RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KESI YA TUNDU LISSU YAAHIRISHWA TENA


Mchapishaji wa kampuni ya Jamana, Ismail Mehbood akitoka kusikiliza kesi inayomkabili.Wahariri wa Gazeti la Mawio lililofungiwa, Jabir Idrisa, Simon Mkina na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbood wakishuka kizimbani.

Mhariri wa Gazeti la Mawio, Jabir Idrisa akitoka katika chumba cha kusikilizia kesi inayowakabili.Simon Mkina akitoka katika chumba cha kusikiliza shauri lao.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba, leo ameahirisha shauri la kumtaka Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana kwa kushindwa kuhudhuria mahakamani hapo kusikiliza kesi ya msingi inayomkabili, ya kutoa chapisho la uchochezi.

Hatua hiyo, imekuja baada ya wakili wa mshtakiwa, Peter Kibatala, kuieleza mahakama kwamba mteja wake, alishindwa kuhudhuria mahakamani hapo jana kama alivyotakiwa, kwa sababu alisafiri kwenda nje ya nchi kwa dharura, kupata matibabu ya maradhi yanayomsumbua.

Jana katika mahakama hiyo, Simba alimtaka Lissu kufika mahakamani hapo leo, kueleza kwa nini hakufika mahakamani kusikiliza mwenendo wa kesi inayomkabilibaada ya kutoridhishwa na maelezo ya wakili wake juu ya sababu iliyomfanya asifike mahakamani hapo.

Kutokana na maelezo yaliyotolewa leo na Kibatala, Simba ameonesha kuridhishwa na sababu zilizotolewa hivyo kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza kesi ya msingi kuwa ni Oktoba 4, mwaka huu.

Pia Simba aliwaeleza wadhamini wa Lissu kuwa endapo mshtakiwa hatahudhuria tena mahakamani siku iliyotajwa, watatakiwa kulipa dhamana ya mshitakiwa huyo na kuhudhuria kesi zote zitakazokuwa zikiendelea mahakamani hapo.

Hatua hiyo ilikuja baada ya jana, Wakili Mkuu wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi kuomba itolewe hati ya kumkamata Lissu kutokana na kutofika mahakamani kusikiliza shauri linalomkabili.

Lissu na wenzake watatu, wanashtakiwa kwa makosa ya kula njama na kutoa chapisho la uchochezi kupitia Gazeti la Mawio lenye kichwa cha habari ’Machafuko Yaja Zanzibar’, kinyume na Sheria ya Magazeti ya Mwaka 2002.Washtakiwa wengine katika shauri hilo ni wahariri wa gazeti hilo ambalo lilifungiwa na serikali kwa muda usiojulikana, Simon Mkina, Jabir Idrisa na mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehbood.