RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

RAIS EDGAR LUNGU ANAONGOZA KURA ZAMBIA, WAPINZANI WAPINGA!


Rais Edgar Lungu.

Lusaka, Zambia.
Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais wa Zambia yaliyotangazwa leo Jumatatu na Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), ambapo asilimia 85 ya majimbo yote yamekwisha hesabiwa, yanaonyesha kuwa Rais Edgar Lungu anaongoza, huku wapinzani wakipinga matokeo hayo kwa madai kuwa hesabu zao zinaonyesha mgombea wao ndiye anayeongoza kama kura hazijachakachuliwa.

Lungu anakabiliwa na upinzani mkali wa Hakainde Hichilema, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Muungano kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND).

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ), Rais Lungu amepata asilimia 50.14 dhidi ya 47.7 alizopata mpinzani wake, Hichilema baada ya kura za majimbo 132 kati ya 156 kuhesabiwa.

Taarifa iliyotolewa na UPND imeeleza kuwa mfumo wao wa kuhesabu kura ulioenda sambamba na ule wa ECZ umeonyesha Hichilema amemshinda kwa kura za kutosha Lungu baada ya asilimia 80 ya kura zote kuhesabiwa.

Vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mkuu nchinio Zambia vina rukhsa ya kuingia kwenye mfumo maalum unaotumiwa na ECZ kuhesabia kura na kuona maendeleo na namna ambavyo mchakato wa kuhesabu kura unbavyoendeshwa.

Maofisa wa ECZ wamevionya vyama vya siasa kutoa taarifa za aina hiyo. Hata hivyo, vyama vyote vina uwezo wa kukusanya matokeo ya upigaji kura na kujumuisha kwa haraka kuliko tume hiyo.

Awali, ECZ ilitarajia kukamilisha kuhesabu kura jana katika uchaguzi huo ambao Wazambia waliwachagua pia wabunge, mameya na madiwani na kuamua juu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, maofisa wa tume hiyo wamesema matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa baadaye bila ya kutaja siku na muda maalumu.