RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SABABU ZA KUJIPONGEZA MWENYEWE KAMA UNAFANYA HIVI

Mara nyingi tunasongwa na tamaa za matarajio ya ndoto zetu kiasi kwamba tunasahau kujifanyia nafasi ya kujipongeza kwa yale mengi au machache tunayoyafanikisha.

Isikupite hii: Madhara ya mazoea

Unaweza kufikiri kuwa hakuna haja ya kujipongeza mwenyewe baada ya mafanikio ya jambo fulani, huu ni uongo ambao akili yako inataka kukuaminisha, kwani zipo sababu millioni za kujipongeza mwenyewe lakini kwa siku ya leo nitakutajia sababu 12 tu, kama ifuatavyo; –

1. Kama umejiwekea malengo fulani.

Kama umejiwekea malengo au una ndoto ambazo umeziwekea rehani maisha yako kuzitimiza, unayo sababu ya kujipongeza. Si kila mtu anaweza kujivunia kuwa na malengo au ndoto, unapaswa kufahamu ya kuwa mafanikio yoyote huanza na ndoto na malengofulani.

2. Kama unaweza kujifunza kutokana na makosa.

Nina uhakika kuwa kila mmoja wetu amewahi kushindwa katika jambo fulani, ingawa hakuliachia tatizo nafasi ya kuyakwamisha malengo yake, kwakuwa maisha hayaishii katika vikwazo pekee. Kama utajifunza kutokana na makosa, utakuwa umetwaa sifa ya kustahili kuitwa mtu mwenye busara. Hivyo unastahiri pongezi binafsi kwakuwa mwenye busara.



3. Kama wewe ni sababu ya furaha kwa wengine.

Kama wewe ni sehemu ya furaha kwa mtu mwingine, una kila sababu ya kujipongeza kwakuwa unamwangazia upendo katika maisha yake. Dunia itakuwa salama kama kila mtu angesambaza upendo kwa wengine.

4. Kama ni muhamasishaji wa wengine.

Kama unawahamasisha watu au umewahi kuwa chachu ya mafanikio ya mtu yeyote katika maisha yetu ya kila siku, unayo sababu ya kujipongeza. Hisia itokanayo na hili jambo ni sifa ya pekee sana, ambayo hata pesa haiwezi kuinunua.

5. Kama wewe ni msaada kwa wengine.

Siku zote tunazungukwa na watu waliopungukiwa au wasio na kitu kitu kabisa, na kama wewe ni mmoja kati ya watu waliojawa na upendo kiasi cha kumkunjulia muhitaji mkono wako, hasa pale unapokuwa na uhiari na nafasi binafsi. Una kila sababu ya kujipongeza kwakuwa dunia inahitaji sana watu kama wewe.

6. Kama hukati tamaa.

Uwezo wa kutokata tama ni uwezo walionao wachache na kama unaumiliki uwezo huu wa pekee unastahili pongezi binafsi. Ni moja ya nguzo muhimu ya mafanikio.

7. Kama umeweza kusonga mbele kwa kuachana na mambo ya kuumiza yaliyopita.

Kusonga mbele ni sehemu muhimu sana ya maisha,na ukweli unabaki kuwa si jambo rahisi. Matatizo mengi unayo yaona katika maisha ya watu yanasababishwa na uamuzi wa mtu kukataa kuachana na vikwazo fulani vya kuumiza alivyowahi kuvipata katika maisha yake kwa mfano;- 

Isikupite hii: Nguvu aliyonayo mwanamke

Mwanamke au Mwanaume anayemua kuyachukia mahusiano ya mapenzi kutokana na sababu za kuwahi kutendwa na mwezi wake aliyempenda kwa dhati, hatimaye anautesa moyo wake kila kukicha kwa manung’uniko licha ya uhitaji wa kuwa na mpenzi mwingine, lakini anajikuta anainyima nafsi yake uhuru kwa shinikizo la kutendwa na mpenzi wake aliyeachana naye miaka kadhaa iliyopita. 

Hivyo kama umeweza kusonga mbele kwa kuachana na mambo fulani yaliyowahi kuumiza moyo wako unayo sababu ya kujipongeza sana kwakuwa umeweza kupiga hatua kubwa ambayo imekuepusha na madhara mengi yakiwemo ya msongo wa mawazo na magonjwa mbalimbali.

8. Kama unajiheshimu na kuheshimu wengine.

Ni jambo baya sana kumdharau mwingine kutokana na shinikizo lolote kama vile umasikini, ipo kanuni rahisi sana ya maisha “usimtendee mwingine jambo ambalo usingependa utendewe pia” Kama unajiheshimu na kuheshimu wengine hakika utaheshimika pia. Hivyo kama wewe ni mmoja wa watu wanao penda kutenda haki, unayo sababu ya kujipongeza.

9. Kama hauna majivuno na ubinafsi.

Kama ilivyokuwa katika sababu iliyopita, tabia ingine unayotakiwa kuiondoa ni majivuno na ubinafsi mbele ya wengine. Kama wewe ni mtu usiyependa kujivuna na kuukumbatia ubinafsi juu ya wengine, unakila sababu ya kujipongeza.



10. Kama unaishi kwa imani.

Ingawa kuishi maisha bila hofu ni jambo gumu, unapaswa kutambua kuwa hofu inaweza kurudisha nyuma maendeleo yako mara million kuliko kitu kingine. Hivyo ishi kwa imani , usimpe hofu na mashaka maisha yako.

11. Kama ni mtu wa Maendeleo.

Muda utakajisemea kuwa umeridhika na kiwango cha maendeleo yako kimaisha, maisha yako yataporomoka , endelea kusonga mbele kila siku bila kujali kiwango cha maisha yako.

Kumbuka “ mwenye mali atazidi kuongezewa, bali asiyekuwa na mali, hata kile kidogo alichonacho atanyang’anywa”

12. Kama unajipenda na kuwapenda wengine.

Kuna usemi usemao “Upendo huanzia nyumbani mwako” Usemi huu una maana gani? Kama huwezi kujipenda mwenyewe utawezaje kumpenda mwingine, taswira gani ya upendo utawaonyesha wengine? Ni vipi unaweza kutoa kitu usichokuwa nacho? Majibu ya maswali hayo yatakupa kipimo halisi cha hali ya upendo wako