RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

HII KALI: UNAJUA NINI KUHUSU ROSE MUHANDO


Unapowazungumzia wasanii wa nyimbo za injili ambao ni maarufu Afrika Mashariki na kati basi jina la Rose Mhando halitakosekana.

Rose Muhando

Rozi amejizolea umaarufu kutokana na staili yake ya kuimba kwa hisia na ukweli kwamba suala la kutawala jukwaa huwa halimsumbui kabisa.

Hata hivyo, katika siku za karibuni Rozi amekaa kimya huku akiacha maswali kwa mashabiki wa muziki wa Injili ambao wana kiu kubwa ya kupata burudani ya dada huyo.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na dada huyo na haya ndio maongezi yake;


YUKO WAPI
Rozi amesema kwa sasa amehamishia makazi yake mkoani Dodoma anakofanya shughuli zake za hapa na pale ambazo zinamwingizia kipato na wakati mwingine huwa analazimika kuzungukia mikoa iliyokuwa karibu na Dodoma akifanya shughuli binafsi.

“Naishi Dodoma nafanya shughuli zangu ndogondogo ambazo zinaniingizia kipato, shughuli hizo zinanisababishia niwe bize mno,” alisema Rozi.

Kaacha muziki?
Kwa upande wa muziki wa injili, Rozi amesema hajaacha na kuwa hatoweza kuacha kwani uko kwenye damu yake, ila kwa sasa amepumzika kidogo akiwa anajiandaa kwa kutoa vitu vizuri kwa mashabiki wake.

“Sijaacha muziki, bado nafanya muziki na sitoweza kuacha muziki kwani muziki uko kwenye damu. Siku si nyingi nitawapatia vitu vipya mashabiki wangu kwa hiyo wakae mkao wa kula.


Ujumbe kwa mashabiki
Amesema mashabiki wake wawe na subira kwani katika maisha kuna mwingiliano wa mambo mengi hivyo wawe wavumilivu kusubiria vitu vizuri kutoka kwake na ana imani watapenda tu.

Rozi amesema licha ya kuwa bize na mambo yake, ametetereka kiafya. Anasema amekuwa akifanya kazi huku akiwa anaumwa. Ameongeza kuwa cha ajabu, kila anapokwenda hospitali huwa haonekani kama anaumwa nini.

Aidha amesema amekuwa akipitia majaribu mengi sana toka akiwa kimya katika anga la muziki na hii yeye huamua kuzidisha maombi kwani yuko karibu na Mungu na ana imani ana uwezo wa kumponya.

Anasema kuna wakati alikuwa kama mtu aliyechanganyikiwa. Anasema hali hiyo ilitokana na ugonjwa wa kujikuna ambao ulimpata ghafla. Anasema alikuwa akihisi vitu vinamtembea mwilini na akapelekwa hospitali na kukutwa hana ugonjwa wowote hapo ndipo alipochoka.

“Kwa kawaida huwa nasumbuliwa na miguu mara kwa mara, lakini nilipata ugonjwa ambao hadi leo sijajua ulianzia wapi. Nilipata vipele nikawa najikuna yaani vilikuwa vinawasha wakati mwingine nilikuwa naona kama mtu ananichoma sindano, nikaamua kwenda hospitali lakini hawakugundua ugonjwa wowote, nilipewa dawa za maumivu tu yaani hivyo vipele vilikuwa vikikauka vinaacha alama nyeusi na kuharibu mwonekano wa mwili wangu, yaani niliumia sana hadi niliona naweza poteza maisha. Hata hivyo baadae nilipona.”

Kuhusu dawa za kulevya
Kumekuwa na madai Rozi anatumia dawa za kulevya lakini amekanusha na kusema kuwa ni njama za watu kumshusha kimuziki.

“Hizo tuhuma nazisikia sana, ila hazina ukweli wowote, kuna watu wana lengo la kuniharibia katika utendaji wangu wa muziki, ila hawajafanikiwa kwani mimi niko vizuri na nitarejea kwa nguvu zote kwani nilishajua mtu aliyeanzisha hizi habari, alikuwa ananifuatilia toka nilipoanza kupokelewa na mashabiki katika kazi ya uimbaji, ila namwachia Mungu.

Maisha yake
Malkia huyu wa muziki wa injili Afrika Mashariki na kati, Rozi Mhando amezaliwa 1976 katika Kijiji cha Dumila, Wilaya ya Kilosa, Mkoa wa Morogoro. Rozi kabla ya kuwa Mkristo alikuwa Muislam na ni mama wa watoto watatu. Alimpokea Yesu Kristo pale alipokuwa anaumwa na yuko kitandani akiwa na umri wa miaka tisa. Aliugua kwa muda wa miaka mitatu na baadae alipona na kubadili dini na kuwa Mkristo.

Rose Mhando alianza muziki wa injili katika kwaya ya Dodoma St. Mary’s katika Kanisa la Kianglikana la Chimuli.

Januari 31, 2005, Rose Muhando alizawadiwa tuzo ya Mtunzi mzuri wa nyimbo, Mwimbaji Bora na albamu Bora ya Mwaka. Tuzo hizo zilitolewa katika tamasha la Tanzania

Baadhi ya albamu za Rose Muhando ni ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Kitimutimu’, ‘Jipange Sawasawa’ na ‘Utamu wa Yesu’ ambayo hadi sasa inafanya vizuri.

Baadhi ya nyimbo zilizotamba ni pamoja na ’Nibebe’ ‘Mteule Uwe Macho’, ‘Jipange Sawasawa’, ‘Utamua wa Yesu’ ‘Pasipo Maono’, ‘Nyota ya Ajabu’na nyingine nyingi.

Mwanaspoti