MelK Premium Suits

TANGAZO MUHIMU

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

BISHOP DR. M.E. ADMIN

BISHOP DR. M.E. ADMIN

SANDLANDS HOTEL KARIAKOO

SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO


SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO

NA: MWALIMU KELVIN KITASO

Suala la malezi ya mtoto katika wakati huu limekuwa ni suala lenye changamoto kubwa sana kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia na pia mwingiliano wa watu wa jamii mbalimbali kutoka katika mataifa mbalimbali ya pande zote za dunia (utandawazi). Na mtazamo huo wa malezi umekuwa na muingiliano mkubwa sana na maandiko Matakatifu katika makuzi ya mtoto kwa kupanga yale yaliyonenwa katika maandiko, hii ni mbinu ya shetani kutaka kuchafua kizazi ili kiwe nje ya kusudi la Mungu katika kumlea mtoto. Shetani hujitahidi sana kutumia watu wakubwa katika dunia hii kuleta mawazo yanayopingana na Biblia akijua kwa kufanya hivyo ataweza kujipatia wafuasi wengi kwa kufanikiwa kukiharibu kizazi.

“Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee”. Mithali 22:6. Maandiko Matakatifu yanasisitiza juu ya kumlea mtoto katika njia impasayo kwa kuwa hataiacha hata atakapofikia uzee wake, na pia ukimlea mtoto katika njia isiyompasayo hatoiacha pia hata atakapokuwa katika uzee wake.

Kumlea mtoto ni suala ambalo Mungu ameweka kwa mzazi na hakuishia tu kuliweka mbele ya mzazi bali alitoa namna gani mtoto huyo anapaswa kulelewa. Dr. Mayles Munroe anasema, “marejeo mengi uweka wazi kuwa watoto hujifunza kila kitu wanachotaka kufunzwa katika miaka saba (7) na kushuka chini. Baada ya miaka saba (7) hujifunza yale tu wanayotaka kujifunza; kwa maana nyingine, kama haujamfundisha mtoto katika njia impasayo katika miaka saba (7) ya kwanza na kama haujamuambukiza tabia yako, mwenendo wako na mambo yako katika wakati huo ni vigumu sana hata neema ya Kristo isaidie baada ya miaka hiyo. Lakini kama umefanikiwa kumuonyesha njia impasayo katika umri huo wa miaka 7, hakika wataweza kuifuata njia hiyo katika siku zote za maisha yake. Wanaweza kujaribu tabia nyingine kama wanavyofanya watu wengine lakini mwisho wake watakumbuka yale mafundisho waliyowahi kuyapata na kurudi tena.”

Ukweli ni kwamba mtoto katika umri wa miaka 12 na kuendelea si rahisi sana kuiga kila kitu kutoka kwa wazazi na mara nyingi upenda kujaribu kufanya yale ambayo wanaona wengine wanafanya na hata yale wakatwazayo kwa kuambiwa kuwa ni mabaya, wao upenda kuyajaribu ili wajihakikishie wao wenyewe kuwa yana ubaya au hayana. Katika umri wa miaka hii na kuendelea mtoto uenenda kutokana na vile alivyokuzwa akiwa chini ya umri huo na yale mafundisho aliyoyapata umsaidia kwenda vizuri. Ndio tafsiri ya msemo usemao ‘mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’.

Wazazi wengi wapo katika majuto makubwa ya tabia za watoto wao, ila ukiangalia chimbuko ni msingi waliowawekea wao wenyewe toka wakiwa wadogo. Msingi ulio imara ujengwa katika neno la Mungu. Mzazi ni lazima awe na juhudi kubwa ya kumlisha mtoto wake neno la Mungu tangu akiwa mdogo, angali katika tumbo la mama yake kwa kumtamkia maneno ya Mungu na yaliyo ya ushindi, neno li hai na tena lina nguvu kubwa, halipingwi na mipaka ya mfuko wa mama alipo mtoto katika tumbo, lenyewe upenya na kwenda kuumba yale maneno yaliyotamkwa kwa imani. Azaliwapo na aendeleapo kukua hakikisha unafanya juhudi kubwa ya kumlisha neno la Mungu likae kwa wingi ndani yake, naye ajue kulisema na kulishika kwa uzuri kwa kuwa hataliacha hata atakapokuwa mzee na ni lazima lizae matunda mema kwake ambayo utayafurahia.

Msidanganyike wazazi, ni neno la Mungu tu, ndilo uweza mfanya mwanao awe salama na kuokoka na dunia hii iliyojaa na uovu wa kila namna. Dunia ipo kwenye hali mbaya sana na inawimbi baya sana liwezalo kumpoteza mtoto wako hata kama amezaliwa katika familia ya ukristo wa viwango vikubwa sana; ukiwekeza kumfundisha neno ni lazima awe mtu wa tofauti sana na utamfurhia kwa mwenendo mwema wa kufurahisha.

“Moyoni mwangu nimeliweka neno lako nisije, nikakutenda dhambi,” Daudi anazungumza ni kwa nini ushindwa kumtenda Mungu dhambi, ni kwa sababu ya lile neno ambalo lipo ndani yake umkumbusha mara zote nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwake. Neno likikaa kwa watoto ndani yao vyema hawatamtenda Mungu dhambi na pia litawasaidia kuwa na nidhamu bora katika jamii.

Ibilisi amekuwa na udanganyifu mkubwa sana hata ndani ya watumishi wa Mungu kwa kutia ushawishi kuwa mtoto uwa haokoki ila wanaookoka ni wazazi tu na mtoto anaokoka akisha kuwa mtu mzima, huu ni udanganyifu mkubwa uliofungwa ndani ya walio wengi sana kwa kuwa maandiko uonyesha habari za Timotheo alianza kumcha Mungu tangu akiwa mtoto mdogo, Daud, Yusufu, Isaka, Yeremia, Samweli na Yesu walianza kumcha na kumtumikia Mungu tangu wangali wadogo kwa kuwa neno la Mungu liliwafikia tangu walipokuwa wadogo. Udanganyifu huu unasababisha watu wajitie moyo kuwa wakikuwa na kujitambua na wao wataookoka, si kweli kwa kuwa wanahitaji neno mapema kabla mambo hayajaanza kuharibika.

Waswahili wanasema “samaki mkunje angali mbichi.,” kwa kumaanisha kuwa hata mtoto uweza rekebishwa na kutengenezwa tabia akiwa katika umri mdogo bado kwa kuwa hakishakuwa mkubwa ni vigumu sana kumrekebisha mtoto kama huyo. Mtoto ni kama samaki mbichi makuzi na maisha yake ya baadae utegemea ni kwa namna gani unamfanya kabla hajakua/kauka.

Watoto hawawezi kujikuza wao wenyewe na ndiyo maana wazazi na walezi wapo ili kuwakuza. Kwa mtoto kuwa vizuri katika maeneo yote ya maisha ni matokeo ya mafunzo anayopata kutoka kwa wazazi na walezi. Zipo shule na taasisi mbali mbali zenye kuwafunza watoto na nyingine uwasajiri toka wakiwa wadogo sana na kuanza kuwalea, ila mlezi mkuu na mwenye dhamana kuu ya kulea ni wazazi wa mtoto, na ni vigumu kuona mtoto yupo kama utakavyo wewe kama ukumlea wewe. 

Mtoto yeyote yule akuzwaye katika makuzi mazuri, ukua kwa kumpendeza Mungu na wanadamu na uwa furaha pia kwa wazazi wamkuzao mtoto huyo, kwa maana mtoto mpumbavu ni mzigo kwa mamaye ila mwana mwenye hekima ni utukufu kwa wazazi wake.

Dunia inalia na haina majibu juu ya kumlea mtoto katika njia impasayo na wasomi na watafiti wengi wamefanya utafiti na kugundua kuwa makelele, fimbo ya adhabu na ukali mwingi kwa mtoto si njia njema ya kumkuza mtoto, wakati ulimwengu unayo maswali mengi yupo Mungu ambaye kwake hakuna lisilowezekana na kwake malezi bora inawezekana lakini pia vitu hivyo havitoshi hususani fimbo ya adhabu pasipo kujumuishwa na neno la Mungu ambalo ni sababu kubwa ya mabadiliko kwa mtoto.

Ni ukweli kabisa kuwa wapo wazazi wengi sana ambao wametumia muda wao mwingi kupiga makelele kwa watoto wao kuhusu tabia mbaya na wengine wamekuwa wakali sana na uogopwa kila wakati wafikapo mbele za watoto wao, na utumia fimbo kila wakoseapo watoto wao, ila kwa jitihada zote hizo bado juhudi zao zinagonga mwamba kwa kutokuwa na matunda mazuri ya kuwakuza watoto hao, hii ni kwa sababu ukali, fimbo na makelele mengi havitoshi kumfanya mtoto abadilike, ila kutumia fimbo pamoja na kumfunza neno la Mungu na likakaa vizuri ndani umfanya mtoto kuwa na hofu ya Mungu ambayo itamzuia kujishughulisha katika uovu ajishughulishao.

Somo hili linatoa majibu ya namna gani mtoto anapaswa kukuzwa katika BWANA, na ni kwa namna gani mzazi anaweza mtengeneza mtoto kuwa katika misingi iliyo myema na ya kupendeza kwa kufuata misingi ya biblia.