RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SABABU TATU (3) ZA KUFA KWA BIASHARA NYINGI


Sababu ya kuanzisha biashara yeyote ile ni kuifanya biashara hiyo ikue kadri siku zinavyozidi kwenda na si kufeli. Mitazamo hasi ambayo imekaa katika halmashauri zetu za ubongo ndizo zinazotufanya biashara zetu kuanza kusua sua na hatimaye kufa kabisa. 


Wapo baadhi ya wafanyabiashara ambao pindi biashara zao zinavyokwenda kombo, wao huamini ya kwamba wamelogwa na sababu nyinginezo nyingi kama hizo. Hivi hujawahi kukutana na mfanyabiashara ambaye anatamka kauli kama "hapa lazima patakuwa na chuma ulete?”


Au hujawahi kusikia mfanyabiashara pale ambapo biashara haiendi sawa akisema hapa ni lazima patakuwa na mkono wa mtu? Bila shaka nadhani utakuwa umewahi kukutana na aina hii ya watu na kama hujawahi kukutana nao basi huenda ukawa ni wewe mwenyewe. 


Lakini nikwambie mfanyabiashara wa kweli hamini katika nguvu za kishirikiana bali yeye huamini katika uwepo wa Mungu katika kukamilisha mipango na mikakati ambayo mwanadamu ameipanga. Hata hivyo kwa kwa kuwa wewe mtazamo wako ni chanya katika biashara nataka kukupasha mambo ambayo kama utayafanya uwe na uhakika biashara yako itakufa.


Twende sambasamba kwa kuangalia sababu za kufa kwa biashara nyingi:-


1. Tamaa za kuhamisha biashara kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine huku ukiamini kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kukua kibiashara kumbe kinyume chake biashara hiyo inakwenda kufa kabisa. 


Naomba nielewe vizuri juu ya maelezo haya, si kwamba kuhama kibiashara ni kosa, la hasha si kosa, ila litakuwa kosa endapo utashindwa kufanya uchunguzi wa kutosha wa kibiashara katika eneo ambalo unategemea kufanya biashara


Katika kufanya uchunguzi wa eneo ambalo unataka kufanya biashara ni lazima ujiulize baadhi ya maswali ya msingi ambayo nitayaekeza kwa uchache hii ni kutoka kalamu yangu siku ya leo kuwa na wino mchache hivyo nahofia itaisha na nikashindwa kuleta ujumbe wangu kwako.


Naomba nikueleze kwa uchache ni nini ambacho unatakiwa kufanya kabla ya kuhama eneo moja kwenda jingine kibiashara;-


Fanya uchunguzi wa kutosha kuhusu wateja wako wanataka nini haswa? Ukipata majibu kutakusaidia kuweza kukata kiu ya wateja hao na hatimaye kupata fedha.


Chunguza kuhusu washindani ambao wapo katika eneo hilo ambalo unataka kufanya biashara.


Tambua vyazo vyao vya mapato. Kufanya hivi kutakusadia kujua, je ni biashara gani ambayo unataka kufanya ambayo wateja watamudu kununua bidhaa au huduma hiyo.

Hayo ni baadhi ya machache kati ya mengi ambayo ni vyema akajiuliza kabla ya kuamua kuhama kwenda kufanya biashara sehemu nyingine.

2. Kukosa soko la uhakika.

Watu hufanya biashara kwa kutokuzingatia na kujua biashara wataifanya vipi, unakuta mtu analima mazao ya kibiashara lakini baada ya kuvuna ndo anaanza kutafuta wateja. Hili ni suala ambalo litakufanya biashara yako ife tu. Kwahiyo ili kuepukana na adhaa hiyo unatakiwa kuanza kutengeneza mazingira mapema ya kuwatafuta wateja. 

Au ili kuweza kupata soko la uhakika unachotakiwa kufanya ni kusoma alama za nyakati, pale ambapo unaona uhitaji wa bidhaa au huduma ni mkubwa ndipo na wewe unatakiwa kuanza kufanya biashara hiyo.

3. Kuongeza kwa washindani kibiashara.

Watu wengi biashara zao hufa kwa sababu ya kwamba kuna wafanyabiashara wengi ambao wanafanya biashara kama yao. Hivyo kuna baadhi ya wafanya biashara hukata tamaa na kuona hawewezi kushindana na wafanyabiashara hao.

Ila nikwambie ya kwamba kuwepo kwa washindani wengine kusikuumize kichwa na kuanza kufikiria hata kuacha kufanya biashara, bali unatakiwa kuwaza na kufikiri ni jinsi gani unaweza kuwa bora zaidi.

Ubunifu unahitajika ili kuwa bora zaidi. Ongeza thamani katika biashara. Kwa mfano unaweza kuweka hata punguzo fulani, kufanya hivi kutakufanya wateja wasikuhame, pia kufanya hivyo kutafanya ongezeko la wateja kwani wateja tuna kasumba ya kuambiana kuhusu uzuri na ubaya wa mfanyabiashara fulani.