RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KAKA YAKE RAIS OBAMA ASEMA ATAMPIGIA KURA TRUM


Ndugu wa damu wa Rais wa Marekani Barack Obama, ambaye ni kaka wa kambo Malik Obama, ametangaza kuwa atampigia kura mgombea urais wa Chama cha Republican, Donald Trump huku akisisitiza kutounga mkono Chama cha Democratic cha Rais Obama ambacho mgombea wake ni Hillary Clinton.
Malik amesema anampenda sana Bw Trump kutokana na “uwazi wake” na kuongeza kwuwa amesikitishwa sana na uongozi wa Rais Obama.
Akiongea na Shirika la Utangazaji la Uingereza la BBC, Malik amesema kwamba anaamini Bw Trump, ni mtu mwenye huruma, mkweli na mwenye ushawishi.
“Akizungumza kwenye runinga anaonekana mtu anasemaye ukweli, kuhusiana na dunia kwamba imeharibika na hakuna usalama,” amesema Bw Malik.

Malik, 58, kwa muda mrefu alikuwa mfuasi wa Chama cha Democratic lakini anasema utawala wa nduguye umemfanya kubadilika na kuanza kuunga mkono Bw Trump.

Akizungumza awali na gazeti la New York Post la Marekani, Malik alisema jambo lililomtamausha zaidi ni hatua ya Mkuu wa Shirika la Ujasusi la Marekani, FBI, James Comey kupendekeza Bi Clinton asishtakiwe kutokana na hatua yake ya kutumia anuani binafsi ya barua pepe akiwa waziri wa mambo ya nje.
Hajafurahia pia kwamba Bi Clinton na Rais Obama waliongoza vita vilivyopelekea kuuawa kwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi ambaye anasema ni mmoja wa marafiki zake wakuu.
Pia, hafurahishwi na hatua ya chama cha Democratic cha Marekani kuunga mkono ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
“Nampenda Donald Trump kwa sababu anazungumza kutoka moyoni. Ningependa kukutana naye,” anasema.
Baba yao Barack Obama Sr., aliondoka Kenya mwaka 1959 Malik alipokuwa na umri wa mwaka mmoja na akajiunga na Chuo Kikuu cha Hawaii, ambapo baadaye alikutana na mama’ke Rais Obama, Stanley Ann Dunham akamuoa.
Malik Obama alikutana na Barack Obama 1985. Wawili hao hata hivyo wamekuwa wakigombana. Malik amekuwa akimshutumu nduguye akisema hamsaidii.
Malik aliwania ugavana Siaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2013 lakini akashindwa. Amesema amejiandikisha kama mpira kura katika jimbo la Maryland na anapanga kupiga kura mwezi Novemba.
Bw Malik amesema hakuna uhasama mkubwa kati yake na Rais Obama lakini hamuamini sana. Amesema wakati Rais Obama alipokuwa akiomba kura alizungumza sana zake Kenya lakini alipoingia uongozini hajakuwa akiwasiliana nao sana.

CHANZO: BBC