RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

MWANAMKE AFUKUA MAITI YA MWANAYE, AIVISHA SUTI.


RUTH Segeleti (52) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufukua kaburi la mwanaye aliyefariki dunia Februari 15 mwaka huu. Mwanamke huyo alifukua kaburi na kuutoa mwili wa mwanaye na kuuvalisha suti ili mchungaji aufufue. Mwili huo ulikutwa umewekwa kwenye pagala moja.

Baraka Mwafongo 22, alifariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu ambapo mama yake aliruhusu azikwe na huku akiamini bada ya siku tatu mtoto huyo angefufuka.

Baada ya wakazi kubaini kaburi la mtoto huyo limefukuliwa watu wengi walijaa makaburini hapo ambapo baadaye polisi waliitwa na kufika. Wananchi waligundua kuwa kaburi lilikuwa wazi majira ya saa tatu asubuhi baada ya majirani kumuona mwanamke huyo akiwa na jembe mkononi na furushi la nguo akitokea makaburini.

“Nilipomsemesha, hakutaka kunijibu,” alisema mkazi wa mtaa huo, Mariam Mwakisepile, ambaye ni jirani wa mwanamke huyo.

“Nililazimika kuwaarifu majirani wengine ambao walikwenda makaburini ambako walikuta kaburi la Baraka likiwa limefukuliwa,” aliendelea kusema.

Shuhuda mwingine wa tukio hilo, Christina Nyopelo, alisema walipiga simu kituo cha polisi cha Mbalizi na kuwaarifu.

“Baada ya muda mfupi polisi waliwasili na wakiwa makaburini waliona sanduku ndani ya kaburi, lakini mwili haukuwapo,” alisema Nyopelo.

Polisi kwa kushirikiana na wananchi waliamua kukagua maeneo ya makaburi na hatimaye walifanikiwa kuukuta mwili ukiwa umelazwa kwenye banda lililopo karibu na eneo hilo.

Habari hizo zilisambaa na kukusanya kundi la watu kutoka mji wa Mbalizi na kusababisha polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya. Alisema baadaye polisi walikwenda nyumbani kwa mwanamke huyo na kumkamata, pia waliupeleka mwili wa Baraka, Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya kuuhifadhi. Kamanda Kidavashari alisema mtuhumiwa alipelekwa Kituo cha Polisi Mbalizi kuhojiwa.

Umati wa watu pia ulijazana Mtaa wa Shigamba na kusababisha polisi walipue mabomu ya machozi ili kuwatawanya watu. Jitihada hizo zilizaa matunda kwa muda mfupi, lakini ilipofika saa nane mchana watu wasiofahamika waliichoma moto nyumba ya mwanamke huyo.

Katika kukabiliana na tukio hilo, polisi waliwatawanya wananchi kwa kupiga baadhi ya watu waliokutwa eneo la tukio. Kamanda Kidavashari alisema polisi wanawasaka watu waliohusika kuchoma moto nyumba ya mwanamke huyo.