RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

SALAMA WA TAIFA WAZUIWA BUNGENI

NAIBU SPIKA WA BUNGE, DK. TULIA ACKSON.

BUNGE limepiga marufuku masuala ya Usalama wa taifa kujadiliwa ndani ya chombo hicho isipokuwa kama mbunge anaweza kuwasilisha hoja mahsusi.

Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alitoa uamuzi huo jana wakati Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Angelina Malembeka alipokuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka wa fedha wa 2017/18.

Katika kuchangia mjadala huo, Malembeka alisema Idara ya Usalama wa Taifa inapaswa kuanza kuwahoji wabunge walioeleza kuwa wana orodha ya wabunge 11 wanaotarajiwa kutekwa nyara na idara hiyo.

Kufuatia mchango huo, Dk. Tulia alisema Bunge haliruhusiwi kuzungumzia kila jambo kwa sababu kuna mambo ambayo sheria zilizotungwa na wabunge zinawazuia kufanya hivyo.

Alisema Kanuni ya 5 na ya 64 1(c) ya Bunge zinaeleza kuwa endapo Mbunge ataleta hoja hiyo mahsusi, anaruhusiwa kuzungumzia suala la idara hiyo nyeti ya serikali.

Alisema kwa kuwa hoja ya Usalama wa Taifa haijawasilishwa mezani na Mbunge Malembeka kama hoja mahususi, suala hilo halipaswi kujadiliwa.

“Kwa kutumia kanuni ya 5 ya kanuni zetu za Bunge na kanuni ya 64 1(c), kama mtu ataleta hoja hiyo mahsusi anaruhusiwa, lakini kwa kuwa hoja hiyo haikuwa mezani mahsusi, wabunge... suala la mjadala kuhusu Usalama wa Taifa linaishia hapa kwa leo mpaka pale mtu mwingine atakapoleta hoja mahsusi kupitia kanuni zetu kama zinavyotuambia,” alisema Dk. Tulia.

Alisema kuna mambo ambayo ni kazi ya bunge kufanya na pia kuna mambo ambayo ni kazi ya vyombo vingine nje ya bunge.

MZAHA KILA MTU
Wakati akichangia, Malembeka alisema kwa sasa imekuwa mzaha kwa kila mtu kusema kuwa ametekwa au atatekwa na Usalama wa Taifa, hivyo kutaka idara hiyo kuanza na wabunge waliosema wana ushahidi kuwa kuna wenzao watatekwa.

“Ni vizuri Usalama wa Taifa wakaongezewa fedha wapate mbinu mpya," alisema Malembeka, na "waongozewe vifaa tuweze kupata usalama zaidi."

"Kutwa mtu anatuma sms (ujumbe mfupi wa simu ya mkononi) kwa rafiki yake eti nimetekwa nyara... hebu waulizeni waliotekwa nyara hiyo simu wamepata wapi?

“Naomba Mheshimiwa waziri uwashughulikie kwa sababu sasa hivi mtu akishakata panki lake akavaa kaunda suti yake anatoa kitambulisho, anasema mimi Usalama wa Taifa. Usalama wa Taifa si mchezo.

"Mtu anajizungusha zungusha anawatisha watu mtaani unasema Usalama wa Taifa. Sasa wale wanaojifanya Usalama wa Taifa na kuogopesha watu mtaani washughulikiwe.”

Naye Mbunge wa Mchinga (CUF), Amidu Bobale alisema hatua ya suala la Usalama wa Taifa kuanza kuwashughulikia wabunge ni kulishusha hadhi bunge. Alisema mambo yanayozungumzwa bungeni kwa mujibu wa katiba ya nchi hayahojiwi kokote.

TETEMEKO LA ARDHI
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Severin Mwijage alihoji matumizi ya fedha zilizochangwa na wananchi na wafadhili kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, mwaka jana mkoani Kagera.

Alisema baadhi ya shule za sekondari zilizoguswa na tetemeko hilo hazijajengwa hadi leo.

“Kuna shule ziko Iyungo na Nyakato, hazijajengwa hadi leo na fedha zipo," alisema Severin.

"Watu wanashangaa sana, hizo fedha zilichangwa ili kuwasaidia waathirika lakini zikapelekwa sehemu ambayo ni ujenzi wa miundombinu.”

Naye Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Upendo Peneza alisema suala la utawala bora, uwazi na uwajibikaji ni la msingi na kwamba miaka ya nyuma wananchi wameshirikiana na wabunge kuiwajibisha serikali tofauti na utawala wa sasa.

Alisema miaka ya nyuma pia kulikuwa na ‘Bunge live’ ambako nao waliwasaidia kujua kinachoendelea moja kwa moja.

'Bunge live' lilibadilisha mfumo dume, alisema, kwani wananchi waliona kinachoendelea kwa kusikiliza Bunge.