RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MAMBO MUHIMU UNAYOPASWA KUYAFAHAMU KABLA YA KUWEKEZA KWENYE GREENHOUSE.

Habari ndugu msomaji wa AMKA MTANZANIA, ni matumaini yangu unaendelea vizuri na mapambano ya kuelekea kwenye mafanikio. Karibu tena katika kona hii ya kupata maarifa ya kilimo. Leo tutaendelea na mfululizo wa makala zinazohusu kilimo cha greenhouse. Kwa leo tutaangalia mambo machache ambayo unapaswa kuyafahamu kabla ya kuingia kwenye kilimo hicho. Pia tutajifunza baadhi ya vigezo vya kuzingatia wakati wa kuchagua eneo la kuweka greenhouse.

Karibu Tujifunze: 
Kwanza kabisa ningependa tuanze na hii dhana iliyojengeka kwamba ukifunga greenhouse unapiga hela za harakaharaka tena kirahisi. Ni kweli kuna hela kwenye kilimo cha greenhouse lakini sio pesa ya kirahisi kama ambavyo watu wamekua wakiaminishwa. Narudia kusema kwamba fedha ipo nzuri kwenye uwekezaji wa greenhouse lakini sio kama wapiga debe wa teknolojia hiyo wanavyotaka wakulima waamini na kununua haraka haraka. 
Ahadi za uongo. 
Watu wamekua wakipewa uhakika wa mavuno mengi sana kwa muda mfupi. Mfano mtu anaambiwa utapata tani 30 kwa miezi 6 hadi mwaka mmoja kwenye greenhouse ndogo tu (8 X15m) akipiga hesabu za haraka anajua tani 30 ni sawa na kilo 30,000 akiuza kila kilo 1000 anapata milioni 30 (30,000,000) mtu anaona milioni 30 kwa miezi 6 wakati greenhouse nimenunua milioni 5 au 6, hapo watu wanachanganyikiwa wengine wanachukua mkopo, wengine wanauza hata mali zao zisizohamishika kama ardhi ili na wao wamiliki greenhouse. 
Kufanya hivyo sio tatizo (kuuza vitu ili kuwekeza) tatizo ni ule mtazamo mtu anaokua nao akijua kwamba anakwenda kuvuna mahela ndani ya muda mfupi. Hii ni biashara kama zilivyo nyingine na ina vihatarishi vyake (risks). Wapo watu ambao wamekua wakijiita wataalamu wa kilimo cha greenhouse lakini wamekua wakitoa ushauri ambao sio sahihi pengine ni kutokana na mtazamo wa kibiashara zaidi walio nao. 
Elimu/Maarifa Sahihi. 
Katika kilimo cha greenhouse kama ilivyo biashara yeyote, maarifa ni nguvu (knowledge is power). Lakini kwa bahati mbaya wakulima wengi wao wanapenda kufahamu tu gharama ya kuwekeza kwenye greenhouse na ni haraka jinsi gani watakavyoweza kurudisha fedha zao na kuanza kupata faida. 
Kama ilivyo biashara nyingine pata elimu na taarifa sahihi. Jifunze kutoka kwa wataalamu, ikiwezekana tenga hata muda wa kutembelea wakulima ambao wamefanikiwa kwenye kilimo hicho cha greenhouse, ili wakupe uzoefu wa uhalisia. Usikwepe gharama kwa kutaka kufanya ujuavyo maana gharama yake itakua kubwa zaidi. 
Kwa wale wenye ufahamu wa kutumia intaneti zipo taarifa nyingi tu kuhusu kilimo hicho, jifunze kuhusu fursa zilizopo lakini pia changamoto na jinsi ya kuzivuka. 
Kutokana na uhitaji wa watu kupata elimu na maarifa kuhusu kilimo cha greenhouse siku za mbeleni tutakua tunaandaa programu maalumu kwa ulimaji wa greenhose. Tutaendesha mafunzo kwa wale wenye nia haswa ya kuwekeza kwenye kilimo hichi. 
Ukiacha ukosefu wa elimu ya kutosha pia ukosefu wa nia ya dhati (commitment) ni sababu nyingine ambayo imekua ikifanya kilimo hiki cha greenhouse kufanya vibaya kwa baadhi ya wakulima wa Uganda na hata hapa kwetu Tanzania. 
Watu wengi wamekua wakiingia katika uwekezaji wa kilimo cha greenhouse wakiwa wanafanya kazi sehemu nyingine (full time jobs) kwa hiyo kazi za kila siku za kwenye greenhouse zinaachwa kwa wafanyakazi ambao uwezo wao na uwajibikaji wao ni wa kutilia mashaka. Unakuta mmiliki wa greenhouse ndiye kapata mafunzo ambayo hata hayaridhishi lakini shughuli zinasimamiwa na mtu mwingine ambaye ana uelewa mdogo zaidi kuliko hata mmiliki, sasa hapo yakitokea yakutokea lawama zinakua nyingi. 
Hali ya hewa ndani ya greenhouse mara kwa mara inabadilika hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu. Ukuaji wa mimea unategemea sana hali ya hewa ndani ya greenhouse. Katika nchi zilizopiga hatua sana kwenye kilimo hichi kama Israel na Uholanzi hali ya hewa ndani ya greenhouse inadhibitiwa kwa kutumia kompyuta. Lakini kwa Tanzania na nchi nyingi za Africa Greenhouse zinazomilikiwa na wazawa shughuli hizi zinafanywa kwa njia za kawaida kama mkono n.k. Kwa hali kama hiyo kufanya ufuatiliaji wa shughuli za kwenye greenhouse kwa kupitia simu au kwa kutembelea kwa masaa machache tena mara moja moja hii inakua ngumu sana kufanikiwa kwenye hichi kilimo. 
Njia nzuri na yenye ufanisi ambayo wakulima wanaweza kunufaika na biashara ya kilimo cha greenhouse ni kwa kujikusanya vikundi au ushirika kwa ajili ya kukusanya rasilimali za kutosha za kufanyia shughuli hii. Huu ni ushauri kwa wale wenye uwezo mdogo. Hii itakua rahisi kwa kuajiri mtu mwenye sifa na uwezo aliyefuzu kabisa (professional manager) wataweza pia kumudu kupata mafunzo kutoka kwa wataalamu waliobobea wataweza kuandaa ziara za kwenda kujifunza kwa wengine (study tours) kwa umoja wao wataweza kutafuta msaada wa kifedha kutoka kwenye taasisi mbalimbali zinazohusika. 
Ila kadiri wanavyoendelea kupata uzoefu wanaweza kutengeneza greenhouse kama mtu binafsi lakini wakaendelea kununua pembejeo na kuuza mazao yao kwa umoja. Maana wanaponunua pembejeo kwa ujumla ni rahisi kupata kwa bei ya punguzo kidogo maana mnaagiza kwa wingi. 
Uchaguzi wa eneo kwa ajili ya kuweka Greenhouse 
Kuchagua eneo sahihi ni muhimu sana. Uchaguzi wa eneo zuri kutaamua kufanikiwa au kutokufanikiwa kwa biashara yako. 
Kuna vigezo 12 vya kuzingatia wakati wa kuchagua eneo ila tutaangalia vigezo 4 kwa kifupi. 
1. Mwanga wa Jua (Solar Radiation) 
Mimea inahitaji mwanga kwa ajili ya kutengeneza chakula chake. Eneo linahitaji kua na mwanga wa kutosha. Mwanga kidogo unapunguza utengenezaji wa chakula kwa mimea. Hivyo usiweke greenhouse sehemu palipojificha, kama vile chini ya miti. Utengenezaji wa chakula ukipungua kutokana na kukosa mwanga wa kutosha hii ina maana : 
· Ukuaji wa mimea unapungua. 
· Maua au matunda yatadondoka kabla ya wakati. 
· Mavuno yatapungua na kipato nacho kitapungua. 
2. Upatikanaji wa Maji 
Eneo la uwekezaji liwe karibu na chanzo cha maji au eneo ambalo maji yanaweza kufika kwa wakati wote yanapohitajika. Eneo linaweza kua karibu na mto, bwawa au kisima cha kuchimba. Ila sio maji tu, lakini ubora wa maji ni muhimu pia. Kuna maeneo ambapo siyo mazuri kwa umwagiliaji wa mimea. Kama inawezekana fanya upimaji wa maji ili kujua kiwango na aina ya chumvi na kiwango cha pH(uchachu). pH ya maji inatakiwa 5.8-6.5 kwa nyanya. Kama maji yana kiwango cha pH kilichozidi maji hayo yatahitaji kutibiwa kwa asidi (nitric acid). Kama maji yana kiwango cha asidi chini 5.5 maji hayo yatahitaji kutibiwa kwa kutumia base/alkali (oH). 
3. Upepo mkali 
Kwa maeneo ambayo kuna upepo mkali yanaweza kuathiri greenhouse. Upepo mkali unaweza kuharibu muundo wa greenhouse Upepo mkali unaweza kuondoa joto lililopo ndani ya greenhouse (joto ambalo linahitjika kwa ajili ya ukuaji wa mmea). Unaweza kuweka vikinga upepo (wind break) kama kujenga ukuta imara au kupanda miti ambayo itatumika kama kizuizi 
4. Barabara/Miundombinu: Green house inapaswa kuwekwa eneo ambapo panafikika kirahisi. 
Mfano wa Greenhouse na bei yake: 

Greenhouse package PRICE Tsh(VAT+)
9m x 15m: Tropical Model Kit , Open Roof; drip irrigation; chemicals package; Fertilizer package; Agronomic Support & Installation 10,980,000
Hii ni greenhouse yenye upana wa mita 9 na urefu wa mita 15. Unapatiwa na vifaa vya umwagiliaji (mipira na tenki. Pia unapata dawa za kuanzia za kupiga wadudu na magonjwa, mbolea za kuhudumia mimea, unapata msaada wa kitaalamu pia unafungiwa Greenhouse yako. 
Wiki ijayo tuweka hapa aina nyingine za Greenhouse na mchanganuo wake, ili kwa mwenye kuhitaji aweze kuchagua kulingana na ubora na ukubwa wa Greenhouse. 
Asante sana.