RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NGUVU NA AKILI, MITAJI YA BURE KWA KILA BINADAMU. .

Watu wengi sana wamekuwa wakilalamika kuwa wanapotaka kuanzisha biashara zao au miradi yao mbalimbali ya kimaendeleo kuwa moja kati ya tatizo wanalokabiliana nalo ni mtaji, mtaji wa aina gani ukiwauliza watakuambia pesa, kila mtu anaamini katika mtaji pesa. Lakini jambo la kusikitisha ni kuwa pesa haipatikani kwa kila mtu kama atakavyo. Lakini ukifikiri na kupembua kwa undani utagundua kuwa tuna mitaji miwili ya bure ambayo kila mtu amepewa na muumba.


Mungu alipomuumba mwanadamu hakumwacha hivi hivi bali alimpatia kitu kimoja muhimu na adimu bila kujari mwanadamu huyu ataishi sehemu gani, iwe ulaya, marekani au afrika. Kitu hiki ni akili, kila mwanadamu amepewa akili na mungu, lakini jambo linalokuja kutofautisha akili ya mtu mmoja na mwingine ni matumizi ya akili yake haswa katika kutatua changamoto zinazomkabili. Kila mtu amekuwa na namna yake ya kipekee ya kutumia akili yake katika kutatua changamoto, lakini jambo baya zaidi ni kuwa wengi wetu hatutumii ipasavyo akili zetu katika kutatua changamoto zetu, ,mara nyingi sana tumekuwa ni watu wa kulaumu laumu tu na kusingizia. Kulaumu na kusingizia sio matumizi sahihi ya akili yako.


Ikiwa hauishughulishi akili yako vyema katika kutatua changamoto zako basi wewe miaka nenda miaka rudi utabaki kulaumu kuwa tatizo lako ni mtaji ambao ni pesa. Jambo la muhimu na la kujiuliza siku zote ni kuwa umeitumia vipi akili yako katika kuhakikisha kuwa unajipatia pesa ambayo ndio unaamini kuwa ni mtaji, na kama hujaishughulisha akili ipasavyo unalaumu nini?, unafikiri pesa zinaanguka kwenye mti?. Mimi ninaamini kuwa hata kama huna pesa kama mtaji, ukiishughulisha akili yako ipasavyo unaweza kupata pesa na kuwa na uwezo wa kuzitumia vyema maana umeiandaa akili yako katika kupata pesa. Tumia akili yako vyema katika kukabiliana na changamoto zinazokukabili maana akili ni moja kati ya mtaji wa bure.


Nguvu, huu ni mtaji wa pili wa bure kwa mwanadamu toka kwa mungu, ndio maana baada ya adamu kushawishiwa na hawa mungu alimwambia adamu “utakula kwa jasho”, hii inamana kuwa utakula kwa kutumia nguvu zako mwenyewe na wala sio za mwingine. Na kwanini aseme utakula kwa jasho ni kwa kuwa anaamini kuwa una nguvu alizokupa yeye mwenyewe. Swali la kujiuliza ni kuwa unatumia vipi nguvu zako katika kujiletea maendeleo unayoyataka.


Mungu alituumba na kutupa nguvu lakini jambo la kusikitisha ni kuwa wengi wetu hatutumii nguvu hizi katika shughuli za kimaendeleo na kama tukizitumia basi ni kwa kulazimishwa sana. Vijana wengi sana leo hii ni wavivu sana na tena ukikuta kasoma hata ana kadigrii basi anaona yeye kufanya kazi yenye kutumia nguvu ni kujishushia hadhi., wanataka kazi nyepesi ambazo watatumia nguvu kidogo maana ni wavivu ila wanazugia elimu zao. Swali la msingi na la muhimu nalo taka ujiulize unazitumiaje nguvu zako katika kujiletea mafanikio?


Nimekutajia na kukuonesha mitaji miwili ya bure toka kwa muumba, kazi kwako kujiuliza unatumia vipi akili yako ili kujiletea mafanikio, unatumia vipi nguvu zako katika kujiletea mafanikio?. Kama huelewi unachofanya na nguvu zako au akili yako basi jua una matatizo makubwa. Kaa chini jihoji vya kutosha na majibu utakayoyapata yafanyie kazi mara moja.