RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MSAJILI AMTAMBUA LIPUMBA, MAALIM SEIF


Profesa Ibrahim Lipumba.

OFISI ya Msajili wa Vyama ya Siasa imetoa orodha ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na viongozi wa vyama hivyo ambako inasisitiza kuwa Profesa Ibrahim Lipumba ndiye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) na Katibu Mkuu ni Seif Shariff Hamad.

Kwa mujibu wa barua hiyo ya Oktoba 4, 2016 iliyoandikwa kwenda kwa makatibu wakuu wa vyama vyenye usajili wa kudumu, Profesa Lipumba ambaye Baraza Kuu la chama hicho limetangaza kumfukuza uanachama, anaonekana kwenye orodha hiyo kama Mwenyekiti wa CUF.

Jina la Profesa Lipumba ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo mwaka jana, limerejeshwa kwenye orodha na Msajili wa Vyama ya Siasa baada ya yeye mwenyewe kutangaza kutengua barua yake ya kujiuzulu.



Katibu Mkuu wa CUF, Seif Shariff Hamad.

Kwa hatua hiyo ya Msajili, uteuzi wa Julius Mtatiro ambao umefanywa na Baraza Kuu kuongoza Kamati ya Uongozi ya CUF hautambuliwi na Ofisi ya Msajili wa Vyama ya Siasa.

Uamuzi huo wa Ofisi ya Msajili umekuwa unalalamikiwa na upande unaoongozwa na Maalim Seif kuwa unakiuka Katiba ya CUF wakati yeye akisisitiza kuwa yuko sahihi kumtambua Profesa Lipumba kwa mujibu wa Katiba hiyo.

“Baada ya zoezi la uhakiki na utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa kwa vyama vyenye usajili wa kudumu kukamilika, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imehuisha taarifa za vyama vya siasa zilizopo katika orodha ya vyama vya siasa.

“Hivyo pamoja na barua hii, nawasilisha orodha ya vyama ya siasa ilivyo leo tarehe 4 Oktoba 2016 kwa taarifa na kumbukumbu zenu. Endapo kuna taarifa ambayo siyo sahihi mnaombwa kuwasiliana na ofisi ya msajili wa vyama ya siasa mapema iwezekanavyo ili irekebishwe,” ilisema barua hiyo.

Barua hiyo imevitaja vyama 22 ambayo vina usajili wa kudumu na chama cha mwisho kusajiliwa ni Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo) ambacho viongozi wake ni Anna Mghwira ambaye ni Mwenyekiti na Katibu Mkuu ni Juma Sanani.

Chama hicho kilipata usajili Mei 5, 2014. Vyama vingine ni Chama Cha Mapinduzi ambacho Mwenyekiti wake ni John Magufuli na Katibu Mkuu ni Abdulrahman Kinana. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mwenyekiti wake ni Freeman Mbowe na Katibu Mkuu ni Dk Vincent Mashinji.

Chama kingine ni Union for Multiparty Democracy (UMD) ambacho Mwenyekiti wake ni Kamana Masoud na Katibu Mkuu ni Moshi Kigundula. Chama cha National Convention for Construction and Reform (NCCR-Mageuzi) Mwenyekiti wake ni James Mbatia na nafasi ya katibu iko wazi.

Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD) bado kinaonesha kuwani marehemu Oscar Makaidi na Katibu wake ni Tozy Matwanga, United Peoples’ Democratic Party (UPDP) Mwenyekiti ni Fahmi Dovutwa na Katibu Mkuu ni Hamadi Ibrahim, National Reconstruction Alliance (NRA) Mwenyekiti ni Marsheed Humudi na Katibu Mkuu ni Simai Abdullah.

Chama cha Haki na Ustawi (CHAUSTA) kwa mujibu wa orodha hiyo Mwenyekiti ni James Mapalala, Katibu Mkuu ni Mwaka Mgimwa, Chama cha Democratic Party (DP) nafasi ya Mwenyekiti iko wazi na Katibu Mkuu ni Georgia Mtikila. Chama hicho kilikuwa kinaongozwa na Mchungaji Christopher Mtikila ambaye alifariki kwa ajali ya gari.

African Progressive Party of Tanzania (APPT-Maendeleo) kinaongozwa na Mwenyekiti wake wa siku nyingi Peter Mziray, Katibu Mkuu ni Nziamwe Samwel, Jahazi Asilia kinaongozwa na Kassim Bakari Ali na Katibu Mkuu ni Mtumweni Jabir Seif, Sauti ya Umma (SAU) Mwenyekiti ni Paul Kyara na Katibu Mkuu ni Ali Kaniki.

Tanzania Farmers Party (AFP) kinaongozwa na Said Soud Said na Katibu Mkuu ni Rashid Ligania Rai, Chama cha Kijamii (CCK) Mwenyekiti wake ni mwanahabari wa siku nyingi Constantine Akitanda na Katibu Mkuu ni Renatus Muabhi, Alliance for Democratic Change (ADC) Mwenyekiti ni Hamad Rashid Mohamed na Katibu Mkuu ni Doyo Hassan Doyo wakati Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kinaongozwa na Hashim Rungwe na Katibu Mkuu ni Ali Omar Juma.