RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KUTIMULIWA NCHINI KENYA, KOFFI AMEVUNA ALICHOPANDA

Koffi Olomide akimpiga mnenguaji wake.


Na Andrew Carlos
AMEVUNA alichopanda! Unaweza sema hivyo kwa maana nyingine baada ya wikiendi iliyopita ndani ya Kenya kutawala kwa sakata jingine la mwanamuziki mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Koffi Olomide la kumshambulia dansa wake wa kike aliyejulikana kama Pamela.

Koffi Olomide.

Koffi a.k.a Le Grand Mopao amekuwa na matukio yanayomuweka hatiani na hili alilolifanya la kutimuliwa nchini Kenya limedhihirisha kuwa amevuna alichopanda.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2012, staa huyo aliwekwa jela miezi mitatu nchini mwao kwa kosa la kumshambulia prodyuza wake, Diego Lubaki baada ya kuombwa kulipwa pesa ya kutengeneza video.

La Kenya ilikuwaje? 

Koffi alialikwa kufanya shoo siku ya Jumamosi (wikiendi iliyopita) nchini Kenya katika Ukumbi wa Bomas na ilipofika Ijumaa alikuwa amewasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Akiwa ameambatana na madansa wake wa kike kama ilivyo ada ya waandishi, alifanyiwa mahojiano na moja ya TV nchini humo (Citizen) na akiwa katikati ya mahojiano hayo alisikia ugomvi nyuma yake baina ya madansa wake ndipo alipoachana na mahojiano na kumvamia mmoja wa madansa wake (Pamela) na kumpiga mateke hadi pale alipoamuliwa na maafisa wa polisi wa uwanja huo.

Wakenya wacharuka 

Baada ya kipande cha video kusambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha udhalilishaji huo. Wakenya kwa ujumla waliungana na kukemea kitendo cha staa huyo anayebamba na Wimbo wa Selfie kuwa atimuliwe nchini humo, hafai na ameonesha kuwadhalilisha wanawake. Wakenya hao waliungana kwa kukataa msanii huyo kufanya shoo nchini humo na akamatwe mara moja kwa kuweka Hash Tag (KickKoffiOlomideBackToCongo) kwenye mtandao wa Twitter.

Ajitetea 

Koffi alijitetea kuwa hakukusudia kumsha-mbulia Pamela na kwamba kwanza aliona kama dansa huyo alitaka kuibiwa pochi hivyo alienda kuamulia. Pili anasema alikuwa anajaribu kumtetea kwani mmoja wa maafisa wa kike katika uwanja huo wa ndege alikuwa akiwasumbua madansa wake.

Atimuliwa 

Baada ya taarifa kusambaa, mkuu wa polisi nchini, Kenya Joseph Boinnet alitoa taarifa na kuwaagiza polisi wachukue hatua ambapo Ijumaa usiku alifukuzwa kwa kusafirishwa na Shirika la Ndege la Kenya Airways kwenda kwao, Kinshasa.

Wakenya wameonesha mfano 

Wakenya wameonesha mfano wa kuigwa hata nchini kwetu kwa kuungana pamoja na kukemea unyanyasaji wa wanawake. Wameonesha kuwa ukatili kwa wanawake hautakiwi katika jamii na siyo kwa wanawake wa nchi yao bali kote duniani kwani dansa aliyepigwa na Koffi hakuwa Mkenya bali ni Mkongo.

Ameleta hasara kubwa 

Kwa alichokifanya Koffi, kwanza ameingiza hasara kubwa kwa promota aliyeandaa shoo hiyo, pia amepoteza muda na kiasi kikubwa cha pesa kuanzia gharama ya hoteli, ukumbi, usafiri na vingine vingi.