RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KUKOSA LA KUFANYA NI MOJA YA CHANZO CHA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA



Kuna sababu nyingi zinazochangia ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya katika jamii. Baadhi ya sababu hizo ni kujikweza, kukata tamaa na kukosa kusudi maishani. Matatizo ya kifedha, ukosefu wa kazi, na mifano mibaya ya wazazi huchangia pia tatizo hilo. Watu fulani wanaoshindwa kushirikiana na wengine hutumia dawa za kulevya ili kukabiliana na hali hiyo. Wanaamini kwamba dawa za kulevya huwasaidia kuwa na ujasiri, zinawafanya wawe wacheshi na wahisi wanapendwa. Wengine huona ni rahisi kutumia dawa za kulevya badala ya kujifunza jinsi ya kukabiliana na maisha.

Vijana hutumia dawa za kulevya kwa sababu hawana la kufanya. Kitabu ‘The Romance of Risk—Why Teenagers Do the Things They Do’ kinaeleza hivi kuhusu kutokuwa na jambo la kufanya na kutopata mwelekezo wa wazazi: “Wavulana na wasichana wanaporejea kutoka shuleni hawamkuti mtu yeyote nyumbani. Hivyo wanahisi upweke na hawataki kuwa peke yao, wanatembelewa na marafiki lakini bado wanahisi uchoshi wakiwa pamoja. Wanatazama televisheni na video za muziki kwa muda mrefu au kutafuta mambo yenye kusisimua kwenye mtandao. Haitoshi vijana huanza kuvuta sigara, kutumia dawa za kulevya na kunywa pombe.” Lengo ni kutafuta furaha na kuishughulisha akili.

Vijana wengi wameanza tabia zisizofaa ikiwa ni pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya katika kipindi cha likizo, kipindi ambacho wapo tu majumbani wakitembeleana na kutembea sehemu mbalimbali kwa lengo la kupoteza muda. Mara tu baada ya kuanza kutumia dawa za kulevya, vijana wengi huendelea kuzitumia kwa sababu moja tu, wanafurahia kufanya hivyo.

Rashid Makwilo ‘Chid Benz’, mwenyeji wa Ilala jijini Dar es Salaam, inasemekana alianza kutumia dawa za kulevya kwa kupenda tu na amekuwa hataki kusikia lolote kutoka kwa watu wanaohitaji kumsaidia, na kila akisaidiwa kupelekewa vituo vya kawasaidia waathirika wa dawa za kulevya (Rehab) anatoroka. Zimefanyika jitihada mbalimbali kama vile kumshauri na kumshirikisha mambo ya kijamii ili asipate muda wa kujiunga na waathirika wa dawa hizo.

Inaonekana vijana hata hawatishwi na maonyo yanayotolewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya. Wao hudhani kwamba ‘hawawezi kupatwa na madhara hayo.’ Kitabu cha Talking With Your Teenager chaeleza kwa nini vijana hupuuza maonyo kuhusu madhara ya dawa za kulevya kwa afya: “Wana afya nzuri na nguvu nyingi hivi kwamba wanafikiri afya yao haiwezi kuathiriwa. Kwa kawaida vijana wengi wanaobalehe hudhani kwamba hawawezi ‘kuumizwa.’ Vijana huona kansa ya mapafu, ulevi, uraibu wa dawa kali za kulevya, kuwa mambo yanayowapata watu wenye umri mkubwa, na hayawezi kuwapata wao.” Kwa kweli wengi hawajui hatari zilizopo. kama inavyothibitishwa na idadi inayoongezeka ya vijana wanaotumia dawa ya kulevya.

Utumiaji wa dawa za kulevya una athari nyingi sana kuanzia ngazi ya familia mpaka taifa kwa jumla, moja kati ya athari hizo nyingi kwa mtu mmoja mmoja ni kupumbaa akili.