RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

AMINA MOHAMMED: MWANAMKE WA PILI KULA KIAPO KUWA NAIBU KATIBU MKUU WA UN



Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Antonio Guterres, akimuapisha naibu katibu mkuu wake, Amina Mohammed raia wa Nigeria. 28 Februari 2017.UN Photo/Mark Garten

Aliyekuwa waziri wa mazingira wa Nigeria, Amina Mohammed, ameapishwa rasmi kuwa naibu katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.

Amina amekula kiapo mbele ya katibu mkuu Antonio Guterres ambaye alimchagua kwenye nafasi hiyo mwezi Desemba mwaka jana. Hata hivyo alikuwa amerejea nchini mwake kukabidhi ofisi kama waziri wa mazingira wa nchi hiyo.

Balozi Amina alikuwepo wakati wa sherehe za kuapishwa kwa katibu mkuu Guterres, ambapo baadae alirejea nchini mwake kuhudhuria vikao vya mwisho mwisho vya baraza la mawaziri nchini Nigeria.

Amina anakuwa mwanamke wa pili kipekee kushika wadhifa huo wa naibu katibu mkuu, ambapo mwanamke wa kwanza alikuwa Asha Rose Migiro raia wa Tanzania aliyehudumu kwenye nafasi hiyo toka mwaka 2007 na 2012 chini ya katibu mkuu wa wakati huo, Ban Ki-Moon.

Kama naibu katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Amina anatarajiwa kwa muda mwingi kufanya shughuli zake nyuma ya pazia, ambapo kwa mujibu wa katibu mkuu Guterres, uteuzi wake unaendana na mabadiliko ambayo anaelekea kuyafanya kwenye umoja wa Mataifa.