RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MAJALIWA AAGIZA UCHUNGUZI MATOKEO MABAYA SHULE ZA MTWARA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameuagiza uongozi wa Wizara wa Elimu Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwenda mkoani Mtwara kufanya uchunguzi ili kubaini sababu za shule tisa za mwisho katika matokeo ya kidato cha pili kutoka mkoani humo.

Pia ameziagiza halmashauri nchini kushirikiana na Idara ya Ukaguzi ili kuhakikisha zinawasimamia vizuri walimu, jambo litakaloboresha ufundishaji na hatimaye kupata matokeo mazuri.

Majaliwa ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na watumishi na wananchi wa Mkoa wa Katavi alipowasili Ikulu ndogo ya Mpanda kwa ajili ya kufungua duka la dawa la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) katika hospitali ya Manispaa ya Mpanda.

Kwa mujibu wa matokeo hayo kati ya shule 10 za sekondari zilizofanya vibaya kwenye mtihani huo, tisa zinatoka katika mikoa ya Mtwara na moja Tanga. Shule za Mtwara zilizofanya vibaya ni Chingungwe, Malocho, Naputa, Chanikanguo, Mtiniko, Michiga, Msimbati, Salama na Lukodoka huku ya Tanga ikiwa ni Nywelo.

“Viongozi wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) waende Mtwara wakafuatilie kwa kina wajue kuna nini hadi shule tisa kati ya 10 zilizofanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya kidato cha pili mwaka jana zitoke huko,” alisisitiza.

Mbali na kuuagiza uongozi wa wizara hizo kwenda mkoani Mtwara, Waziri Mkuu amewataka wasimamie vizuri mikoa ambayo awali ilikuwa na matokeo mabaya na sasa inafanya vizuri na wahakikishe shule za mikoa hiyo hazishuki na badala yake ziendelee kupata matokeo mazuri zaidi.

Awali, akisoma taarifa ya mkoa huo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga alisema katika matokeo ya mtihani kidato cha pili ya mwaka jana mkoa wake ulishika nafasi ya pili kitaifa ukiongozwa na mkoa wa Geita.

Alisema kwa sasa wanajipanga kuhakikisha katika mitihani ya mwaka huu wanashika nafasi ya kwanza kitaifa, hivyo alitoa wito kwa watendaji wa idara ya elimu, wakuu wa shule, wazazi na walezi kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha malengo hayo yanafanikiwa.

Salum Milongo/ GPL