RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

ECOWAS: HAKUNA MAKUBALIANO YOYOTE YA JAMMEH KUTOSHTAKIW


Yahya Jammeh mwenye vazi jeupe akiondoka mjini Banjul, kulia ni mlinzi wake akiwa analia. 

Viongozi wa nchi za Afrika Magharibi wamesema kuwa, hakuna makubaliano yoyote ya kutoshtakiwa kwa rais Yahya Jammeh yaliyofikiwa mwishoni mwa juma, makubaliano yaliyomshawishi kiongozi huyo kuondoka mwenyewe kwa hiari nchini mwake, amesema waziri wa mambo ya Kigeni wa Senegal.

Jammeh, ambaye anatuhumiwa kwa uvunjifu mkubwa wa haki za binadamu wakati wa utawala wake, aliliongoza taifa la Gambia kwa miaka takriban 22, lakini akakataa kukubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Desemba mosi mwaka jana.

Jammeh aliondoka mjini Banjul siku ya Jumamosi, saa chache kabla ya vikosi vya ukanda wa ECOWAS kuingia mjini Banjul kudhibiti hali ya usalama na kuandaa mazingira ya rais Adama Barrow kurejea.

Kuondoka kwa Yahya Jammeh nchini Gambia kunatoa nafasi sasa kwa rais Barrow kurejea nchini mwake baada ya kuwa amekula kiapo katika ubalozi wa nchi yake nchini Senegal.
Rais wa Gambia, Adama Barrow akionekana kwenye picha akiwa mjini Dakar. Tarehe 20 Januari, 2017REUTERS/Sophia Shadid


Uamuzi wa Jammeh kuondoka nchini mwake, ulizua maswali kuhusu makubaliano yaliyofikiwa kati yake na wakuu wa nchi za ECOWAS katika mazungumzo ya siku mbili mfululizo mwishoni mwa juma, mazungumzo yaliyoongozwa na rais wa Guinea, Alpha Conde na mwenzake wa Mauritania, Mohamed Ould Abdel Aziz.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters, waziri wa mambo ya kigeni wa Senegal, Mankeur Ndiaye, amesema kuwa, wakuu wa nchi za ECOWAS hawakukubaliana chochote kuhusu kutoshtakiwa kwa Jammeh licha ya kufikia makubaliano.

Waziri Mankeur amesema kuwa Jammeh na timu yake walikubali kuondoka baada ya kuahidiwa usalama na kupewa hakikisho chini ya makubaliano yaliyopendekezwa na umoja wa Mataifa, ECOWAS na umoja wa Afrika, makubaliano ambayo hata hivyo hayakutiwa saini na upande wowote.

Waziri huyu amesema haya baada ya kutolewa kwa chapisho la makubaliano ya umoja wa Afrika na umoja wa Mataifa kuhusu mapendekezo ya kufikia suluhu ya amani ya kisiasa nchini Gambia.

Katika hatua nyingine, vikosi vya nchi za ECOWAS tayari vimewasili mjini Banjul, Gambia, ambako vimeenda kwaajili ya kutoa usalama kwa rais Barrow na raia wa Gambia.