RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

15.09.2016: HABARI LEO REPORT: DK LWAKATARE AWATOA GEREZANI WAFUNGWA 78


MWENYEKITI Bodi ya Parole Taifa, Augustine Mrema amependekeza kufanyike harambee kwenye makanisa na misikiti yote nchini ili fedha zitakazopatikana zitumike kuwalipia faini wafungwa waliopo magerezani na kuisaidia bodi hiyo itekeleze majukumu yake.

Mrema amesema leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akimshukuru Askofu Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto Assemblies of God, Mikocheni B, Dk Getrude Lwakatare kwa kuwatoa gerezani wafungwa 78 kwa kuwalipia faini ya Sh milioni 25 wiki mbili zilizopita.

Amesema pamoja na wafungwa hao kutolewa katika magereza ya Keko, Segerea na Ukonga jijini Dar es Salaam, bado wapo wengine wengi nchi nzima wanaopaswa kutoka magerezani na kumalizia vifungo vyao nje kwa mujibu wa Sheria ya Parole, lakini wameshindwa kwa sababu hakuna fedha za kukamilisha mchakato wa sheria hiyo.

Amesema ili mfungwa atolewe gerezani kuna mchakato mrefu wa kufuata unaohitaji fedha hivyo kutokana na ukosefu wa fedha hizo wafungwa wengi wenye sifa za kutolewa kwa Sheria ya Parole wanaendelea kuteseka magerezani.

“Natoa wito kwa viongozi wa dini zote wamuunge mkono Dk Lwakatare kwa kuwalipia faini wafungwa waliofungwa kwa kukosa fedha za kulipa faini, pia waisaidie Bodi ya Parole ya Taifa ili iweze kutekeleza mchakato wa kuwatoa wafungwa wote wanaostahili kwa mujibu wa sheria hiyo,” amesema Mrema na kumshauri Dk Rwakatare aratibu kazi hiyo na kukusanya michango hiyo kwa kuwa ndiye mwanzilishi wa kampeni hiyo ya kuwakomboa wafungwa kutoka magerezani.

Alishauri ukusanyaji huo wa fedha ufanyike kabla ya sikukuu za Krismasi na mwaka mpya ili wafungwa washerehekee sikukuu hizo wakiwa na familia zao.

Amewataka wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima wakubwa wachangie kwenye kampeni hiyo.

Dk Lwakatare alisema amepokea rasmi jukumu hilo la uratibu, lakini pia awe sauti ya wanyonge, wafungwa na wale waliopotezana na familia zao kwa muda mrefu.

Amesisitiza kampeni hiyo haitakuwa Dar es Salaam tu, bali nchi nzima hivyo wanatarajia kwenda mkoa wa Morogoro kuwatoa wafungwa katika magereza ya huko.

Amesema baada ya kuwatoa wafungwa hao gerezani hakuwaacha hivyo hivyo bali kila mmoja alipewa sabuni, taulo, nguo mpya, nauli na Sh 50,000 kwa ajili ya kujikimu.





CHANZO CHA HABARI: http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/14810-dk-lwakatare-awatoa-gerezani-wafungwa-78