RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

NABII NA MTUME JOSEPHATE MWINGIRA: NINI UFANYE ILI MAOMBI YAKO YAJIBIWE?


Wewe uliyeokoka uwe sababu ya kuwafanya wale waliomjua Mungu kwa kupitia wewe wasirudi nyuma. Usikubali kuwa sababu ya kuwaumiza wengine kwa tabia yako au maneno yako na kusababisha wale Mungu aliokupa kuwalea wakashindwa kusonga mbele.

Imani sio kwenda Kanisani tu bali Imani pia ni kuwapenda wengine na kusababisha wavutwe na kumfuata Mungu.

Mtu aliyeokoka na kukua kiroho anapokutana na changamoto anatakiwa kutiwa moyo ili asonge mbele sio kubembelezwa.

Huu ni mwaka wa kujibiwa maombi yetu, lakini ili maombi yetu yapate kujibiwa ni lazima tufanye mapenzi ya Mungu kwa kukubali kuzaa matunda na matunda yetu yapate kukaa, sio unazaa matunda baada ya miaka miwili yanakufa. Kama ambavyo binadamu akibeba mimba ikaharibika anaumia ndivyo hivyo Baba yetu wa Mbinguni anahuzunika mtu anapookaka na kurudi nyuma. Ili uweze kuwa bora katika maisha yako ni vizuri kuhakikisaha hauwi sababu ya kuwakwaza wengine kwa maneno au matendo yako.

Katika utaratibu wa Mungu Mume anatakiwa kumfurahisha Mungu kwa gharama yoyote, lakini mke anatakiwa kumfurahisha Mume wake na watoto wanatakiwa kumfurahisha mama yao. Mwanaume asiye na akili anasubiri mke wake akatafute pesa kwaajili ya kutunza familia, lakini mwanaume mwenye akili nzuri anatafuta pesa kwa bidii analeta chakula nyumbani na mke anampikia na kumpetipeti.

Unapokubali kufanya hivyo unasababisha Amani, furaha na ustawi mkubwa katika familia yako na ugomvi hautakuwepo. Watoto lazima wamuheshimu mama yao na wakati mama anapomuadhibu mtoto wewe baba usimtetee mtoto hii itasaidia watoto wako kuwa na adabu. Mama kujua kuomba sana kusikufanye umpuuze mumeo kwani yeye ni kichwa cha familia.

Unapokubali kuoa ina maana umekubali kubeba majukumu ya familia, ukubali kuambiwa sukari imeisha, chumvi, kitenge na unapoambiwa usikasirike kwani ni jukumu la baba kutunza familia sio mama. Kwa asili wanaume hawapendi kelele ndio maana Mungu amesema ishi na mke wako kwa akili na sio maombi, wewe baba usianze kufanya maombi ili sukari ije bali nenda kafanye kazi kwa bidii na umtumikie Mungu kwa bidii ndipo utaona baraka katika familia yako, katika kitabu cha mwanzo kimeeleza nafasi ya mwanamke kuwa ni msadizi na msaidizi hatoi amri kwa kichwa(mume). Ukikubali kuolewa ukubali kukandamizwa kwa sababu kichwa kiko juu yako(mume) na wewe ni kama kiwiliwili. Ukikubali kuyafanya haya utamwona Mungu kwa sababu Mungu anaonekana sana katika familia.

Ni hatari sana familia ambayo haiwezi kumsikiliza mama yao na kwa kufanya hivyo hiyo familia itaharibikiwa. Kazi ya baba ni kuonyesha njia na akisha onyesha njia mama ana kazi ya kuielekeza familia yake namna ya kupita katika ile njia. Mama unatakiwa kukaa mkao wa mama na baba unatakiwa kukaa mkao wa baba na wewe binti kaa mkao wa mwanamke sio unakaa kama dume, unatakiwa uonyeshe kuwa unafaa kuwa mama wakati wowote.

Mwanaume mwenye akili hata mke wake anajisikia fahari kuolewa nae. Unatakiwa kuangalia je tabia yako inamuonekano wa Mungu au unaonyesha una shetani? Unapokubali kufanya mapenzi ya Mungu, utaona mapenzi ya Mungu katika maisha yako kwani Mungu sio dhalimu.

Siku hizi wanawake wanataka faraja kwa waume zao lakini biblia haisemi hivyo bali inasema mume anatakiwa kuwa faraja kwa Mungu na mke anatakiwa kuwa faraja kwa mume na watoto wanatakiwa kuwa faraja kwa mama yao, ndio maana neno linasema mwana mpumbavu ni mzigo wa mama yake. Binti na Kijana wa kazi wanatakiwa kumsaidia mke na sio wewe mwanaume, kazi yako wewe mwanaume ni kutafuta pesa ni ujinga kupangiana na mume wako zamu ya kupika. Mwanaume lazima ukubali kuchoka, mwanaume ni mpiganaji. Onyesha wewe umekubalika na Mungu kwakuweka familia yako katika hali ambayo Mungu akikaa kule juu anatamani kuitembele hiyo familia,

Tabia yako inaambatana na mawazo yako na mawazo yako yanaambatana na maombi yako na tabia yako inaonyesha maombi yako yatakuwa ya namna gani, jitahidi kwa nguvu zako zote kutafuta mapenzi ya Mungu. Mungu hawezi kuku bariki wakati wewe hautunzi familia yako. Haulindi heshima ya Mungu watu wanamtukana Mungu kwa sababu ya tabia yako pale nyumbani. Unaonaje ukapiga magoti ukamwambia Mungu ni dhambi gani inayonifanya nisiwe furaha yako? Mungu ni mwaminifu atakuonyesha ili ubadilike na usonge mbele.