RUMAFRICA Magazine

RUMAFRICA FASHION

RUMAFRICA FASHION

KUWA MWENYE FURAHA NI UAMUZI WAKO MWENYEWE!

Ni mara ngapi umewahi kukutana na mtu aliyekukwaza kiasi cha kumtupa katika kapu la “watu wa hovyo” wasiostahili heshima kama binadamu? Umewahi kupatwa na tukio ambalo lilibadili kabisa mtazamo wako kuhusu maisha, watu na maisha kwa ujumla? Kwa nini watu kukata tamaa? Umewahi kuwaza kwa nini kinachomkwaza huyu si lazima kimkwaze yule?
Umewahi kuonana na mtu anayeshangaa inakuwaje “huyu bwana achukue uamuzi wa ajabu namna ile” wakati kilichotokea kinachukuliwa na wengi kuwa “ni jambo la kawaida”?

Natamani ukimaliza kusoma hapa uelewe kwamba sehemu kubwa ya matatizo tunayokabiliana nayo kama binadamu kila siku, tunayasababisha wenyewe. Na kwa yale tusiyo naudhibiti nayo, tunaweza kubadili mtazamo wetu kwayo, na hilo linaloonekana kuwa tatizo ama likawa si tatizo au likabadilika kuwa changamoto. 

Wengi wetu tunapokumbana na vikwazo (ambavyo mara nyingi huwa ni watu, vile mambo yalivyo na matukio yanayokuwa katika namna tusiyoitegemea) hujenga mawazo kwamba vitu hivyo vi vibaya. Matokeo yake tunatumia muda mwingi sana kusononeka na hivyo kujikuta tukijiumiza sisi wenyewe zaidi na/au kuwaumiza wengine. Tunajikuta tukizalisha matatizo mengine ambayo kimsingi hatukuwa na sababu ya kuwa navyo, kwa sababu tu ya mtazamo.

Hasira, kukata tamaa, kuvunjika moyo, msongo wa mawazo na yote yanayofanana na hayo yanatupa ujumbe kwamba mwenye hayo anaamini kwamba yupo mtu, ama tukio, ama hali imemkosea! Hayo niliyoyataja huja kama matokeo ya mtazamo hasi. Huja kama matokeo ya tatizo letu wenyewe.

Sijui kama unajua kuwa matukio yote yatokeayo katika uasili wake hayana uzuri ama ubaya? Una habari kwamba mengi kama sio yote anayoyafanya mwanadamu katika asili yake hayana uzuri ama ubaya? Unajua kuwa jinsi mambo yalivyo/situations katika uasili wake hayana ubaya wowote ama uzuri?

Pengine utaniuliza swali la kifalsafa: uzuri ni nini na unatofautianaje na ubaya? Ni bahati mbaya kwamba mazungumzo yetu ya leo hayana mwelekeo huo. Hata hivyo katika mipaka ya mazungumzo ya leo, uzuri tutaufafanua kama hali ya kupendeza wakati ubaya ni kinyume chake.

Kwa hiyo, hakuna kilicho katika uasili wake chenye uzuri ama ubaya. Naipenda kanuni hii, kwamba jinsi mambo yalivyo, watu, na matukio vyote hivyo ni neutral, havina uzuri wala ubaya! Uzuri ama ubaya wake hututegemea sisi! Hiyo ina maana kwamba ni mtazamo wetu sisi ndio huyageuza matukio, watu ama vile mambo yalivyo (situations) kuwa ama mabaya ama mazuri.

Nikifikiri kwa mtindo huo (kwamba uzuri ama ubaya wa lolote unanitegemea mimi na na sio kitu ama tukio) sikosi kugundua kuwa vingi vya vile vinavyonikesesha raha, utulivu na amani yangu vingeweza kabisa kufanya kazi tofauti kama ningebadili tu namna ninavyovichukulia.

Hebu fikiria ni misongo mingapi ya mawazo tunaisababisha wenyewe? Mara ngapi tumekosa amani na kukata tamaa kwa sababu tu “ya mtazamo wetu wenyewe”? 
Mara ngapi tumejiumiza wenyewe kwa kuwawazia wapendwa wetu “ubaya” wasiokuwa nao kwa sababu tu tulijipa kazi ya “kuwabandika lebo ya ubaya”?

Najua yapo matukio ambayo kwa hali ya kawaida yanaweza kubadili kabisa “sripti” ya sehemu ya maisha yetu yaliyobaki. Matukio kama ya kufiwa na watu tuwapendao, kufukuzwa kazi na kadhalika. Lakini tunapotulia na kujibidiisha kubadili mitazamo yetu kwayo, twaweza kabisa kubaki na amani ya mioyo yetu na maisha yakaendelea! 


Watoto wadogo huonekana kuwa na furaha kuliko watu wazima kwa sababu nyingi. Moja wapo ni kutokujua ubaya wa vingi vinavyowazunguka. 
_______________________________________________________________________
Ipo orodha ndefu ya watu wanaotukosesha amani, tunaokosana nao kirahisi ama kukaripiana na kuvunjia heshima hadharani, ambao (kwa kubadili tu mitazamo yetu) tungeweza kabisa kuwapenda na kuishi nao kwa namna inayoweza kutushangaza sisi wenyewe!

Niliwahi kuishi na rafiki yangu mmoja siku za nyuma aliyekuwa na tabia za kunikera. Vingi vya alivyovipenda vilikuwa kinyume na yale yanayoitwa “maadili” yaani ethos. Majaribio ya mara kwa mara kuzungumza naye hayakusaidia kumbadili. Kila siku tuliyoishi naye ilioongezea hasira. 

Ilinichukua muda kukubali kuwa yule rafiki yangu hakupenda kuwa vile alivyo. Kwamba alichokuwa akikifanya kilikuwa msukumo ulio nje ya uwezo wake mwenyewe. Hakupenda kuwa vile na hata kuamini alikuwa sahihi. Ni kwa kutambua hivyo, nikabaini kuwa kujaribu kumbadili hakutawezekana. Nikabaini kuwa anayo haki ya kuwa yeye. Na ni makosa mimi kujaribu kumgeuza yeye awe mimi. 

Tangu kipindi kile, nilichokuwa nakiona awali kuwa kero kikabadilika kuwa sehemu ya maisha. Hatimaye nakumbuka ilikuja kuwa huzuni sana kuachana na rafiki yangu huyo tulipolazimika kutengana kimakazi. Kwa nini? Nilifanikiwa kubadili mtazamo wangu kwake na kusitisha “jaribio” la kumbadili yeye!

Huo ni mfano mdogo sana kutosha kukuelewesha namna ambavyo mara nyingi tatizo huwa kwetu tunaokwazwa, kuchukizwa na kuumizwa na wengine. Kwamba namna tunavyoyachukulia mambo huathiri sana “ubaya na uzuri wa jambo”.

Anza kuona uzuri wa watu wanaokuzunguka (hata kama itakubidi uutafute sana). Anza kuuchukulia udhaifu unaouona kwao kama tofauti baina yenu. Utashangaa.

Ni salama zaidi kuelewa kuwa mara nyingi watu hufanya mambo fulani kwa msukumo ulio juu ya uwezo wao. Msukumo huu ndani yetu hujengwa na vingi, kikubwa kikiwa ni mazingira tunayokutana nayo tangu dakika ile tunapozaliwa (malezi, dini/imani, marafiki nk) mpaka pale msukumo huo unapoota mizizi minene kiasi ya kutuongoza kutenda vile vinatenda!

Chukulia kuwa tofauti zetu si za hiari. Chukulia anayekuchukia hajapenda kukuchukia. Chukulia mengi ya yanayotokea kwa sababu ya uzembe wako, unayo nafasi ya kuyarekebisha. 

Kumbuka amani na furaha yetu vyatutegemea sisi. Tusiwategemee wengine kutufanya tufurahi. Tupunguze matarajio kwa wengine. Tusiruhusu watu wengine kutunyima amani. Wajibu wa kujipa ama kujioondolea amani hauko kwa mwingine isipokuwa sisi. Uamuzi ni wetu wenyewe.

Comments