RUMAFRICA Magazine

MelK Premium Suits

TANGAZO MUHIMU

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

BISHOP DR. M.E. ADMIN

BISHOP DR. M.E. ADMIN

SANDLANDS HOTEL KARIAKOO

HATUA 5 ZA KUMFIKISHA KORTINI MWENYE MAKOSA YA MTANDAO

Na Hashim Aziz

Septemba Mosi, 2015, Sheria ya Makosa ya Mtandao (The Cybercrimes Act, 2015) ilianza kutumika rasmi nchini Tanzania, baada ya muswada wake kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa sheria lakini uchunguzi wa gazeti hili, umebaini kwamba bado wengi hawajui namna ya kuitumia sheria hiyo.

Licha ya kupungua kwa kiasi kikubwa kwa makosa ya mtandao tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, bado vipo vitendo vya uvunjaji wa sheria vinavyoendelea kutokea kila kukicha, ikiwemo watu kutukanwa mitandaoni, kupostiwa kwa picha za utupu, kutishiwa maisha na kudhalilishwa.

Zikiwa zimesalia siku kadhaa kutimia kwa mwaka mmoja tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, gazeti hili limechimba hatua tano zinazoweza kutumika kumfikisha mhalifu wa makosa ya mtandao kortini pamoja na mbinu ambazo kila mmoja anapaswa kuzifuata ili kuwa salama na sheria hii.

HALI ILIVYOKUWA AWALI

Kabla ya kupitishwa kwa sheria hiyo ya makosa ya mtandao, wimbi la matukio ya watu kudhalilishwa mitandaoni, ikiwemo kuwatumia meseji za matusi, kuposti picha zao za utupu kwenye mitandao ya kijamii kama Facebook, Instagram na mingineyo, kuibiwa pesa kwa njia za mtandao wa simu sambamba na kudukua (hacking) akaunti za watu kwenye mitandao ya kijamii, lilikuwa kubwa na lilifikia hatua ya kutishia usalama wa wananchi na mali zao.

Hata hivyo, tangu kuanza kutumika kwa sheria hiyo, makosa hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa ingawa bado hayajakoma kabisa. Wanaofanyiwa makosa hayo, kama wanajua nini cha kufanya, sheria imekuwa ikiwasaidia kupata haki zao lakini kama ulikuwa hujui nini cha kufanya ili kupata haki yako, mwandishi wetu amewasiliana na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambao wametoa ufafanuzi ufuatao.

TCRA WANASEMAJE?

Wiki iliyopita, mwandishi wetu alifunga safari mpaka makao makuu ya TCRA na kufanikiwa kuzungumza na Afisa Mawasiliano Mkuu, Semu Mwakyanjala kuhusu sheria ya makosa ya mtandao na hatua za kufuata sheria inapovunjwa.

Kabla ya yote, Mwakyanjala alimueleza mwandishi wetu kwamba sheria hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza makosa ya kimtandao ingawa bado wapo wanaoendelea kuvunja sheria ambao nao wanakumbana na dola.

Alipoulizwa ni makosa mangapi mpaka sasa yamesharipotiwa kwake na namna walivyoyashughulikia, Mwakyanjala alisema wao hawashughuliki na wahalifu wa kimtandao moja kwa moja badala yake, huwa wanaletewa taarifa na jeshi la polisi, kitengo cha Cyber Crime Unit ambao ndiyo wanaoshughulika moja kwa moja na wanaovunja sheria hiyo.

Mwakyanjala akaongeza kuwa taarifa zaidi, anaweza kuwa nazo bosi wake, Innocent Mungi ambaye ndiye Meneja wa Mawasiliano wa TCRA. Akamtaka mwandishi wetu kumtafuta Mungi kupitia namba ya simu ya mkononi aliyomtajia mwandishi wetu.

HATUA TANO ZA KUFUATA

Mwakyanjala alimueleza mwandishi wetu kwamba licha ya kuwepo kwa sheria hiyo, bado watu wanaojitokeza kuomba msaada wa kisheria ni wachache, akaeleza kuwa huenda Watanzania wengine ni waoga au hawajui taratibu. Mwandishi wetu alipomuuliza taratibu za kufuata mtu anapofanyiwa makosa ya kimtandao, Mwakyanjala alitoa ufafanuzi wa nini cha kufanya.
HATUA YA KWANZA

Mtu anapofanyiwa makosa ya kimtandao, iwe ametukanwa, picha yake ya utupu imepostiwa mtandaoni, akaunti yake imedukuliwa, ameibiwa pesa au vinginevyo, hatua ya kwanza anatakiwa kwenda polisi kuripoti tukio hilo akiwa na vielelezo vyake.
HATUA YA PILI

Baada ya kufungua jalada kituo cha polisi, mshtaki atasaidiana na polisi kuwasiliana na kitengo cha Cyber Crime Unit kilichopo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi (Wizara ya Mambo ya Ndani ) ambao nao wataanza kulichunguza kwa kina suala hilo.
HATUA YA TATU

Baada ya kuchunguza kwa kina, polisi wa kitengo cha Cyber Crime kama watahitaji ushahidi wa kitaalamu zaidi, watawasiliana na makao makuu ya TCRA ambao watawapa maelezo yote kwa kina, kuhusu mtu aliyefanya uhalifu huo, mahali ulipofanyika, muda na jinsi ulivyofanyika.

Polisi hao wa Cyber Crime Unit, watashirikiana na polisi wa kituo ilipofunguliwa kesi na mhusika mwenyewe.
HATUA YA NNE

Baada ya vielelezo vyote kukamilika ikiwa ni pamoja na ushahidi, mtuhumiwa atakamatwa na polisi na kufunguliwa jalada la mashtaka kulingana na makosa aliyoyafanya.
HATUA YA TANO

Mtuhumiwa atapandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka yanayomkabili ambapo akikutwa na hatia, atahukumiwa kulingana na uzito wa kosa alilolifanya ambapo hukumu inaweza kuwa ni kwenda jela, kulipa faini au vyote kwa pamoja.