RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NJIA ZA KUFIKIA MALENGO KATIKA MAISHA



KATIKA sayansi ya mafanikio kuna mambo mengi sana yanahusika kutufikisha pale tunapopataka. Pia kuna njia tofauti zinazopendekezwa na wataalamu wa masuala ya saikolojia. Mfano mwanafilosofia wa Ugiriki, Aristotle anasema: “Binadamu ni kiumbe wa malengo.” Pia kuna watu wanaweza wakahoji kwa nini tuwe na malengo katika maisha yetu ya kila siku. Zifuatazo ni sababu chache tu za kwanini tuwe na malengo. Kwa sababu mafanikio ni malengo na vingine vinafuata kwa hiyo kama unataka mafanikio ya kweli inabidi uwe na malengo, bila malengo unakuwa ni sawa na kisiwa chenye utajiri mwingi, lakini bado hakijavumbuliwa, kwa hiyo jitahidi uwe na malengo ikiwa ndiyo njia ya kufanikiwa. Malengo ni kama mafuta katika safari ya kufanikiwa, umuhimu wa malengo unafananishwa na mafuta katika gari kwani bila mafuta haiwezi kwenda, ni sawa na malengo katika kazi hata kama una bidii sana kufanya kazi bila malengo itakuwa vigumu kupima utendaji wako mwenyewe wa kazi wa kila siku. Malengo yanakusaidia kufikiria kile unachotaka, na kuwa na uwezo wa kufikiria kile unachokitaka inakusaidia kuwa na nguvu ya ziada kuelekea kupata yale unayoyataka katika maisha, ili uweze kufanikiwa ni lazima uwe na maono ya kule unakoelekea. Malengo yanakupa uwajibikaji kwa sababu mtu unakuwa unajua nini unachokitaka au umepanga kufanikiwa nini kwenye sehemu yako ya kazi. 


Malengo pia yanakusaidia kutumia muda vizuri ambao ni kitu muhimu katika maisha, ukishindwa kutunza muda huwezi kufanikiwa. Lakini vitu vya msingi ni kujifunza kwa mbinu tofauti ili tuweze kufikia malengo. Kwa mfano mwandishi mmoja anaitwa Brian Tracy, anaelezea umuhimu wa malengo katika kitabu chake kinachoitwa Goals. Anasema malengo ndio kitu pekee kinachosababisha mafanikio na jinsi ya kuwa na mtazamo wa mbele kuelekea kile unachokitaka. Kuna sababu nyingi sana za kwanini watu hawaweki malengo katika maisha licha ya kuwa njia majawapo ya kufikia mafanikio. Zifuatazo ni baadhi ya sabababu za kwanini watu hawaweki malengo. Kuogopa kukataliwa kama kitu unachopanga kufanya watu watakikataa, hivyo utajikuta unakata tamaa na kuhisi kukataliwa kihisia. Hiyo inasababisha kuogopa kuweka malengo, hasa pale unapohisi utashindwa kuyafanikisha, kwa ushauri tu jiamini, jipange na usije ukamwambia mtu yeyote malengo na anza kuyatekeleza acha waone matokeo ya kile unachokifanya. Hofu ya kushindwa Kushindwa kitu chochote kunaumiza na kunakatisha tamaa na msongo wa mawazo. Lakini inabidi ujifunze kukabiliana navyo kwa sababu unapoanza kitu chochote kipya ujue kuna changamoto zake. Hapa namaanisha kwamba usije ukadhani unavyoanzisha kitu kipya utakutana na urahisi, hapana kushindwa ni sehemu ya kujifunza. Kutojua jinsi ya kuweka malengo Watu wengi hawajui jinsi ya kuweka malengo wanafananisha malengo na matarajio. Kwa mfano kuwa na familia yenye furaha na pesa nyingi hivi kila mtu anavyo, malengo ni yale yaliyoandikwa kiufasaha na yanaeleweka pia yakiwa na muda. Pia watu wengi hawajui umuhimu wa kuweka malengo katika maisha, pia familia nyingi hazina utamaduni wa kuwa na malengo, sasa basi jiwekee utaratibu wa kuwa na malengo. Malengo hayana umuhimu Kama unaishi na watu ambao hawana malengo au familia ambayo hawazungumzii umuhimu wa malengo ni kweli utafika umri wa utu uzima bila kujua umuhimu wa kuweka malengo. Ukiwa hujaweka malengo yoyote katika maisha ni bure. Wengi tuna matarajio mengi bila ya kuwa na malengo. Mara nyingi watu ambao hawana malengo ni wale ambao hawana furaha katika kazi na ndoa zao, kwa sababu siri ya kupata furaha ya kweli ni kuwa na mipango inayokuletea mafanikio. Kabla hutujaangalia ni kwa namna gani ambavyo mtu unaweza kuweka malengo, lazima tuelewe malengo ni nini hasa na yana sifa zipi. Malengo lazima yaandikwe vizuri tena katika lugha nyepesi, pale unapoyaandika yanakuwa yanajiandika kwenye moyo wako na kusababisha uyakumbuka kila siku. Malengo yawe rahisi kueleweka. Ina maana kwamba malengo ili iwe rahisi kufikiwa ni lazima yawe rahisi kuelezea na ili lengo liweze kufanikiwa ni lazima liwe na wazo moja la msingi likiwa ndilo wazo kuu na la msingi katika lengo lako. Kwa mfano ukiandika unataka kufanikiwa, ukaishia hapo bila kueleza kwenye nyanja ipi, lazima uandike iwe ya kifedha au vinginevyo. Malengo lazima yawe yamejieleza vya kutosha, mfano unataka kuongeza kipato kwa kiasi gani kama ni 350,000 kwa mwezi lazima uandike unataka kuongeza kipato kwa kiasi gani katika lengo lako kuu, usipoweka kiasi mwisho wa siku utashindwa kujipima kama kweli umefikia lengo au la. Na kisha ainisha ni kwa kiasi gani, itakusaidia kuweka mikakati ya jinsi ya kufikia pale unapopataka. Baada ya kuangalia jinsi malengo yanaweza kuandikwa, tuangalie ni jinsi gani tunaweza kuweka malengo. Angalia au chunguza tatizo ambalo linakuzuia kushindwa kufika pale unapopataka na unawajibika kwa kiasi gani katika kutatua hilo tatizo, kikwazo au changamoto inayokukabili. Ukishajua tatizo linalokufanya uwe hapo ulipo na sio pale unapopataka itakusaidia kuwa na mikakati na malengo ya jinsi utavyotatua tatizo au jinsi ya kukabili changamoto ambayo unayo katika kufikia lengo. 


Jione wewe mwenyewe kama ndio rais au mmiliki wa maisha yako mwenyewe, hakuna yeyote anayehusika na kubadilisha hali ambayo unayo katika maisha yako. Acha kulaumu mtu yeyote kwa makosa yaliyojitokeza au matatizo, cha kufanya ni kuchukua jukumu la kutatua tatizo kuliko kulalamika. Kulalamika hakutatui tatizo ila kunakupunguzia uwezo wa kufikiria na kutatua matatizo. Hivyo basi, chukua hatua matatizo yanapojitokeza ili kujijengea uwezo wa kiutendaji na uwajibikaji. Punguza sababu pale unapokosea, zaidi jikite katika kutatua tatizo, utajijengea misingi imara ya kuwa na malengo katika kazi zako za kila siku na utakuwa na mchango chanya katika eneo lako la kazi. Ukiwa unatoa sababu sana huwezi kuwa mtendaji mzuri na pia utakosa mipango kwa sababu kila kitu unajitetea baada ya kuvaa uwajibikaji wa jinsi ya kutatua tatizo. Jione wewe ndio chachu ya mabadiliko katika maisha yako mwenyewe, kwa sababu uko hapo ulipo kwa sababu ya uamuzi uliofanya na mipango uliyoifanikisha na pia upo hapo kwa uamuzi na mipango uliyoshindwa kuifikia. Hivyo, weka mipango ya jinsi unavyotaka kuwa na kufanikiwa katika nyanja ipi. Kwa kuanzia sasa chukua uamuzi wa kumsamehe mtu yeyote aliyekukosea, msamehe na usijadili tena mambo yaliyopita na weka malengo ya nini unataka kufikia katika maisha yako. Kwa mfano, kama umepunguzwa kazi usimlaumu bosi wako, kama umeonewa jipange upya na anza kutafuta njia nyingine ya kuishi au kupata kazi, usipende kujadili watu wanaokufanyia fitina za kukurudisha nyuma, cha msingi weka mikakati ya kufikia malengo.