RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

JAJI MTUNGI AVIFUTIA USAJILI VYAMA VITATU VYA SIASA NCHINI


Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mtungi leo amevifutia usajili wa kudumu vyama vitatu vya siasa kwa makosa mbalimbali. 

Vyama hivyo vilivyofutwa ni pamoja na Chama cha Haki na Ustawi wa Jamii (CHAUSTA) kinachoongozwa na James Mapalala, Chama cha The African Progressive Party of Tanzania (APPT Maendeleo) kinachoongozwa na Peter Kuga Mziray na Chama cha Jahazi Asilia kilichokuwa kinaongozwa na Kassim Bakari Ally.

Akiongea na wanahabari leo, Jaji Mtungi amesema amevifuta vyama hivyo kwa kutumia kifungu cha 19 cha sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992. 

Jaji Mtungi ameongeza kuwa, mchakato wa kufuta usajili wa vyama hivyo unatokana na zoezi la uhakiki wa utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya sheria ya vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu lililofanyika kuanzia Juni 26 hadi Julai 2016.

Katika zoezi hilo la uhakiki ilibainika kuwa vyama tajwa hapo juu vimepoteza sifa za usajili wa kudumu kwa kukiuka masharti ya sheria ya vyama vya siasa na walipewa taarifa.

Zifuatazo ni sababu za kufutwa vyama hivyo; 

Kutokuwa na ofisi ya chama Tanzania Bara na Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 10 d, kutokuwa na wanachama Zanzibar kifungu cha 10 b, kushindwa kuweka kumbukumbu za mapato na matumizi ya chama kifungu cha 14 ( 1) a, kushindwa kuwasilisha hesabu zake na matumizi ya mwaka kwa mthibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mujibu wa vikifungu 14 (1) b (1), kushindwa kuwasilisha tamko la orodha kwa msajili wa vyama vya siasa mali za chama na mwisho kushindwa kutekeleza matakwa ya kifungu cha 15 (1) kwamba mapato yote ya fedha ya chama yawekwe katika akaunti ya chama.