RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SOMO: UJANJA WA MAISHA EXPRESS

Neno express limekuwa la kawaida miongoni mwa watu, likimaanisha jambo linalofanyika kwa haraka. Ndio maana kuna vibao unaweza kukutana navyo ikiwemo, Dobi Express – yaani kwamba dobi huyu hacheleweshi nguo, utazipata ndani ya muda mfupi ukazivae kwa ratiba zako.

Halikadhalika baadhi ya magari yananayotoa huduma ya usafiri kwa watu, huwa na neno express mbele yake, wakimaanisha kwamba utawahi kufika. Kwa siku za hivi karibuni, neno express linaweza kuwa limepata mwenza; mwendo-kasi.

Halikadhalika maisha tuyaishiyo, kuna “ubunifu” umetokea, ambao unaweza kupewa jina express. Katika moja ya vitabu vyake, Askofu T.D. Jakes anasema kwa sasa tunaishi kwenye ulimwengu ambao watu hawana subira, kila kitu ni mwendokasi tu.

“We now live in a fast-food world where nobody wants to wait.” Kwa tafsiri nyepesi ya neno fast food, ni vile vyakula vya chapchap, dakika tatu mkate wako umeandaliwa unaubeba na kuondoka zako ukiutafuna.

Kimantiki, wengi wetu hupenda kuwa na mafanikio ya papo kwa papo, na kusahau kwamba kuna yatokanayo. Fast-food kwa lugha nyingine huitwa junk food. Yaani kwamba chakula kisicho na faida mwilini. Na kuishi kwetu ki-express, kuna mambo ambayo yanatugharimu siku za mbeleni.

Kuna msemo mmoja amewahi kutoa bosi wangu, nami nikapata tafsiri mpya kutokana na sentensi yake, alisema akimuambia mfanyakazi mwenzangu.

“We umekuja juzijuzi tu Arusha afu unategemea uwe na makoti mengi kama mimi.”

Hapa mjadala ulikuwa kuhusu hali ya hewa ya baridi ilivyo kwenye Jiji letu hili, ambapo ilionekana bosi wetu ana makoti mengi, tena mazuri. Lakini muulizaji ambaye amehamia kutoka mji wenye joto, ni lazima angepata uzoefu kidogo kidogo na kuendelea kuwekeza kwenye nguo za kujikinga dhidi ya baridi tofauti na mzawa anayejua misimu yote vizuri. Hapa nikajifunza jambo.

Kwamba nimeanza kazi juzi tu afu nitegemee niwe na nyumba na gari zuri, bila kuangalia yahitaji kitambo gani kusubiri na kupata hayo mambo. “Good things come to those who wait”, Nasi Waswahili husema mvumilivu hula mbivu, na pia haraka haraka haina Baraka.

Kama ambavyo una shauku ya kuwa na mafanikio ndani ya muda mfupi, lakini kanuni ya maisha haibadiliki. Kuna njia iliyo sahihi na njia isiyo sahihi. Kitabu cha Mithali 16:8 chaweka bayana;

“Afadhali mali kidogo pamoja na haki, kuliko mapato mengi pamoja na udhalimu”

Acha ionekane kana kwamba ni mtindo wa kisasa “fashion” lakini usijiunge nayo, maana muelekeo wake ni huohuo mmoja. Aidha uwe kwenye mfumo mzuri, ama mfumo usio sahihi. “you either be right or wrong, there is no in-between.”

1 Petro 4:4 “Mambo ambayo wao huona ni ajabu ya ninyi kutokwenda mbio pamoja nao katika ufisadi uleule usio na kiasi, wakiwatukana.”

Acha wakucheke kwamba uko ‘outdated’, lakini wasikutoe nje ya mstari stahiki.

Kuna mtego ambao unaweza kujikuta umeingia ndani yake, na kujitoa ikawa ngumu. Aliyeiba shilingi mia mbili, na aliyeiba milioni 10 wote wana sifa moja, ya wizi. Utofauti pekee ni kiwango walichofanikiwa kukiiba – lakini njia yao wote ni moja.

Mambo huweza kukuwia magumu hata ukatahayari kufanya yale yasiyompendeza Mungu, kwa “kujifariji” kwamba hata Mungu anajua. Ni kweli anajua, lakini unamuangusha pale unaporudi nyuma maana anataka umuite akuonyeshe mambo makubwa na magumu usiyoyajua.

Sio bure Biblia imeainisha kwamba jaribu huja la kiwango chetu, na kwamba Mungu anatupa mlango wa kutokea ili tuweze kustahimili. 

1 Korintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.”

Mstari huu na unatukumbusha ya kwamba kama tukivuta subira japo kidogo tu, hamadi mlango wetu tutakutana nao ambao Mungu ametufanyia.

Ila kuna wale ambao huona ni bora kupeleka mifugo kwa kalumanzila na hata wajanja na matapeli wachache wa mjini, mmoja wao nikakutana naye polisi akisaka ushauri baada ya dawa alipyopewa kutofanya kazi. Jibu la polisi ndilo likanikosha, “mama mpeleke mwanao kwenye maombi, polisi hatuwezi kutibu hilo.” Nikatabasamu sana siku hiyo. Nakuombea usiwe mmoja ya wasaka njia za mkato kufikia mafanikio.