RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NANASI:KINGA DHIDI YA MAGONJWA YA UVIMBE


Mwili unapokosa kinga imara, huwa katika hatari ya kushambuliwa na kila aina ya magonjwa. Katika orodha hiyo ya magonjwa, yamo pia yale ya kutokwa na uvimbe yakiwemo majipu. Kitaalamu magonjwa haya yanajulikana kama ‘Inflamatory diseases’.

Katika kukabiliana na matatizo kama hayo, nanasi ni moja kati ya matunda yenye vitamin nyingi na virutubisho vingine vyenye uwezo wa kuupa kinga mwili wako dhidi ya magonjwa hayo na mengine.

Siri na umuhimu wa nanasi upo kwenye kirutubisho aina ya ‘Bromelain’ ambacho kinapatikana kwa wingi kwenye tunda hili. Virutubisho hivi hulifanya tunda hili kuwa muhimu sana katika kujenga na kuimarisha kinga ya mwili.

Ukilipa umuhimu na ukiliweka nanasi katika orodha ya matunda unayokula mara kwa mara, utajiepusha na utajipa kinga dhidi ya magonjwa mengi hususan ugonjwa wa kuwashwa na kuvimba koo, ugonjwa wa baridi yabisi (Arthritis) na ugonjwa wa gauti (Gout).

Ili upate kinga dhidi ya maradhi hayo kwa kula nanasi, unashauriwa kula tunda hilo kabla au baada ya kula mlo wako. Usile nanasi pamoja na chakula kingine kwa wakati mmoja. Kwa kufanya hivyo, virutubisho vitafanya kazi nyingine tofauti na uliyokusudia. Faida nyingine za nanasi ni kama ifuatavyo;

USAGAJI WA CHAKULA
Nanasi lina virutubisho vinavyouwezesha mfumo wa usagaji chakula tumboni kufanya kazi yake ipasavyo. Pindi mfumo huu unapowezeshwa kufanya kazi yake vizuri, mtu huweza kupata choo laini na kwa wakati kama inavyotakiwa.

KINGA YA MWILI
Nanasi linaaminika pia kuwa miongoni mwa matunda yenye Vitamin C kwa wingi ambayo kazi yake ni kuupa mwili kinga dhidi ya ‘wavamizi’ mbalimbali (free radicals), ambao wanapoingia mwilini, kazi yao huwa ni kuharibu chembembe hai za mwili.

Kwa kuongezea, Vitamin C inaaminika kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha mfumo wa kinga ya mwili. Mwili huwa na uwezo wa kujikinga dhidi ya magonjwa madogo madogo kama vile mafua, kikohozi, homa na maambukizi mengine. 

CHANZO CHA MADINI
Mbali ya kuwa ni chanzo kizuri cha vitamin C, nanasi pia ni chanzo kizuri cha madini aina ya ‘Manganese’ ambayo yanaaminika kuwa na uwezo wa kuboresha ufanisi wa vimeng’enyo mbalimbali vya mwili, vikiwemo vya kuzalisha nishati na kinga. Hali kadhalika tunda hili lina kiwango cha kutosha cha Vitamin B1 (Thiamine).

KUIMARISHA NURU YA MACHO
Inawezekana karoti ikawa ndiyo inayojulikana na watu wengi kuwa na uwezo wa kuimarisha nuru ya macho lakini nanasi nalo lina uwezo mkubwa wa kuimarisha nuru ya macho. Utafiti unaonesha kuwa ulaji wa tunda hili na matunda mengine, kiasi cha milo mitatu kwa siku, kunaondoa hatari ya kupungua kwa nuru ya macho kwa asilimia 36 kwa watu wazima.

NANASI BORA
Nanasi bora ni lile kubwa na lililoiva vizuri. Ni kweli kwamba nanasi kubwa lina nyama nyingi kuliko nanasi dogo lakini hakuna tofauti ya ubora wa virutubisho kati ya nanasi dogo na kubwa, ili mradi lisiwe limeoza au lenye michubuko mingi. Chagua nanasi lilioiva vizuri na lenye kunukia.

Mara baada ya nanasi kumenywa na kukatwa vipande, linatakiwa kuliwa mara moja, iwapo litahifadhiwa kwenye jokofu kwa ajili ya kuliwa baadaye, njia sahihi ya kuhifadhi ni kuliweka kwenye chombo chenye mfuniko (container). Hii husaidia kuhifadhi virutubisho vyake kwa kipindi cha hadi siku tano bila kupoteza ubora wake, ikiwa pamoja na ladha. Unaweza kula vipande vya nanasi au juisi yake, vyote vina faida.