RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

TOZO WODI YA WAZAZI ZAIPONZA MUHIMBILI

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu.

SIKU moja baada ya gazeti la Nipashe kufichua namna kina mama wanavyotozwa wastani wa Sh. 300,000 kwa ajili ya huduma ya uzazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Ummy Mwalimu, ameitaka bodi ya hospitali hiyo kueleza sababu za kuwalipisha kinyume na sera ya taifa ya afya.

Jana katika toleo la Nipashe lilichapisha habari iliyokuwa ikieleza namna wanawake wajawazito wanavyotozwa fedha kwa ajili ya kujifungua.

Akizungumza na Nipashe jana kwa njia ya simu, Mwalimu alisema baada ya kusikia taarifa hiyo, ameutafuta uongozi wa bodi ya hospitali hiyo kwa ajili ya kutaka maelezo na sababu za kutoza fedha hizo.

Alisema utaratibu unaotumiwa na hospitali hiyo ni kinyume cha Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 inayosisitiza kuwa kina mama wajawazito ni lazima wapate huduma hizo bure.

Mwalimu alisema suala hilo wamekuwa wakilisisitiza kila mara na wataendelea kulisisitiza, ili kila hospitali ya umma itoe huduma bure kwa wanawake walio kundi la msamaha.

“Nimeongea na Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, nimemweleza nataka kupata taarifa ya sababu za kutoza wanawake fedha kwa ajili ya kujifungua kinyume cha sera ya afya ya uzazi ya mwaka 2007 na mwenyewe ameniahidi atakaa na uongozi wa hospitali ili kunipa taarifa hiyo,” alisema Mwalimu.

“Bodi imeniahidi itakaa na uongozi wa hospitali ili kujadili kwa pamoja na kunipatia majibu ya hoja hii mara moja.”

Alipoulizwa kama serikali imepeleka fedha za kutosha katika hospitali za serikali ili kusaidia utoaji wa huduma hizo bure, Waziri Mwalimu alisema wanapeleka fedha kwa ajili ya huduma.

Alisema mishahara ya wauguzi na madaktari inatoka serikalini kwa ajili ya kutoa huduma za matibabu kwa makundi hayo maalumu.
“Kabla hujamalizia swali lako, naomba nikueleze kuwa madaktari tunawalipa mishahara kwa fedha za serikali na dawa zinanunuliwa na kusambazwa katika hospitali za serikali,” alisema.

“Lakini pia serikali inahakikisha dawa zinapatikana katika hospitali zote za serikali inakuwaje sasa hospitali inawatoza wanawake hizo fedha?”

Pia alieleza serikali inapeleka fedha za kutoa huduma na uendeshaji wa hospitali za umma ili madaktari wawahudumie wananchi.
Alisema gharama wanazotozwa wagonjwa wa kundi la msamaha zinakuwa hazina tofauti sana na zile za hospitali binafsi hali ambayo inampa wasiwasi.

“Kama wanatoza fedha hizo kwa ajili ya kutoa huduma kwa makundi maalumu na siyo kwa wagonjwa wa private, inamaana fedha wanazopata ni nyingi ingawa wamejitetea ni kwa ajili ya kuboresha huduma katika hospitali hiyo.”

KUCHANGIA HUDUMA
Wakati wanawake waliojifungua katika hospitali hiyo wakilalamikia kutozwa wastani wa Sh. 300,000, juzi Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa wateja wa Muhimbili, Aminieli Aligaesha alithibitisha wanawake wanaokwenda kujifungua hospitalini hapo wanatozwa fedha hizo kwa ajili ya kuchangia huduma.

Kiasi alichokitaja ni Sh. 125,000 kwa wanawake wanaojifungua kawaida na Sh. 250,000 kwa wanawake wanaojifungua kwa upasuaji.

Aidha, Aligaesha alisema hospitali hiyo inatoza kundi hilo lililo nje ya malipo kwa kuwa haina fedha za kutosha kutoa huduma. Alisema hawajapokea fedha kutoka serikalini kwa miezi tisa.

Wakati serikali ikiendelea na kampeni yake ya kutoa huduma ya afya bure kwa ajili ya makundi maalumu ya msamaha wakiwa kina mama wajawazito, wazee, watoto chini ya miaka mitano na watu wenye maambukizi ya Ukimwi, mwaka wa fedha wa 2016/17 serikali imetenga Sh. bilioni 251 kwa ajili ya sekta hiyo.

Kufikia robo ya mwaka wa fedha katika utekelezaji wake, zimeshatolewa Sh. bilioni 20 pekee badala ya bilioni 62.5 katika kipindi hicho iwapo fedha hizo zingetolewa kwa uwiano sawa wa vipindi vinne vya mwaka.

Hata hivyo utaratibu wa utoaji fedha si lazima kufuata mgawanyo sawa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Fedha na Mipango, serikali inatoa Sh. bilioni 68 kila mwaka kwa ajili ya mishahara ya watumishi 3,121 wa Hospitali ya Muhimbili yenye makusanyo ya Sh. bilioni 4 kwa mwezi.

Mishahara hiyo inagawanywa kwa madaktari bingwa 238, madaktari wa kawaida 173 na wauguzi 1,699.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) wastani wa kipato cha Mtanzania ni Sh. milioni 1.9 kwa mwaka sawa na kila mwezi Sh. 159,910.

Gharama hizo hazilingani au kuendana na gharama za huduma ya uzazi wanazotozwa kina mama wanaopata huduma ya kujifungua katika Hospitali ya Muhimbili.