RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NJIA 10 ZA KUJIKINGA DHIDI YA VIRUSI VYA ZIKA.



1. Kutumia dawa au mafuta ya kufukuza mbu
Ushauri wa kwanza kabisa ni kuepukana na mbu. Kituo cha Kudhubiti na Kuzuia Maradhi (CDC) nchini Marekani kinapendekeza watu wajipake mafuta yenye kemikali za kufukuza mbu kama vile N, N-diethyl-meta-toluamide (DEET) au picaridin.
Mafuta haya yanafaa kujipakwa mara kwa mara, kwa kufuata maagizo kwenye mikebe, au mtu anapoanza kuumwa na mbu. Mtu anafaa kujipaka baada ya kujipaka mafuta ya kukinga ngozi dhidi ya miali ya jua.
Mafuta mengi ya kufukuza mbu ni salama hata kwa kina mama waja wazito, lakini ni vyema kutafuta ushauri wa daktari kabla ya kuanza kuyatumia.

2. Kuvalia mavazi ya kufunika mwili
Wataalamu pia wanakubaliana kwamba inafaa kuvalia mavazi yanayofunika mwili vyema. Mfano shati au nguo zenye kufunika mikono na pia suruali au long’i ndefu. Mavazi yanafaa kuwa mazito kuzuia mbu kufikia ngozi.
Katika baadhi ya mataifa, mavazi huwekwa dawa maalum aina ya permethrin, ambao hufukuza mbu.
Iwapo utajipaka mafuta ya kufukuza mbu, usijipake na kisha kufunika maeneo uliyojipaka kwa nguo unazovalia.

3. Kuzuia mbu kuingia nyumbani
Ikiwezekana, wataalamu wanawashauri watu walale ndani ya nyumba zilizojengwa vyema na kuwekwa kinga ya kuzuia mbu kuingia.
Usiku, lala chini ya neti zilizotibiwa.
Lakini usitahadhari usiku pekee kwani mbu aina ya Aedes aegypti, wanaoeneza virusi vya Zika, hupenda sana kuuma watu mchana.

4. Chunga mimea inayokua ndani ya nyumba
Ingawa ni muhimu kuzuia mbu kuingia, ni muhimu hata haidi kuzuia mbu kuzaana. Na mbu huhitaji maji.
Watu wanashauriwa kuchunga sana maeneo yenye maji yaliyosimama kwani huko ndiko viluwiluwi wa mbu huwa. Maeneo haya ni pamoja na mikebe, maeneo ya kuwapa mifugo na wanyama wengine lishe, jagi za kuweka maua, vibanda vya kufugia ndege na mimea ya kupandwa ndani ya nyumba.
Ni vyema pia kusafisha mifereji ya maji mara kadha kila wiki, mufunika matangi ya mali na vidimbwi la sivyo kuweka dawa ya krolini (krolini huwafukuza mbu).
Maji ambayo yametulia kwa zaidi ya siku tano yanafaa kutupwa kwa kumwagwa ardhi kavu, kwani viluwiluwi wa mbu watafariki baada ya maji kukauka. Kiasi kidogo tu cha maji kinatosha kwa viluwiluwi hao kukua kwa hivyo, ni vyema kuosha na kukausha vyema maeneo hatari.

5. Kufunika taka
Maeneo ya kutupwa taka mara nyingi huwa na maji na hutumiwa sana na mbu kuzaana.
Ili kuzuia hili, ni vyema kufunika taka, hasa katika mifuko ya plastiki.
Tairi kuukuu na vitu vingine vya ujenzi pia vinafaa kuwekwa vyema, kwani sana huhifadhi maji ambayo yanaweza kutumiwa na viluwiluwi wa mbu.

6. “Kunyunyizia dawa”
Maafisa nchini Brazil, ambako virusi vya Zika vimeenea sana, wanatafakari wazo la kunyunyizia maeneo yaliyoathiriwa na virusi hivyo dawa ya kuua mbu.Hii inachukuliwa kama njia ya dharura kabla ya michezo ya Olimpiki, ambayo itaanza mjini Rio de Janeiro mwezi Agosti.
Hata hivyo, kuna utata kwani njia hii inaweza kuwa na madhara mengine kwenye mazingira na pia kuathiri afya ya wakazi.

7. Kudhibiti mbu
Serikali katika nchi kadha za Amerika Kusini tayari wameanza kampeni ya kuangamiza mbu wanaobeba virusi vya Zika kwa kutumia teknolojia.
Moja ya njia tata zinazopendekezwa ni kueneza mbu waliofanyiwa mabadiliko ya kijeneti ambao hawana uwezo wa kuzaana. Hili litapunguza idadi ya mbu na kuzuia ugonjwa huo kuenea.
Wengine wamejaribu mbinu nyingine, mfano jiji la Itapetim nchini Brazil. Maafisa mjini humo wanatumia samaki kuangamiza mbu huo.
Samaki hao hula mayai ya mbu na hivyo kuzuia kuongezeka kwa idadi ya mbu hao.

8. Vifaa ya kukabili mbu nyumbani
Maafisa wa serikali wanapojaribu kukabiliana na mbu kwa kiwango kikubwa, watu binafsi manyumbani pia wanatumia njia mbalimbali kukabili mbu.
Wanatumia vifaa mbalimbali vya kuwawinga na kuwaua mbu. Mfano ni kutumia kifaa kinachoiga mwili na kutoa hewani ya kaboni dayoksaidi pamoja na joto, ili mbu waingie ndani wakidhani ni binadamu.
Mitambo mingine ya kunyunyiza dawa ya kuua mbu pia inatumiwa, lakini inapingwa na baadhi ya watu kwani inaathiri pia nyuki, vipepeo na wadudu wengine.

9. Kukwepa kusafiri
Wale wanaoishi maeneo ambayo hayajaathirika na virusi hivyo, wanajizuia kusafiri.
CDC imewashauri wanawake waja wazito nchini Marekani kuahirisha ziara zao Amerika Kusini na visiwa vya Caribbean kadiri wawezavyo.
Kituo hicho kimewashauri wanawake wanaopanga kusafiri maeneo hayo kutafuta ushauri wa madaktari kwanza.

Shirika la Afya Duniani (WHO), hata hivyo, halijaunga mkono ushauri huo wa CDC.
“Kwa kutumia ushahidi uliopo, WHO haipendekezi vikwazo vya usafiri au biashara kuhusiana na virusi vya Zika. Lakini kama tahadhari, mataifa mbalimbali yanaweza kutoa mapendekezo mbalimbali ya kiafya na kuhusu usafiri kwa raia wake, kwa kuzingatia utathmini,” WHO imesema.

10. Kuzuia kuenea.
Mtu anapoambukizwa, hatua zaidi zinafaa kuchukuliwa kuzuia kuumwa tena na mbu wiki ya kwanza baada ya kuugua, CDC inasema.
Hii ni kwa sababu virusi vya Zika vinaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mtu mwingine kupitia damu baada ya kuumwa na mbu.
Ingawa hatari ya kuenezwa kwa virusi hivi kupitia kujamiiana haijathibitishwa kisayansi, baadhi wanapendekeza watu watumie mipira ya kondomu hadi wiki mbili baada ya kupona.
Aidha, watu wachukue tahadhari kuepusha kuambukizwa virusi hivyo kupitia mate na majimaji ya mwili.