RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

LIKITEKELEZWA HILI, WASICHANA 83 WA CHIBOK WATAACHIWA HURU NA BOKO HARAM


Siku chache baada ya kuwaachia huru wasichana 21 wa Chibok, Kundi la kigaidi la Boko Haram kutoka Nigeria limeeleza juu ya utayari wake wa kuwaachia huru wanafunzi wengine wa kike waliowateka nyara zaidi ya miaka miwili iliyopita.


Taarifa ya Garba Shehu, ambaye ni msemaji wa Rais wa Nigeria amesema kundi hilo la kigaidi limetangaza kuwa tayari kuwaachia huru wanafunzi wengine 83 iwapo serikali itakubali kuketi kwenye meza ya mazungumzo na wanamgambo hao. Aidha msemaji wa Rais amesisitiza kuwa serikali iko tayari kufanya mazungumzo na kundi hilo la kigaidi kuhusiana na kuachiwa huru wanafunzi hao.


October 13, 2016, wanafunzi 21 wa Shule ya Upili ya Chibok waliachiwa huru katika eneo la Banki, kwenye mpaka wa Nigeria na Cameroon, katika kile kilichotajwa kuwa makubaliano maalumu baina ya serikali ya Abuja na kundi la Boko Haram. Garba Shehu, msemaji wa Rais wa Nigeria alithibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Shirika la Msalaba Mwekundu na serikali ya Uswisi ndizo zilizofanikisha kuachiliwa huru wasichana hao. 

Juhudi mbalimbali yakiwemo maandamano ya kimataifa ya amani yamekuwa yakifanyika kwa ajili ya kushinikiza kuachiwa huru wasichana wote waliotekwa nyara na kundi la Boko Haram.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 14 Aprili 2014, kundi hilo la kigaidi liliwateka nyara wanafunzi 276 wa kike katika eneo la Chibok, wakati wasichana hao walipokuwa wanafanya mtihani. Wasichana 57 walifanikiwa kutoroka mara baada ya kutekwa nyara na genge hilo.