RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

25.09.2016: WAUMINI WA KANISA LA MLIMA WA MOTO MIKOCHENI WAKIONGOZWA NA BISHOP DR. GERTRUDE RWAKATARE WAKIWAOMBEA WATU WENYE SHIDA MBALIMBALI SIKU YA JUMAPILI

Siku ya Jumapili 25.09.2016 ndani ya kanisa la Mlima wa Moto Mikocheni "B" nguvu za Mungu ziliweza kutanda katika kipindi cha maombezi na uponyaji. Watu wengi sana waliweza kuombewa na watumishi wa Mungu wakiongozwa na Bishop Dr. Gertrude Rwakatare. Mungu aliweza kugusa watu wake wenye shida mbalimbali. Nguvu za Mungu ziliweza kutibua mapepo, majini, na kila kitu kilichokuwa kinawatesa watoto wa Mungu. Watu waliweza kupiga kelele na wengine wakijikuta wanadondoka chini wakati watumishi wa Mungu wakiwagusa mikono yao na kukemea kazi za shetanini.

Hakika tuna kila sababu ya kumshukuru huyu Mungu kwa mambo makuu anayoyafanya katika hekalu lake la Mlima wa Moto Mikocheni "B" kila kuitwapo leo. 

Nasi kama watoto wa Mungu popote tulipo tunatakiwa kufanya kazi ya Mungu na kuwasaidia wale wenye uhitaji. Kuna watu wengi sana wako mitaani wanahangaika, wamefungwa minyororo ya shetani, macho yao yamezibwa wanaona giza na hawaoni nuru, hawafurahi maisha yao kutokana na changamoto za kimaisha, shetani amewabana mpaka wanashindwa la kufanya. Lakini wewe unayo neema ya kupata mwanga na shetani ameshindwa kukukandamiza, sasa ni jukumu lako na kuchukua hatua ya kuwaombea hawa watu na kuwaleta kanisani wakutane na nguvu za Mungu kupitia watumishi wake.

Jitahidi sana unapokuja kanisani ongezana na mtu ambaye hajawahi kuingia katika kanisa hilo unaloabudu ili na yeye aweze kupata upako na hamu ya kutamani kuja kanisani akiwa peke yake au akiongozana na mwingine kama alivyofanyiwa na wewe. Huu ni wakati wa kufanya kazi ya Mungu na kuwaleta watu kwa Yesu, sio wakati wakutamani tu kubarikiwa peke yako wakati ndugu yako anateseka. Mungu akubariki sana na karibu kanisani Mlima wa Moto Mikocheni "B" kila Jumapili saa 3 asubuhi hadi saa 8 mchana.