mbinguni wa kuzaliwa. Kwahiyo kuokoka kimsingi ni kuwa raia wa mbinguni wa kuzaliwa lakini unafanya shughuli zako duniani ukiwa ndani la Ufalme wa Mungu hapa Duniani. Ukielewa maana hii huwezi kuguswa na mtu yeyote sababu wewe ni raia wa Mbinguni na ukiguswa tu mbinguni wanasimama kukutetea. (Raia wa Marekani akuwa Tanzania na akitenda kosa hawezi kukamatwa kama raia wa Tanzania lazima taratibu zifuatwe)

Ukiwa ndani ya Ufalme huu wa Mbinguni na kujitambua wewe kama raia wa kuzaliwa na ukaifahamu sheria ndipo sasa unaweza kufanya kazi zako za biashara, uongozi, safari ukiwa ndani ya Ufalme.

Lile neno ulilolitamka ulipozaliwa mara ya pili kwa njia ya imani kwenye koloni la mbinguni ukasema “Bwana Yesu karibu ndani ya moyo wangu” lile neno Bwana Yesu kwa kiyahudi maana yake ni mmiliki yaani unakiri Bwana Yesu ndiye mmiliki wako ambaye anakumiliki ndani ya Ufalme huu.

Ukiri:
“Kwa jina la Yesu, Baba Mungu naomba fungua moyo wangu nifahamu sheria yako”

Ndani ya Ufalme huu kuna sheria za kufuata ambazo mfano wake ni usizini, usiibe n.k ambapo ukivunja sheria hizo unaadhibiwa. Ukiwa ndani ya Ufalme huu na kuzifuata sheria zake basi wewe unaitwa Mtakatifu. Ukiwa huzifuati sheria za ufalme unakuwa si raia kamili wa ufalme,kwa lugha nyingine unakuwa kama “mbabaishaji”.

“Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano? Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.” Mathayo 13:10-11

Kumbe ukiwa ndani ya Ufalme huu kuna watu waliojaliwa kuzijua siri za Ufalme huu na wengine hawakujaliwa kuzijua.

“Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.”Mathayo 13:44-46

Yesu anajaribu kusema kwamba ukitaka kuingia ndani ya Ufalme huu ni afadhali upoteze vitu vyote lakini uingie kwenye Ufalme huu.

Maana yake tangu wakati wa Yohana mbatizaji mpaka sasa Ufalme huu wa mbinguni hupatikana kwa wenye Nguvu nao wenye nguvu wauteka.

“Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” Mwanzo 1:26

Mungu amesema tumfanye mtu kwa mfano wetu na sura yetu (neno ‘Sura’ kwa kiyahudi limeandikwa kama Utukufu). Kilichomfanya Yesu aje duniani ilikuwa ni kurudisha kile ambacho Adam alikipoteza ili tutawale tukiwa ndani ya Ufalme wa Mbinguni kama raia wa Ufalme na Biblia yetu kama sheria ya Ufalme na lugha yetu ya Ufalme (Kunena kwa lugha) na Mmiliki wetu akiwa ni Bwana Yesu.

Ukiri:
“Katika jina la Yesu, Baba Mungu naomba nifungue akili nijue niko ndani ya Ufalme”

Ukiwa ndani ya Ufalme hakuna anayeweza kukutoa, na ukivunja sheria ya Ufalme ulinzi wa ufalme unaondoka kwako na ndio maana unaweza ukapatwa na magonjwa, laana, matatizo.

Magonjwa, wala laana, wala Matatizo hayawezi kukupata ukiwa ndani ya Ufalme, kama unataka kufanikiwa unasema “Bwana Yesu nakuja kwako nakupokea uwe Bwana na Mwokozi wa Maisha yangu leo” unaposema maneno hayo shetani na wakala wake; waganga wa kienyeji, wachawi na wasoma nyota wakikuangalia wanaona uko ndani ya Ufalme wa Mbinguni.

Ukiwa kwenye hiyo nchi kuna namna ya kusoma, kuolewa/oa, kufanya biashara, uongozi, kuna namna ya kusafiri. Ukiwa ndani ya Ufalme huu kuna haki zake ambazo ni:- hulogwi, huugui, huibiwi, hutaabishwi, hufi kabla ya wakati, wala mabaya hayakupati. Hizo ni haki sio za kuomba bali ni haki zako kama raia wa Ufalme wa mbinguni.

“Kuokoka ni kuhama nchi”
Watu wanalogwa kwasababu wamesema wameokoka ili wapigane na shetani kitu ambacho si kweli maana ukiwa uko ndani ya Ufalme una haki zao na huwezi kutaabishwa. Umekuja duniani kufanya kazi iliyokuleta na hivyo mpaka uimalize ndipo urudi mbinguni.

Kwenda mbinguni sio jambo la ajabu sababu tumetumwa kuja kufanya kazi ya kueneza mila ya Ufalme wa Mbinguni hapa duniani.

Hama kwenye ngazi ya kusema “Baba Mungu nakuja kwako nataka kulala naomba unilinde” sababu ni sheria ya Ufalme wewe kama raia wa Ufalme ni lazima uwe na ulinzi.

Ukiri:
“ MIMI NI RAIA WA UFALME WA MBINGUNI”

Ukifahamu hilo unatakiwa ujue kuna baadhi ya Mambo hutayaomba tena, kuna mambo hayatakusumbua tena.

Ulisulubiwa na Yesu kwa njia ya imani na ulipompokea Yesu umezaliwa upya kama raia wa Mbinguni.

“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Wagalatia 2:20

Sisi tulio ndani ya Ufalme huu tupo mbali sana na watu ambao tunaishi na wenye dhambi kimwili tunaweza tukagusana nao lakini kiroho tumeketiswa mbali sana nao.

Unapokuwa ndani ya Ufalme hauombi bali unaachia “unaachia Baraka, unaachia uponyaji, unaachia uzima, unachia afya, unaachia amani, unaachia hauombi sababu upo ndani ya Ufalme.
Maombi dhaifu ni yale ambayo unaomba bila kutambua upo ndani ya ufalme ni yale maombi ya kumwomba Baba wa Mbinguni ashuke ili aje atende.

Ukiri
“Kwa jina la Yesu Mimi ni mwana wa Ufalme usio haribika, Mimi ni mwanadamu nimeingia kwenye Ufalme wa Mbinguni, mfalme wake ni Bwana Yesu, katiba yake ni Biblia”

Ukoloni maana yake ni mfalme wa kutoka sehemu fulani kuja kuanzisha ufalme wake. Sisi tumetumwa hapa dunia kueneza Ufalme wa Mbinguni.

Hatuzini, hatuibi, hatutendi maovu sio kwasababu hatujui au hatuna mahali pa kutendea, hapana!! hatutendi maovu kwasababu sio mila yetu na katiba yetu hairuhusu, watu wenye matatizo kwenye ufalme huu ni wale ambao hawakujua sheria za Ufalme huu.

Watu wengi tumewaombea matatizo waliyonayo yawatoke lakini matatizo hayo yamewatoka na kuwarudia baada ya muda kwasababu ya kutokutambua kwamba walipoingia kwenye Ufalme wa Mungu kwa kumkiri Bwana Yesu waliukuta Ufalme ambao una Katiba yake yenye Haki zao na zipo Sheria za kuzifuata.

Tumeingia kwenye Hatua ya Kuutangaza Ufalme wa Mungu Duniani ili kuueneza Utawala wa Mbinguni Duniani kote na mila ya Ufalme pamoja na haki zake zishikwe na kufahamika kwa watu wote. Kuna vitu utavipata sio kwasababu umeomba bali kwasababu umetambua asili yako. Amen