RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

Ronaldo Amezaliwa Maskini, kwa Nini wewe Ushindwe?


MAKALA: Nyemo Chilongani na Mtandao

MPENZI msomaji lengo la ukurasa huu ni kupeana mbinu za namna ya kutengeneza fedha na kupata utajiri hivyo usipange kukosa kufuatilia kila Jumatatu.

Bado kuna baadhi ya watu hawaamini kwamba mtu anaweza akatoka katika umaskini wa kutupwa na baadaye kuwa bilionea anayetengeneza fedha ndefu. Wapo wanaoamini kwamba kuna watu wamezaliwa kwa ajili ya kuwa matajiri tu. Lakini pia kuna wengine wakikaa na kumwangalia Bill Gates au Mark Zuckerburg wanaona kwamba walizaliwa wakiwa hivyo, kwenye familia za kitajiri ndiyo maana kwa sasa ni mabilionea wakubwa.


Ndugu yangu, kama unafikiria hivyo, utakuwa unakosea na hilo linaweza kukufanya kuwa mahali ulipo kwa miaka nenda rudi na utajiri ukabaki kuusikia kwa wengine.

Nikukumbushe tu kuwa, hakuna kati yetu aliyezaliwa na nguo. Wote tumezaliwa tukiwa watupu lakini tunapokufa, tunakuwa tumeacha vitu vingi nyuma yetu.

Wiki iliyopita Jarida la Forbes la nchini Marekani linalojihusisha na kutafiti rekodi za utajiri walionao watu mbalimbali duniani lilitoa orodha ya wanamichezo wanaoingiza mkwanja mrefu kwa mwaka. Amini, usiamini, kijana yuleyule ambaye alikulia kwenye umaskini mkubwa nchini Ureno, kijana ambaye baba yake alikuwa mlevi wa kupindukia ambaye hakuweza kuingiza kiasi kikubwa cha fedha, mshambuliaji wa Klabu ya Real Madrid ya Hispania, Cristiano Ronaldo ‘CR7’ ndiye ameshika nafasi ya kwanza kwa mwaka huu akijiingizia kiasi cha pauni milioni 71.8 ambazo ni zaidi ya Sh. bilioni 200 za Kitanzania.


Yaangalie maisha yako, inawezekana leo hii una fedha kuliko hata walizokuwanazo familia ya Ronaldo wakati anazaliwa. Inawezekana kabisa kwani miongoni mwa nchi maskini barani Ulaya ni Ureno na ina uchumi wa chini hata zaidi ya Afrika Kusini.

Unaposoma hapa leo, Ronaldo ni bilionea, anatengeneza fedha kila siku, miguu yake ni fedha ndefu. Unapomwangalia Ronaldo, usiangalie mafanikio yake, hebu angalia juhudi zake ambazo zimemfanya kufika mahali alipo leo, kupambana kwake kuwe chachu kwako.

Hebu tuangalie baadhi ya vitu ambavyo vimemfanya Ronaldo kufika hapo alipo ambavyo naamini kama na wewe utavifanya, unaweza kupiga hatua;


1: KUJITUMA KUFANYA KAZI KWA BIDII

Hii ndiyo chachu ya mtu yeyote anayetaka mafanikio. Si Ronaldo tu, wasikilize mabilionea wote, kitu cha kwanza kabisa wanachokisema ni kufanya kazi kwa bidii. Huwezi kufanikiwa kiujanjaujanja tu. Huwezi kusema kwamba usiku unapolala tu, ukiamka asubuhi utakuwa tajiri mkubwa, kwenye kufanikiwa, kuna siri moja kubwa, nayo ni hii.

Ronaldo amekuwa mfuasi mkubwa wa hili, mara kwa mara imeripotiwa kwamba yeye ndiye mtu wa kwanza kufika mazoezini, anafanya mazoezi saa mbili kabla ya wenzake kufika na huondoka baada ya wenzake kuondoka.

Aliona kwamba bila kufanya kazi kwa bidii, hakuna mafanikio. Bidii na kujituma kwake kumemfanya kuchukua tuzo ya uchezaji bora wa dunia mara nne mpaka sasa. Kama Ronaldo alifanya kazi kwa bidii na kufanikiwa, kwa nini wewe ushindwe? Unahisi Ronaldo ana miguu minne? Unahisi ana ubongo wenye nguvu ya kufikiria zaidi yako? Hapana. Kile ulichokuwanacho ndicho ambacho kinakuingizia fedha. Hebu kifanye kwa nguvu kubwa, inapowezekana kukesha usiku kucha, kesha. Jambo hilo linapokutaka kuhangaika huku na kule, fanya hivyo na mwisho wa siku utafanikiwa.


2: UWE NA UPINZANI UTAKAOKUSUKUMA

Ukifanya kazi kwa bidii ni lazima utafanikiwa, ila ili ufanikiwe zaidi ni lazima uwe na mpinzani mmoja. Mwangalie Ronaldo, mpinzani wake mkubwa ni mshambuliaji wa FC Barcelona ya Hispania, Leonel Messi. Amekuwa akijituma sana kwa ajili ya kumpiku mpinzani wake huyo. Hupambana usiku na mchana huku kichwa chake kikimfikiria Messi, ni kitu gani anatakiwa kufanya ili kumpiku mpinzani wake.

Hata wewe kwenye biashara zako ni lazima uwe na mpinzani ambaye anaonekana kuwa bora zaidi yako. Ni lazima upange mikakati mikubwa ya kuweza kupambana naye. Hili litakusaidia kwani itakulazimu kupambana usiku na mchana kuhakikisha unatoka mahali hapo ulipo.

Leo, Microsoft wasingepiga hatua kubwa zaidi kama kusingekuwa na Apple. Walipokuwa peke yao, walifanya kazi kawaida, lakini baada ya Apple kuibuka na kuleta upinzani, nao pia wakaongeza gia na kupiga hatua zaidi. Ni lazima utafute mpinzani wa kupambana naye kimyakimya ndipo utafanikiwa zaidi, vinginevyo hutapiga hatua kubwa kama unayotakiwa.

3: TAMANI KUWA BORA KULIKO WOTE

Hili ni muhimu sana katika safari ya mafanikio. Ronaldo aliliangalia taifa lake, akawaangalia wachezaji waliopita akiwemo Luis Figo, walikuwa ni wachezaji bora ila alichokitaka ni kuwa bora zaidi ya wote waliowahi kupita. Akapambana hadi sasa hivi amekuwa bora zaidi ya wengine.

Hilo ndilo unalotakiwa kufanya. Kuna watu wamekutangulia ambao wamekuwa bora zaidi yako, panga mikakati mikubwa ili kuwa bora hata zaidi yao. Hili litakufanya kufanikiwa. Hebu fikiria taifa kama Ureno kusingekuwa na watu bora waliopita, unadhani Ronaldo angepambana zaidi? Hapana, asingekaza kamba, ila kwa kuwa kulikuwa na waliokuwa bora, naye akakaza ileile na leo amefanikiwa zaidi.

4: SAIDIA WENGINE BAADA YA KUFANIKIWA

Hili halikwepeki rafiki yangu. Ili uweze kufanikiwa zaidi ni lazima uwe unasaidia watu wengine kifedha au kimawazo. Ni mara nyingi tumesikia Ronaldo akisaidia watu wenye matatizo mbalimbali hadi kufikia hatua ya kuuza kiatu chake cha dhahabu kisha kwenda kusaidia watoto walio kwenye matatizo makubwa ya vita nchini Palestina.

Unapofanikiwa wasaidie wengine huku ukikumbuka kwamba hakuna mtu aliyefilisika kwa kufanya hivyo. Unaposaidia wengine, Mungu anakubariki zaidi. Rafiki yangu, unapomwangalia Ronaldo, usiangalie tu mafanikio yake, bali angalia njia alizopitia kufika hapo ili uwe mfano mzuri kwako.