MSAMA PROMOTION YAKANA KUIPA BASATA SH. MILIONI 6
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Msama Promotion inayoandaa masha la Pasaka, imekanusha kulipa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), sh. milioni 6, kama ada a wasanii wanaoingia nchini kufanya maonesho mbalimbali.
Habari hizo zilizoandika na gazeti moja litokalo kila siku (jina tunalo), siyo za ukweli, hivyo ameliomba msamaha baraza hilo kwa usumbufu uliojitokeza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alisema kuwa, kampuni yake haijatoa fedha hizo zinazodaiwa ni ada ya wasanii wanaokuja nchini kushiriki tamasha hilo.
Msama alisema katika tamasha lililofanyika mwaka jana mgeni rasmi akiwa Rais Jakaya Kikwete, waliomba kupunguziwa gharama za ada hiyo, jambo lililofanyiwa kazi na BASATA.
"Mwaka jana tuliomba kwa Rais Kikwete, atusaidie kupunguza gharama za ada za kuwaleta wasanii, ombi letu lilikubaliwa na likafanyiwa kazi, hivyo hatujapeleka fedha hizo BASATA kama ilivyoripotiwa na gazeti moja la kila siku (jina tunalo)," alisema.
Msama alisema baada ya serikali kupitia baraza hilo kufuatilia kwa makini kazi za kampuni hiyo na kubaini mchango mkubwa wanaotoa kwa vikundi mbalimbali, waliamua kufanyia kazi maombi yote.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa, BASATA lilifuatilia na kushuhudia kampuni hiyo kupitia tamasha la Pasaka wakitoa misaada mbalimbali zikiwemo baiskeli kwa walemavu, mitaji kwa wajane na kuwasomesha watoto yatima.
Tamasha la Pasaka mwaka huu limepangwa kufanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam likiwashirikisha waimbaji wa ndani na nje ya nchi.
Waimbaji kutoka nje ya nchi ni Rebecca Malope kutoka Afrika Kusini, Maryanne Tutuma, Solomon Mukubwa na Anastazia Mukabwa wote kutoka Kenya.
Kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) ni Faraja Ntaboba na Ephraim Seleketi kutoka Zambia.
Msama ameliomba msamaha baraza hilo kwa usumbufu uliojitokeza baada ya habari hiyo kuchapwa katika gazeti hilo, huku akisisitiza kuwa, suala hilo si la kweli.
Msama alisema baada ya maombi yao kusikilizwa na kufanyiwa kazi, serikali kupitia BASATA lilipunguza ada za wasanii kutoka nje na kuwataka kulipa ada ya pamoja ambayo imepunguzwa kwa kiasi kikubwa.
Source: fullshangweblog.com
Comments