RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

BODI YA UHURU MEDIA GROUP YAJIUZULU


Mwenyekiti wa bodi aliyejiuzulu, Adam Kimbisa.

DAR ES SAALAM: Bodi iliyokuwa inasimamia shughuli za Uhuru Publications leo imejiuzulu kufuatia ziara ya kushtukiza aliyoifanya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli kwenye ofisi ndogo za chama hicho zilizoko Barabara ya Lumumba jijini Dar es Salaam, Jumatatu iliyopita.

Kwenye ziara hiyo mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alipokea malalamiko mengi kutoka kwa wafanyakazi yakiwemo madai ya msingi ya kutopatiwa mishahara kwa muda wa miezi saba.

Taarifa iliyotolewa na msemaji mkuu wa chama hicho imeeleza kwamba Christopher Ole Sendeka imeeleza kwamba mwenyekiti wa bodi Adam Kimbisa amewasilisha barua ya kujiuzulu kwa Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia leo tarehe 22 Septemba 2016.

Kujiuzulu kwa bodi hiyo kumekuja kufuatia madai ya msingi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo ya Uhuru Publications yakiwemo madai sugu ya mishahara pamoja na kutofuatilia madeni sugu kwa baadhi ya wizara serikalini na kampuni binafsi.

Taarifa kamili kuhusu kujiuzulu kwa bodi hiyo hii hapa chini:

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Bodi ya Uhuru Media Group inayosimamia vyombo vya habari vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambavyo ni Uhuru Publications Limited (UPL) wachapishaji wa Gazeti la Uhuru, Mzalendo na Burudani pamoja na Peoples’ Media Communication Limited (PMCL) inayoendesha kituo cha redio Uhuru imejiuzulu kupitia barua ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo Al-haj Adam O. Kimbisa.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwa bodi hiyo leo tarehe 22 Septemba 2016 ambayo nakala yake imenakiliwa kwa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahaman Kinana. Barua hiyo inaeleza kuwa Mwenyekiti pamoja na wajumbe wote wa Bodi hiyo wameamua kwa hiyari yao kujiuzulu nafasi zao.

Bodi ya Uhuru Media Group ndiyo iliyokuwa na majukumu ya kusimamia, kuzielekeza na kuzishauri Menejimenti ya Makampuni hayo na kubuni mbinu na mikakati ya kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa vyombo vya habari vya Chama.