RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

CHINI YA MIAKA 30 HELLEN DAUSEN BILIONEA MTARAJIWA BONGO



Generated by IJG JPEG Library

Boniphace Ngumije

WAZO ni hatua ya kwanza katika mafanikio, vitendo ni hatua inayofuata. Haijalishi wazo la kufanikiwa unalipata ukiwa na umri gani, ilimradi tu ukiwa ‘active’ katika kulitendea kazi.

Hivyo ndivyo ilivyotokea kwa mwanadada wa Kitanzania, Hellen Dausen ambaye ametajwa hivi karibuni na Jarida la Forbes katika orodha ya mabilionea wa miaka michache ijayo wenye umri chini ya miaka 30.

Katika mahojiano ‘Exclusive’ na Over Ze Weekend kutoka nchini Marekani ambako yuko kimasomo, Hellen amefunguka mambo mengi ikiwemo siri ya yeye kufanikiwa hata kufika mahali alipo sasa.

OVER ZE WEEKEND: Watanzania wangependa kujua elimu yako, ulikozaliwa na hata kukulia.

HELLEN: Nimezaliwa na kukulia Mitaa ya Makumbusho, Kijitonyama, Dar. Elimu ya Msingi nilipatia Shule ya Msingi Muhimbili huku sekondari nikisoma Shule za St. Mary’s kwa elimu ya awali na baadaye Shaabani Robert zote za jijini Dar. Nilipomaliza masomo ya sekondari nilijiunga na chuo cha United International University kilichopo Kenya kwa masomo ya biashara ambapo nilichukua digrii.

OVER ZE WEKEEND: Elimu yako inaonesha wazi ungeitumia kuajiriwa na kufanya mambo makubwa, nini hasa kilikuvutia kwenye ujasiriamali?

HELLEN: Ndoto yangu kubwa siku moja niwe bosi. Niwe na kampuni yangu, niweze kuajiri watu na kuishi maisha mazuri. Baada ya kumaliza tu masomo niliamua kujiingiza kwenye mitindo nikiamini siku moja nitamiliki kampuni ya masuala hayo.

Nilienda Marekani kusomea mitindo na uigizaji pia nikiwa huko nilitafuta fursa kwenye tasnia ya u-miss na mitindo lakini sehemu kubwa niliambiwa mfupi na pia walihitaji wasichana wenye umri mdogo zaidi yangu miaka 17 hadi 18 na mimi nilikuwa na miaka 25. Sababu hizo zilinikatisha tamaa ambapo baada ya kurudi nyumbani mwaka 2012 na kukosa kazi ya kufanya ndipo nilipoamua kujiingiza rasmi kwenye ujasiriamali.

OVER ZE WEEKEND: Lakini umewahi kuwa mshindi wa u-miss nchini, kwa nini hukuhamishia nguvu uliyokuwanayo Marekani na kuendeleza masuala ya mitindo nyumbani?

HELLEN: Yah! ni kweli nimewahi kushinda Shindano la Miss Universe mwaka 2010. Lakini nilisomea biashara na sikutaka kung’ang’ania kitu ambacho hakiniletei faida hasa kwenye suala zima la kifedha.

OVER ZE WEKEEND: Wazo la kuwa na ‘products’ zako mwenyewe lilitoka wapi?

HELLEN: Kwa kweli wazo lilikuja tu bila kutegemea. Ilikuwa ni siku moja nimetoka kuoga nikawa napaka mafuta ya ubuyu nikajikuta tu najiuliza kwani siwezi kuwa na sabuni za mafuta haya? Baadaye nikaingia mtandaoni na kuanza kusoma kuhusu vipodozi vya asili baadaye nikaomba wazazi wangu kuniwezesha na kwenda kusomea masomo yanayohusu vitu hivyo nchini Malaysia na baada ya hapo ndiyo kama hivi nina bidhaa zangu ambazo ziko tano. Sabuni za kuogea, mafuta mepesi ya kupaka, Mafuta halisi ya nazi, body scrub na zingine pia.

OVER ZE WEKEEND: Changamoto gani ambazo umekutana nazo wakati unaanza?

HELLEN DAUSEN: Sana ilikuwa ni kukatishwa tamaa, wengi walikuwa wananiambia kwa nini nisifanye mambo mengine, wengine wakinisema kuwa nachomeka juani na nisingefika popote lakini Mungu mkubwa nilipambana na wazazi wangu walinisapoti mpaka nimefika hapa.

OVER ZE WEEKEND: Forbes Afrika walipataje taarifa kuhusu wewe?

HELLEN: Mimi ndiye niliona tangazo la fomu yao kwenye Ukurasa wa Instagram zikihitaji kuwafahamu wajasiriamali ambao wanahisi biashara zao ndani ya miaka michache zinaweza kuwafanya kuwa mabilionea. Kwa hiyo baada ya kuiona nikaijaza na kawaida ya Forbes huwafanyia uchunguzi wahusika wanaojaza fomu hizo zaidi ya miezi mitano. Hilo lilifanyika na nikaibuka kuwa mmoja wa watu waliokuwa wanawahitaji.

OVER ZE WEKEEND: Baada ya Forbes kukutaja katika orodha yao hiyo imekusaidia vipi kibiashara?

HELLEN: Watu wameongeza imani zaidi kwenye bidhaa zangu. Nakumbuka kabla kuna makampuni niliyafuata ili kunisapoti kwenye suala zima la mtaji lakini hayakuonesha ushirikiano, baada tu ya kutangaza yamenitafuta na tunafanya kazi tena pamoja.

OVER ZE WEKEEND: Shughuli zako hasa unazifanyia wapi kwa sasa? Umeajiri watu wangapi na vipi kuhusu tetesi kuwa una mpango wa kujenga kiwanda?

HELLEN DAUSEN: Makao makuu yangu kibiashara kwa sasa ni Zanzibar, watu niliowaajiri si zaidi ya 10. Lakini ni wengi kidogo maana kuna ambao wananisaidia hapo Zanzibar na wengine Dar ila kuna uwezekano wa kuajiri wengine zaidi kutokana na ukomavu wa biashara. Kuhusu kujenga kiwanda nina mpango huo na malengo nikufikia mwaka ujao niwe nimekijenga.

OVER ZE WEKEEND: Kuna namna yoyote serikali inakusapoti tangu Forbes wakutangaze?

HELLEN: Hapana bado haijaanza kunisapoti.

OVER ZE WEKEEND: Vipi kuhusu familia, umeolewa au una watoto?

HELLEN DAUSEN: Hapana sijaolewa, sina mtoto na wala siko katika uhusiano wowote ule.