RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

HOJA: TUSIMLAZIMISHE MUNGU KUFANYA MAPENZI YETU


Siku hizi tunaishi katika ulimwengu wa ibada na huduma za maombezi ambayo maelfu ya watu wanahudhuria kwa ajili ya kumtafuta Mungu awatatulie matatizo yao. Kwa upande mmoja tunaweza kuona kama hii ni dalili nzuri ya kumtumaini Mungu kwa mahitaji yetu. Lakini upande wa pili ni changamoto kwa wengi ambao wanamkimbilia Mungu kwa matumaini lakini hawapokei mahitaji yao kutoka kwa MUngu kama walivyotarajia. Je Mungu amekuwa mwongo? La hasha, Mungu si mwanadamu hata aahidi uongo. Lakini pia Mungu hawajibiki kufanya mapenzi yetu sisi. Na huu ndio ujumbe wa wiki hii:

Sio kila maombi 
Mungu atajibu ndiyo

Biblia imeandika mengi kuhusu umuhimu wa maombi kwa kila mchaji Mungu aliyeko duniani. Aidha, Mungu mwenyewe amehimiza kila mwenye kumcha amwite kwa njia ya maombi na kuna ahadi zake nyingi sana za kujibu maombi ya kila mwombaii


Pamoja na ukweli huu wa kibiblia, uhalisia wa mambo sivyo ulivyo kwa kila mtu anayemwomba Mungu. Tena naweza kuwa na ujasiri wa kusema miongoni mwa waombaji wengi wenye kupokea majibu ya “ndiyo” ni wachache na maombi yanayojibiwa ni kidogo sana. Nasema hivi sio kwamba nimepungukiwa na imani kwa Mungu, la hasha. Nataka kuwa mkweli kwa Neno la Mungu jinsi lisemavyo kuhusu suala la Mungu kujibu maombi.


Pamoja na kwamba Neno la Mungu limetuhimiza kumwomba Mungu, na limetuhakikishia kwamba tutapokea majibu ya maombi yo yote tuyaombayo; lakini Neno la Mungu hilo hilo limetutahadharisha kwamba si kila maombi tuombayo Mungu ajibu “Ndiyo”! Kwa maelezo mengine ni kwamba si maombi yote tuombayo tunaomba vizuri. Haya yanashuhudiwa na Neno la Yakobo alipoandika akisema: “Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu.” (YAK.4:3)


Maandiko haya yanagusa hoja yangu moja kwa moja kwamba si maombi yote tuombayo lazima yatajibiwa na Mungu kwa kufanya kama tuombavyo. Hapa Yakobo anashuhudia hali halisi iliyokuwepo katika jamii ya waaminio wa enzi za karne ya kwanza ambao walikuwa wanalalamika kwamba wamemwomba Mungu lakini hawajapokea majibu ya ndiyo kama walivyoomba.


Yakobo anatoa sababu ambayo ilikuwa ni kikwazo kwa Mungu kujibu “ndiyo” maombi yao. Sababu iliyotajwa ni tamaa binafsi ambazo ziliwasukuma kuomba fedha na mali za kujinufaisha wenyewe. 


Hata hivi leo tunashuhudia watu wengi wakidhuhuria kwenye ibada na huduma za maombezi ambapo wanaombewa kupokea Baraka za kiuchumi, lakini wengi hawapokei majibu ya ndiyo kutoka kwa Mungu kwa sababu ya ukweli huu kwamba wanaomba vibaya, na wanataka wakipokea Baraka hizo wazitumie kwa manufaa ya wenyewe na sio kwa ajili ya kuendeleza ufalme wa Mungu.


Vipi wewe ndugu yangu? Umewahi au unapitia kwenye changamoto hii ya kutokujibiwa na Mungu ndiyo maombi yako? Jitathmini nia yako ya ndani. Mungu anaijua nia yako ya ndani kuliko maombi yako ya mdomoni. Mungu hawezi kuvunja ahadi alizoweka kwa waombaji na hawezi kukiuka Neno lake. Si kila maombi tuombayo atajibu ndiyo. Majibu ya ndiyo kwetu yatategemea nia ya ndani ya kuomba kwetu na matumizi ya majibu ya maombi hayo yatakuwa na manufaa gani kwa ajili ya Ufalme wa Mungu.





Si kila kufunga kuna
thawabu ya Mungu


Biblia imeandika habari za kufunga zaidi ya mara mia moja. Kufunga pia limechukua kiasi cha 61.8% katika Agano la Kale na kiasi cha 38.2% katika Agano Jipya. Humo kuna maelezo mazuri yanayofundisha kwa kina kuhusu kufunga, faida na changamoto zake kama masharti hayakuzingatiwa. Kimsingi suala zima la kufunga limejumuishwa na maombi au sala au dua kwa Mungu. Ni tendo la unyenyekevu na kujidhili mbele za Mungu ili sala na dua zetu zipate kusikilizwa na kujibiwa na Mungu.


Lakini, kama ilivyo kwa suala la maombi kwamba si yote ambayo Mungu hujibu ndiyo; hali kadhalika na kufunga nako. Si kila kufunga kuna thawabu za Mungu. Haya yanapatikana kwenye mwongozo wa Yesu mwenyewe:


“Tena mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao, ili waonekane na watu kuwa wanafunga. Amin nawaambia, wamekwisha kupata thawabu yao…. Bali wewe ufungapo, jipake mafuta kichwani unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” (Mt.6:16-18)


Katika maandiko haya Yesu anatahadharisha habari za kufunga isivyostahili akionesha kwa kutaja kikwazo cha unafiki. Hapa unafiki lina maana ya kujifanya kwa nje kinyume na uhalisia wa ndani ya moyo. Kujionesha mbele za watu ili uonekane mchaji Mungu wakati moyo umejaa uovu na uasi dhidi ya Mungu. 


Ni hali hii ya unafiki ambayo Yesu anasema kwamba, kufunga kunapofanyika kwa sababu ya kupata sifa kwa watu mfungaji anaishia kupata sifa hiyo ambayo kimsingi sio thawabu kutoka kwa Mungu. Na ile thawabu ya kufunga kutoka kwa Mungu inakuwa batili kwa mfungaji mnafiki. Thawabu ya kufunga kutoka kwa Mungu hupatikana kwa Mungu pale ambapo mfungaji amedhamiria kutoka moyoni kumtafuta Mungu kwa faragha pasipo kujionyesha kwa watu ili kupata sifa kutoka kwao. 


Vipi mwenzangu? Umewahi kukutaka na changamoto hii ya kufunga na kuomba lakini hupati matokeo mazuri ya kufunga kwako? Mahali pa kuanzia kujua kikwazo ni katika nia ya ndani ya moyo. Usipende kufanya usanii kwa mambo makini kama kufunga. Kuwa mkweli na kuzingatia Neno la Mungu lisemavyo kuhusu kufunga ndipo utaona matokeo yake mazuri.


Si kila kutoa kuna
thawabu ya Mungu


Jumbe mbili zizopita zilihusu habari za “maombi” na “kufunga”! Leo ninawasilisha ujumbe unaohusu utoaji. Kama ilivyo kawaida suala la kutoa katika Biblia limeandikwa mara 880! Katika Agano la Kale limechukua kiasi cha 75% na katika Agano Jipya limmechukua kiasi cha 15%! Kutoa kwa mujibu wa Biblia kuna Baraka nyingi za kiuchumi na hasa pale masharti ya kiimani yanapokuwa yamezingatiwa. Hata hivyo, tukirudi kwenye uhalisia tunakutana na changamoto ya watu kutokupata thawabu ya Mungu itokanayo ya utoaji wao.


Ninatambua pia kuwepo kwa nadharia tofauti kuhusu mtoaji kupata thawabu ya utoaji wake. Kuna nadharia inayofundisha kwamba thawabu ya kutoa haipatikani duniani mpaka siku ile ya hukumu ya mwisho mbele za Mungu. Nadharia nyingine inafundisha kwamba thawabu ya kutoa hupatikana hapa hapa duniani ili kila mtoaji anufaike na thawabu hiyo na huko mbinguni ni thawabu za kiroho tu.


Nadharia zote hizi zina ukweli kiasi fulani na sehemu nyingine zimepungukiwa na tafsiri makini ya maandiko vile yasemavyo. Ukweli wa kimaandiko ni kwamba thawabu ya kutoa hupatikana kuanzia duniani na kilele chake ni hazina za kiroho mbinguni; na hapo ni kama mtoaji atakuwa alimaliza vema safari yake ya maisha ya hapa duniani. Ndiyo maana Yesu alisema kwamba, kutoa ni kuweka hazina mbinguni lakini thawabu ya kutoa inapatikana mtu akiwa duniani. Swali la kujihoji ni kwa kiasi gani kila mtoaji anaipata thawabu ya kutoa kwake hapa duniani? 


Tukizingatia kanuni ya uhalisia watu wengi wametoa sadaka sana, tena kwa wingi na wengine kwa muda mrefu. Lakini wengi wao hawajapokea thawabu ya utoaji wao kama vile walivyotarajia wakati walipokuwa wanatoa. Tatizo ni nini? Turejee kwenye masharti ya kutoa sadaka kwa Mujibu wa Yesu Kristo mwenyewe:


“Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu. Amin nawaambieni, wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe utoapo sadaka, hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba yako aonaye sirini atakujazi.” (MT.6:2-4)


Kikwazo ni kile kile. Unafiki. Kujionyesha kwamba ni mtoaji. Kila kutoa kunakosukumwa na kutaka kujulikana na kusifiwa kunabatilisha thawabu ya kutoa kutoka kwa Mungu. Hii haina maana kwamba sadaka haitakiwi kujulikana immetolewa na nani. Kinachokatazwa na ni nia ya mtoaji anapotaka kujulikana na watu kuwa ni “mtoaji bora” kuliko wengine! 


Yesu anasema mtoaji mnafiki anaishia kupata sifa za watu lakini hawezi kupata thawabu ya kutoa kwake kutoka kwa Mungu kwa sababu nia yake ya ndani ya moyo haikuwa kumpendeza Mungu bali wanadamu.